Wednesday, 31 August 2016

CHADEMA YAFUTA MAANDAMANO YA UKAWA


HATIMAYE Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, ametangaza kusitisha maandamano ya UKUTA, akidai kupisha mazungumzo baina ya viongozi wa dini  na serikali.

Akitangaza msimamo huo jana, mbele ya waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam, Mbowe alidai wamepata wakati mgumu kufikia uamuzi huo, kwa kuwa sio kila wakati viongozi watafanya mambo yatakayowapendeza wanachama.

Alisema viongozi wa dini, awali walikwenda na ajenda moja ya kuomba wabunge wa UKAWA warejee bungeni na Kamati Kuu ya CHADEMA ilipokea kwa heshima wito wa viongozi hao.

"Ni matumaini yangu kuwa wana- CHADEMA watatuelewa kamati kuu, asanteni sana kwa kunisikiliza,''alisema Mbowe katika mkutano aliozungumza kwa muda mfupi sana.

Katika mkutano huo, Mbowe alionekana kulalamika huku akishindwa kujibu maswali ya waandishi wa habari, waliomtaka atoe ufafanuzi wa maswali, hasa kuhusiana na kesi walizoshindwa mahakamani.

"Mimi ni miongoni mwa watu tuliotamani kesho (leo) watu wawe barabarani, wanachama wetu, ambao watakwazika UKUTA si CHADEMA, UKUTA ni mchanganyiko wa makundi ya Watanzania, sasa hayo makundi yamekuja kutushauri tuwe pamoja,"alisema.

Kwa mujibu wa Mbowe, miongoni mwa watu waliowafuata na kuzungumza nao ni Taasisi ya Mwalimu Nyerere huku akidai kuwa, mgombea wao wa Urais, Edward Lowassa, amezungumza na Mama Maria Nyerere na amewasihi wasifanye maandamano, hivyo wamefikia uamuzi wa kusitisha maandamano hayo.

No comments:

Post a Comment