Monday, 31 October 2016
PIKIPIKI TANO ZA UVCCM ZATOWEKA
WAKATI Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dk. John Magufuli, akiagiza mali za Chama na jumuia zake zihakikiwe upya na kuhakikisha zinatumika kwa manufaa ya Chama, pikipiki tano za Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) jijini hapa, hazijulikani zilipo.
Pikipiki hizo, mbili aina ya Suzuki, zilizonunuliwa na makao makuu ya umoja huo pamoja na nne, aina ya Sanlag, zilizotolewa msaada na mjumbe wa zamani wa Baraza Kuu la UVCCM Taifa, kutoka mkoani Mwanza, Balnabas Mathayo.
Mbali na vyombo hivyo vya usafiri, fedha za kodi ya pango za kiwanja cha UVCCM, kilichoko Kata ya Mabatini, wilayani Nyamagana, zinadaiwa kutafunwa na kigogo mmoja wa jumuia hiyo.
Vyanzo vyetu mbalimbali vya habari vimeeleza kuwa, baadhi ya pikipiki hizo zinatumiwa kama bodaboda katika maeneo ya Kata ya Mabatini, wilayani Nyamagana na nyingine kudaiwa kuuzwa huku moja ikiwa imetelekezwa gereji, ikiwa kwenye hali mbaya.
“Ni kweli Suzuki mbili za Nyamagana na Ilemela zilizonunuliwa na makao makuu ya UVCCM pamoja na Sanlag nne, mbili za Nyamagana na mbili za Ilemela, hazijulikani zilipo.Tunasikia baadhi zimekodishwa na kiongozi wetu mmoja na nyingine kuuzwa bila taarifa,”alieleza mjumbe mmoja wa UVCCM wilayani Ilemela bila kutaka jina lake litajwe kwa kuwa siyo msemaji.
Kiongozi mwingine wa wilaya ya Nyamagana, ambaye pia hakutaka aandikwe gazetini, alisema habari hizo ni za kweli na makatibu wapya wa UVCCM waliokuja katika wilaya hizo, wanahaha kuzisaka bila mafanikio.
“Wala siyo pikipiki tu, hata kiwanja chetu cha Mabatini, kimepangishwa na kigogo mmoja na fedha zake analipwa yeye,” alisema kiongozi huyo na kudai mmoja wa wahusika wa ubadhirifu wa mali za vijana kwa sasa yuko wilayani Ukerewe.
Akizungumzia suala hilo, Katibu wa UVCCM wilayani Ilemela, Benedicto Bujiku, alisema hawezi kulitolea maelezo kwa sasa, isipokuwa ieleweke kuwa hajakabidhiwa pikipiki hizo tangu aanze kazi Mwanza siku chache zilizopita.
“Tunahaha kuzisaka, lakini siwezi kuzungumzia suala hilo hivi sasa, waliokupa taarifa wanaweza kukusaidia zaidi mimi ni mgeni,” alieleza Bujiku kwa njia ya simu, baada ya kutafutwa kwa muda mrefu.
Kwa upande wake, Katibu wa UVCCM wilayani Nyamagana, Odlian Batromayo, hakuweza kupatikana kuelezea madai hayo.
Mathayo alieleza kusikitishwa na baadhi ya viongozi wa UVCCM wanaotuhumiwa kutumia pikipiki alizotoa kwa ajili ya kuwakwamua vijana huku akisema alitoa msaada huo uwe kama nyavu ili wasimuombe samaki.
Mjumbe huyo wa zamani wa Baraza la UVCCM Taifa, alitoa pikipiki aina ya Sanlag tano kwenye wilaya mbalimbali za mkoa wa Mwanza, zikiwemo Sengerema na Ukerewe mwaka 2014, huku Suzuki moja moja ikitolewa na makao makuu ya umoja huo mwaka 2010.
Agosti, mwaka huu, Rais Dk. Magufuli akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Mwanza, aliagiza mali za CCM na jumuia zake zihakikiwe na kutaka zitumike kunufaisha wanachama wote na siyo kushibisha matumbo ya baadhi ya watu, hususan viongozi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment