Tuesday, 24 May 2016
SILAA: WAFUASI CHADEMA WALITISHIA KUICHOMA NYUMBA YANGU
ALIYEKUWA mgombea ubunge wa Jimbo la Ukonga, Jerry Silaa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), amedai wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), walimtishia kuichoma moto nyumba take wakati wa uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka jana.
Jerry, alidai hayo jana, katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, alipokuwa akitoa ushahidi wake kwa njia ya kiapo, katika kesi ya uchaguzi aliyoifungua kupinga ushindi wa mbunge wa jimbo hilo, Mwita Waitara.
Shauri hilo lilianza kusikilizwa mbele ya Jaji Fatuma Masengi, baada ya kutolewa uamuzi wa kutupiliwa mbali pingamizi la awali lililowasilishwa na walalamikiwa katika shauri hilo kwa madai ya kwamba, ushahidi wa Jerry wa maandishi una upungufu.
Jerry, anayewakilishwa na Wakili Dk. Masumbuko Lamwai, alidai Oktoba 26, mwaka jana, kuanzia asubuhi hadi saa sita 6 usiku, alishinda kwenye kituo cha kujumuishia matokeo Pugu Sekondari.
Hata hivyo, alidai hakukuwa na chochote kilichoendelea, hadi msimamizi wa kituo alipowatangazia waondoke kwa sababu kuna baadhi ya vituo vilikuwa havijamaliza kukusanywa kura na Oktoba 27, idadi ya wapigakura wa CHADEMA iliongozeka huku wakiwa wamesimama mita 20, kutokea usawa wa kituo cha majumuisho.
Alidai wafuasi hao walianza kuwatishia mawakala na msimamizi wa kituo, hivyo polisi waliwaonya na mjibu maombi wa pili na wenzake walisema hawatapokea majibu ya kupigakura na pia watachoma moto nyumba yake pamoja na kituo chenyewe.
Alidai hadi kufikia Oktoba 27, mwaka jana, baadhi ya vituo vilikuwa havijakusanywa kura, jambo lililosababisha aandike barua kwenda kwa msimamizi wa kituo, akimuomba mchakato wa kuhesabu kura urudiwe.
Alidahi kuwa hadi kufikia saa 10 jioni ya Oktoba 27, msimamizi wa kituo alizungumza na mlalamikiwa wa pili (Waitara), kisha baadaye kutangaza kuwa hawezi kurudia mchakato wa kuhesabu kura na kutokana na mvutano huo, timu yake iliyokuwa maeneo hayo, ilikataa, jambo lililosababisha mabishano, ambapo ndani ya tarehe hiyo, CHADEMA walisababisha fujo, ikiwemo kuchukua fulana za mawakala.
Alidai wakati huo huo, msimamizi wa kituo alianza kuingiza matokeo ya uchaguzi, licha ya kuwa fomu B 21 zilikuwa hazijafika kituoni hapo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment