WATU wanne, wakiwemo mwanafunzi na mwandishi wa habari,
wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwa tuhuma za
kujitambulisha kwa kutumia jina la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Pia, washitakiwa hao wanadaiwa kughushi barua zisizo na
tarehe kuonyesha zimetoka Ofisi ya Rais, Ikulu, zikielekeza kampuni mbalimbali
kuingiza sh. milioni 25, katika akaunti zilizopewa ili ziweze kupata punguzo la
kodi.
Washitakiwa katika kesi hiyo ni mwanafunzi Issa Awadh au
Charles Mwamunyange au Trah Rio Mwenge (29), mtengeneza mihuri, Nicolaus Obado
(32), mtangazaji, mwandishi wa habari na mfanyabiashara, Hamis Tembo (37) na mfanyabiashara
Wakati Mungi (51).
Obado, Tembo na Wakati walipandishwa kizimbani
mahakamani hapo jana, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, ambapo Wakili
wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi kwa kushirikiana na Wakili wa Serikali
Mwandamizi, Pamela Shinyambala, waliwasomea mashitaka.
Kabla ya kuanza kusomewa mashitaka kwa washitakiwa hao
watatu, Wakili Nchimbi alidai mshitakiwa Awadh, amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH),
hivyo aliomba mahakama kuhamia hospitalini hapo kwa ajili ya kumsomea mashitaka
yanayomkabili.
Akiwasomea mashitaka washitakiwa waliokuwepo mahakamani
hapo, Pamela alidai washitakiwa wote wanne kwa pamoja tarehe isiyofahamika,
kati Machi 10 na 17, mwaka huu, sehemu tofauti wilayani Ilala, mkoani Dar es
Salaam, walikula njama kutenda makosa ya kughushi na kujipatia fedha kwa njia
ya udanganyifu.
Awadh, Obado, Tembo na Wakati wanadaiwa katika kipindi
hicho, sehemu tofauti mkoani Dar es Salaam, kwa pamoja walijitambulisha wao ni
Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu huku wakijua si kweli.
Kuanzia shitaka la tatu hadi la 11, washitakiwa hao
wanadaiwa katika kipindi hicho, mkoani humo, walighushi barua mbalimbali zisizo
na tarehe, kuonyesha ni halali, zimetoka ofisi ya Rais, Ikulu zikiwaelekeza
wakurugenzi wa kampuni kuingiza sh. milioni 25 kila mmoja katika benki ya ABC,
kwenye akaunti namba 1801833619, yenye jina la TRA. HR. MWENGE ili kupata
punguzo la kodi, wakati wakijua si kweli.
Washitakiwa hao wanadaiwa kughushi barua hizo
kuzielekeza kwa wakurugenzi wa kampuni za Usangu Logistics, Bakhresa and
Company Limited, IPP Media, Oil Com, GAPCO Limited, Lake Oil CO Tanzania
Limited na PUMA Company Limited.
Shitaka la 11, linamkabili Awadh, ambaye anadaiwa Machi
17, mwaka huu, katika ofisi za kampuni ya Usangu Logistics, aliwasilisha kwa mtu wa mapokezi nyaraka za uongo, ambazo ni
barua isiyokuwa na tarehe, kuonyesha kwamba ofisi ya Rais, ikimuelekeza
mkurugenzi wa kampuni hiyo, kuingiza fedha hizo katika akaunti hiyo ili aweze
kupata punguzo la kodi kwa kampuni hiyo.
Awadh na Tembo wanadaiwa Machi 10, mwaka huu, katika ofisi
ya TSN Foundation, iliyoko wilayani Ilala, Dar es Salaam, kwa pamoja kwa nia ya
udanganyifu, walijipatia Dola za Marekani 1,000, kutoka kwa Farough Ahmad au
Bagozah, baada ya kudanganya kwamba fedha hizo ni kwa ajili ya kudhamini masomo
ya Awadh huko Marekani.
Tembo, Wakati na
Obado walikana mashitaka, ambapo Nchimbi alidai upelelezi haujakamilika, hivyo
aliomba shauri kuahirishwa hadi tarehe nyingine kwa kutajwa, na mahakama izuie
dhamana za washitakiwa hao kwa muda kwa madai ya kwamba, iwapo watakuwa nje,
kuna hatari ya kuingilia upelelezi kwa namna unavyofanywa.
Kwa upande wao, washitakiwa waliomba mahakama iwapatie
dhamana. Hata hivyo, Hakimu Simba alikubaliana na ombi la upande wa Jamhuri na
kusema maombi yao yana msingi kwa kipindi hiki cha upelelezi, hivyo washitakiwa
watabaki rumande hadi hapo upelelezi utakapokamilika.
Hakimu Simba alitoa rai kwa upande wa Jamhuri
kukamilisha upelelezi haraka na kuahirisha shauri hilo hadi Aprili 11, mwaka
huu, kwa kutajwa.
Baada ya kuwasomea washitakiwa hao mashitaka, mahakama
hiyo ilihamia Hospitali ya Taifa Muhimbili, kwa ajili kumsomea mashitaka Awadh.
Awadh alikana mashitaka, ambapo upande wa Jamhuri
uliomba anyimwe dhamana kama wenzake. Hakimu alikubaliana na ombi hilo.
No comments:
Post a Comment