Monday, 31 October 2016

TEF YASISITIZA MUDA UONGEZWE KUJADILI MUSWADA WA HABARI

JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF), limesisitiza kutaka kupatiwa muda kujadili Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari nchini, ili kutoa maoni yatakayowezesha kutungwa kwa sheria yenye kuzingatia maslahi ya taaluma ya uandishi wa habari.

TEF imeeleza kuwa, bado muswada huo una mapungufu ya kisheria yanayopaswa kupatiwa muda zaidi kujadiliwa na kufanyiwa marekebisho, hivyo endapo serikali isipozingatia ushauri huo, jukwaa hilo halitakuwa sehemu ya sheria itakayowasilishwa bungeni, Novemba, mwaka huu.

Msimamo huo wa TEF umetolewa baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Peter Selukamba, kusema kuwa, bunge litaendelea na mchakato wa kutunga sheria hiyo hata kama baadhi ya wadau wameshindwa kutoa maoni yao.

Akizungumza Dar es Salaam, jana, Mwenyekiti wa TEF, Theophil Makunga, alisema sheria hiyo inayokusudiwa kutungwa bado ina masuala kadhaa, ambayo hayahitaji uharaka katika kuyafanyia uamuzi.

“Masuala haya yanahitaji mjadala mpana wa wanataaluma na wadau wengine, kwani kuomba muda zaidi kulilenga kutoa fursa kupatikana kwa maoni, ambayo yangeweza kuongeza thamani katika sheria husika,” alisema.

Makunga alisisitiza kuwa, kwa hatua iliyopo, bado mchakato wa majadiliano na utoaji mapendekezo katika ngazi za taasisi za waandishi wa habari, haujakamilika.

Alieleza kuwa wamelazimika kuomba muda zaidi kwa sababu kazi ya kusoma na kuchambua muswada huo, imechukua muda mrefu kuliko walivyotarajia kwa sababu ya kuwepo kwa masuala yenye kuhitaji mjadala mpana zaidi.

Baada ya kuwasilisha maombi hayo, alisema Kamati ya Bunge iliwaarifu kwa maandishi kuwa, ombi hilo limekubaliwa hivyo walitakiwa kuwasilisha maoni yao Oktoba 26, mwaka huu.

“Hata hivyo, baadae tulitumiwa ujumbe kuwa barua hiyo tuipuuze kwani tungetumiwa mwaliko mwingine utakaowaeleza siku nyingine, lakini Alhamisi, Oktoba 27, tulipokea barua nyingine ikieleza maombi yetu ya kuongozewa muda yamekamilika, hivyo tulitakiwa juzi tufike Dodoma au kutoa maoni kupitia barua pepe.

“Tumeshindwa kwenda Dodoma wala kutuma maoni maana hatukuweza kukamilisha mchakato kama tulivyosema mbele ya kamati wakati tulipoitwa mara ya kwanza,” alieleza.

Makamu Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, alisema TEF haiogopi wala kuikataa sheria hiyo, bali inapaswa kutungwa kwa kuzingatia misingi ya utungaji sheria.

Alisema bado kuna vipengele vya kisheria vinavyoiweka tasnia ya uandishi wa habari kuwa ngumu zaidi, hivyo kunahitajika kuwepo kwa mjadala mpana kabla ya kutungwa kwake.

No comments:

Post a Comment