Tuesday, 24 May 2016

CCM ITASHINDA UCHAGUZI KWA MIAKA 100 IJAYO-MALECELA

WANACHAMA wa CCM wametakiwa kutembea kifua mbele licha ya kuwepo kwa vyama vya upinzani kwani kinaweza kushinda uchaguzi kwa miaka 100 ijayo.

Kauli hiyo ilitolewa juzi na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM,
Samuel Malecela, alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa vyuo vikuu kuhusiana na matumizi ya mitandao katika siasa.

Malecela alisema hali ya CCM kuendelea kushika dola inajionyesha wazi kutokana na utaratibu iliyojiwekea.

Alisema hakuna chama ambacho kina mfumo mzuri wa uongozi hadi ngazi za chini za wananchi kama CCM.

"Hakuna sababu ya kuogopa wana CCM, mimi naamini bado CCM ina nguvu kubwa na itaongoza dola nchini hata kwa miaka 100 ijayo.

"Hao walioungana na kujiita UKAWA hawana jipya kwani hata CCM ni muunganiko wa vyama vya ASP na TANU, lakini walikubaliana kuvunja uongozi wa vyama hivyo wa juu na kuunda upya, mbona wao wanashindwa," alihoji Malecela.

Makamu huyo mstaafu aliwataka vijana kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Chama ili kiwe na damu na mawazo mapya.

"Ili chama kiweze kuendelea, ni lazima kuwepo na mawazo mapya kila wakati, huko ndiko kukifanya chama kiwe endelevu,"alisema.

Mwenyekiti huyo mstaafu pia aliwataka vijana hasa wa vyuo vikuu kutoingiwa na hofu na mitandao ya kijamii katika kukisema chama.

Malecela alisema mitandao ni moja ya nyezo ya kupata taarifa mbalimbali, lakini ni vyema ikawekewa utaratibu wa kuitumia.

Kwa upande wake, Mbunge wa Dodoma Mjini, Antony Mavunde (CCM), akizungumza katika kongamano hilo, alisema hivi sasa vyama vya upinzani vimekuwa mbele katika kutumia mitandao hiyo.

Alisema hilo linajionesha pale wabunge wa CCM wanapochangia na kutafuta kipande tu cha mchango na kisha kukirusha katika mitandao hiyo.

Mbunge huyo kijana alisema ni vyema pia vijana wa vyuo vikuu, ambao wapo katika mitandao, nao wakajibu kwa kusema ukweli ulivyo kuliko kuacha uongo ukiendelea kusemwa na watu wakaamini kuwa ni ukweli.

No comments:

Post a Comment