Monday, 31 October 2016

WANAFUNZI WASIO NA SIFA KUSITISHIWA MIKOPO


BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, itaanza kufanya uhakikiwa wa taarifa za wanufaika wa mikopo wanaoendelea na masomo na watakaobainika hawana sifa stahiki, watasitishiwa mikopo na kutakiwa kuzirejesha fedha walichokwisha pokea.

Hivyo bodi hiyo imewataka wanafunzi kujaza taarifa za kiuchumi za wazazi au walezi wao, kwenye dodoso maalumu ndani ya siku 30, kuanzia Novemba, mwaka huu.

Uhakiki huo ni mkakati wa kubaini wanafunzi, ambao licha ya kutokuwa na sifa za kupata mkopo, wameendelea kunufaika na fedha hizo, hivyo kusababisha wanafunzi stahiki kukosa.

Aidha, bodi hiyo imesisitiza kuwa, utoaji mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu utazingatia vipaumbele vya kitaifa, wanafunzi wanaotoka kwenye familia masikini, yatima na walemavu.

Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam, jana, Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Abdul-Razaq Badru, alisema upangaji wa mikopo kwa mwaka huu wa masomo, umezingatia bajeti iliyotengwa na serikali ya sh. bilioni 483.

Alisema fedha hizo zimetengwa kuwakopesha wanafunzi 119,012, kati yao 25,717 wa mwaka wa kwanza na 93,259, wanaoendelea na masomo kwenye vyuo mbalimbali.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, hadi sasa wanafunzi 20,319, wamepata mikopo kwenye awamu ya kwanza, kati yao yatima 4,321, wenye ulemavu 118, wanaosoma kozi za kipaumbele 6,156, wanaofadhiliwa kutoka taasisi mbalimbali 295 na wanafunzi wanaotoka kwenye familia duni 9,498.

Badru alibainisha kuwa wanafunzi 27,053, hawakupangiwa kupata mikopo kwa sababu mbalimbali, kati yao wanafunzi 6,581, hawakuomba mkopo, 8,781 ni wahitimu binafsi, 9,940 walifuzu kwa vigezo wianishi.

Wengine ni 1,416, ambao wameshindwa kukamilisha maombi yao, 245 waliohitimu kidato cha sita zaidi ya miaka mitatu na wadahiliwa 90, hawakupewa mkopo kwa sababu ya kuwa na umri zaidi ya miaka 30.

“Baada ya uchujaji huo, idadi ya waombaji wenye sifa stahiki ilipungua hadi 30,957, ambao waliingizwa kwenye mfumo wa kuchakata na kupanga mikopo kwa mujibu wa sifa na vigezo vilivyowekwa,” alieleza.

Alisema kuanzia Novemba 2, mwaka huu, bodi hiyo itaanza kupokea rufani za waombaji, ambao hawakuridhika na matokeo ya upangaji wa mkopo awamu ya kwanza.

Uhakiki huo wa wanafunzi ni muendelezo wa serikali katika kukabiliana na ubadhirifu wa fedha hizo, ambazo zimekuwa zikiishia mikononi mwa wanafunzi wasiostahiki.

Agosti 17, mwaka huu, Waziri wa Elimu, Sayansi na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, alitoa siku saba kwa vyuo vikuu kurejesha fedha vilizopokea, ambazo ni za wanafunzi, ambao hawapo chuoni.

Profesa Ndalichako alichukua hatua hiyo baada ya kubainika kuwepo kwa wanafunzi hewa wanaopokea fedha za mikopo ya elimu ya juu.

Ndalichako alisema uhakiki wa wanafunzi hao umefanyika katika vyuo 31 kati ya vyuo 81, vilivyopo nchini, ambapo ilibainika wanafunzi 2,192, wameshindwa kuhakiki majina yao, hivyo kushindwa kuthibitisha uwepo na uhalali wa wanafunzi hao.

Kwa mwaka wa fedha 2015/16, wanafunzi hao hewa wameigharimu serikali zaidi ya sh. bilioni tatu, kiasi ambacho kinatakiwa kurejeshwa na vyuo ambavyo wanafunzi hao wamebainika.

Tyari serikali imeshaanza kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwa mwaka huu wa masomo, ambapo zaidi ya asilimia 90 ya wanafunzi hao wanaostahili, wameshaingiziwa fedha hizo kupitia vyuoni.

Katika maadhimisho ya miaka 55 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka huu, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema serikali inatambua changamoto zilizopo, ikiwemo madai ya malimbikizo ya mishahara kwa watumishi, hususan baada ya kuanza kwa muundo wa pamoja wa wanataaluma wa vyuo vikuu vya umma.

Alisema serikali itaendelea kuweka kipaumbele kwa upatikanaji wa fedha za kutosha kwa ajili ya mafunzo huku vyuo hivyo vikiweka taratibu za kurithishana nafasi.

“Pia nimekuwa nikipata malalamiko juu ya vyuo kutopata fedha za kutosha za uendeshaji (OC) na hivyo kuathiri utoaji wa taaluma. Serikali hii imeamua kuimarisha ukusanyaji mapato ya ndani ili iweze kumudu majukumu ya uendeshaji wa serikali bila kutegemea  wafadhili,”alisema.

Licha ya kauli hiyo, Rais Dk. John Magufuli alishatoa ufafanuzi wa namna ya kutekeleza utoaji mikopo kwa kuitaka Wizara ya Elimu kuendelea kufanya uhakiki wa taarifa za waombaji.

No comments:

Post a Comment