Tuesday, 24 May 2016

BILIONI 15 ZATENGWA KUWAONGEZEA UJUZI VIJANA


JUMLA ya sh. bilioni 15, zimetengwa na serikali kwa ajili ya kuongeza ujuzi kwa vijana wa Tanzania ili waweze kujiajiri na kuajiriwa katika viwanda vitakavyoanzishwa nchini.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Jenister Mhagama, alisema hayo bungeni jana, wakati akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Josephine Chagula.

Mbunge huyo alitaka kujua serikali itawasaidiaje vijana kupitia kuongeza ujuzi ili waweze kujiajiri.

Jenister alisema fedha hizo zimetengwa kupitia ofisi ya waziri mkuu kitengo cha vijana, katika mwaka huu wa fedha ili kuwasaidia vijana, ambapo zitatumika kwa makusudi ya kuwaongezea ujuzi.

Naye Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, alisema jukumu la Shirika la Viwanda Vidogo nchini (SIDO) ni kutoa elimu na mafunzo ya ujuzi bure.

Alisema serikali inatoa pesa kwa shirika hilo ili kuwawezesha kuendesha na kutoa mafunzo hayo kwa jamii, ikiwemo vijana wa kitanzania.

Mwijage alitumia nafasi hiyo kuwataka wabunge pamoja na watanzania wote kufika SIDO ili waweze kupatiwa mafunzo hayo kwa fedha zinazotolewa na serikali.

Katika swali la msingi, mbunge huyo alitaka kujua serikali ina mpango gani wa kujenga viwanda vya kusindika mazao katika mkoa wa Geita.

Mwijage alisema kwa kutambua umuhimu wa viwanda katika kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi, wizara hiyo kupitia mkakati unganishi wa maendeleo ya viwanda, umebuni mradi huo kwa lengo la kuhamisha wananchi na wadau kuwekeza katika kuanzisha viwanda.

Alibainisha kuwa wizara kupitia SIDO, itaendelea kushirikiana na wadau mkoani Geita, kuibua miradi kupitia programu ya wilaya moja, bidhaa moja, kwa lengo la kuanzisha na kukuza viwanda katika ngazi ya wilaya na hivyo kuleta ajira vijijini.

Pia, alisema wizara inamfuatilia mwekezaji, ambaye ni bingwa wa kutengeneza juisi, anayeshika kati ya namba 5-7 duniani ili ajenge kiwanda Geita.

No comments:

Post a Comment