Monday 31 October 2016

JPM: WATANZANIA NA WAKENYA NI NDUGU



NA MWANDISHI MAALUMU, NAIROBI

RAIS Dk. John Magufuli amesema Kenya ni nchi inayoongoza kwa uwekezaji hapa Tanzania ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika.

Dk. Magufuli alisema hayo jana, katika mkutano na waandishi wa habari, uliofanyika Ikulu ya Nairobi nchini Kenya, ambako ameanza ziara ya kiserikali ya siku mbili kwa mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, Uhuru Kenyatta.

Rais Dk. Magufuli kabla ya mkutano huo na waandishi wa habari, alipokelewa rasmi kwa kupigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride rasmi lililoandaliwa kwa heshima yake na baadaye kufanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake, Rais Kenyatta.

Alisema takwimu za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) zinaonyesha kuwa, Kenya inazo kampuni 529, zinazoendesha shughuli zake nchini, ambapo zimewekeza Dola za Marekani bilioni 1.7 na zimeajiri watu 56,260.

Aidha, Rais Magufuli alibainisha kuwa, biashara kati ya Tanzania na Kenya, imeongezeka kutoka sh. bilioni 652.9 za Tanzania hadi sh. trilioni 2.044.

"Naomba niwahakikishie kuwa uhusiano na ushirikiano wetu ni mzuri na utaendelea kuwa mzuri zaidi na kwetu sisi Tanzania, Kenya ndio nchi ya kwanza kwa uwekezaji kuliko nchi zote za Afrika.

"Tunashirikiana vizuri katika uchumi, watu wetu wanafanya kazi pamoja, yapo makabila yetu, ambayo yanaingiliana kwa shughuli zao za kila siku na hata wanyamapori wetu wanazunguka katika nchi zote mbili bila kujali mipaka,"alisema Rais Magufuli.

Dk. Magufuli alisisitiza kuwa serikali yake itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano na Kenya, ulioasisiwa na Rais wa Kwanza wa Tanzania Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa Kwanza wa Kenya, Hayati Mzee Jomo Kenyatta na amewakaribisha wafanyabiashara wengi zaidi wa nchi hiyo kuwekeza Tanzania.

"Kabla ya kuja hapa nimekwenda kutoa heshima katika kaburi la Mzee Jomo Kenyatta, kwa kweli nimeguswa sana na kazi kubwa iliyofanywa na wazee wetu, naomba niwahakikishie kuwa tunawathamini sana ndugu zetu Wakenya na tutaendelea kufanya hivyo,"alisisitiza Dk. Magufuli.

Kwa upande wake, Rais Kenyatta alimshukuru Rais Magufuli kwa kukubali mwaliko wake na kumhakikishia kuwa Kenya itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano na Tanzania.

"Kwetu Tanzania ni ndugu zetu, ni kaka na dada zetu, tunao ushirikiano wa siku nyingi na wa kindugu na tutahakikisha tunauendeleza ushirikiano na uhusiano huu mzuri ulioasisiwa na wazee wetu,"alisema Rais Kenyatta.

Rais Kenyatta alisema Tanzania na Kenya ni nchi zinazofanana kwa mambo mengi muhimu, ikiwemo kubadilishana uongozi wa serikali kwa njia ya amani na kuongeza kuwa, katika mazungumzo yao, wamekubaliana nchi hizo zitaendelea kuzisaidia nchi nyingine za Afrika Mashariki zinazokabiliwa na matatizo mbalimbali.

Rais Kenyatta pia alisema Kenya itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza miradi ya ushirikiano, ikiwemo ujenzi wa miundombinu kama barabara ya Bagamoyo (Tanzania) hadi Malindi (Kenya) pamoja na mambo mengine, ambayo Tume ya pamoja ya ushirikiano kati ya nchi hizo itayaainisha.

Rais Magufuli, jana jioni, alitarajiwa kuhudhuria dhifa ya kitaifa katika Ikulu ya Nairobi, aliyoandaliwa na mwenyeji wake, Rais Kenyatta.

Leo anatarajiwa kutembelea kiwanda cha maziwa cha  Eldoville kilichoko Karen, Jijini Nairobi na  kuzindua barabara mchepuko ya Southern By-pass, iliyoko jijini hapa.

Wakati akiondoka nchini jana, Dk. Magufuli, aliagwa na viongozi mbalimbali wa serikali, akiwemo Makamu wa Rais,  Samia Suluhu Hassan, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na viongozi mbalimbali wa vyombo vya ulinzi na usalama.

No comments:

Post a Comment