Tuesday, 24 May 2016
CCM YAIBOMOA CHADEMA MOROGORO
ZIARA ya Naibu Katibu wa Oganaizesheni na Siasa ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), mkoani Morogoro, Pili Agustino, imeleta maumivu makubwa kwa CHADEMA na UKAWA, baada ya wafuasi wake kumiminika kuhamia CCM, wakiwemo vigogo.
Miongoni mwa watu tegemeo walioihama CHADEMA na kujiunga na CCM, ni Steven Daza, ambaye katika uchaguzi mkuu uliopita, alitangaza nia ya kuwania ubunge kupitia UKAWA na kushika nafasi ya pili katika kura za maoni.
Daza, ambaye alikuwa mwiba kwa CCM wakati wa kampeni, hatimaye aliamua kubwaga manyanga juzi na kutaja sababu kuwa ni kutokana na kuukubali utendaji uliotukuka wa Rais Dk. John Magufuli, hali iliyomfanya afute fikra potofu kwamba mabadiliko hayawezi kutoka ndani ya CCM.
“Nawaomba radhi wana Morogoro kwa sababu nikiwa CHADEMA, nilifundishwa kutukana matusi, kufanya fujo, kulazimisha maandamano na kutumia watu kama mpira wa kiume yaani kondomu. Nimerejea nyumbani CCM, naomba mnipokee, mnilee nami niweze kuwa mtu makini,”alisema Daza.
Aliongeza:”CCM ni chama makini, ambacho kiliangalia kushoto, kiliangalia na kulia, kikaangalia nyuma na kikaangalia mbele, kikamchagua mtu makini, jemedari wa kweli, si mwingine bali ni John Pombe Magufuli. Nataka niwaambie, huyu jamaa ni noma, alinifanya tangu achaguliwe nikose usingizi, nikihangaika jinsi ya kujiunga na kurudi ndani ya Chama Cha Mapinduzi.”
Alisema hayuko peke yake, wapo wengi ndani ya UKAWA, ambao waliamini kwamba mabadiliko hayawezi kutoka ndani ya CCM, lakini hivi sasa gurudumu limebadilika na wanaamini mabadiliko ya kweli yanatoka ndani ya CCM, kutokana na kazi kubwa anayoifanya Rais Magufuli.
“Kipindi hicho tuliambiwa mabadiliko yanatoka ndani ya UKAWA, lakini baadaye tukaambiwa mabadiliko yanaletwa na mtu, Lowassa (Edward).Tunataja jina la mtu. Lakini mpambanaji wa kweli ni Magufuli, amenisuuza kwa utendaji wake, nimeamua kurudi ndani ya Chama. Muda wa kuvaa gwanda umekwisha na hivi sasa kila kitu mbele kwa mbele. Kila mtu sasa hivi anaona kinachotokea,”alisema.
Alisema wakati wa kutumia watu kama mpira wa kiume, umekwisha na Watanzania waamke, hasa walioko upinzani kwani vyama hivyo vinawapotezea muda.
Akimkabidhi kadi ya CCM , Pili alisema ni wakati kwa vijana walioko upinzani kurejea ndani ya Chama, kwani kuna mabadiliko makubwa yanakuja.
“Wanaohitaji kurudi warudi ndani ya CCM tutawapokea. Tumedhamiria kuleta mabadiliko makubwa ya maendeleo na kuhakikisha kwamba, Ilani ya CCM inatekelezwa ipasavyo kwa manufaa ya wote,”alisema Pili.
Aliupongeza uongozi wa CCM na UVCCM kwa kazi kubwa waliyoifanya kwa kukiletea Chama ushindi wakati wa uchaguzi mkuu.
Kaimu Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro, Kulwa Milonge, alimhakikishia Pili kwamba, Chama mkoani humo kiko timamu na kumpongeza Daza kwa kuhamia katika chama makini.
Katibu wa UVCCM Mkoa wa Morogoro, Issaki Ole Kalleiya, alisema jumuia hiyo imejipanga kikamilifu katika kuleta mageuzi ya kweli ndani ya Chama, kwa kuhakikisha inakuwa tanuru la kuoka vijana watakaoshika hatamu katika nafasi mbalimbali za uongozi.
“Tumedhamiria na tumejipanga kikamilifu kuwaletea maendeleo wananchi wetu. Tunawaomba wananchi wamuunge mkono Rais Dk. Magufuli kwa kila hatua njema anayofanya ili tuweze kuneemeka na matunda ya nchi hii.
"Sisi UVCCM tumeamka na tutahakikisha kwamba mtendaji yeyote, ambaye atajaribu kuhujumu utekelezaji wa Ilani yetu, tutamfichua na kumtumbua jipu,”alisema Ole-Kalleiya.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment