Tuesday, 24 May 2016

MAJANGILI WANANE WA KIMATAIFA WATIWA MBARONI


WIZARA ya Maliasili na Utalii, imetangaza kukamatwa kwa majangili wanane wanaoendesha mitandao wa kimataifa, maarufu duniani, wanaotambulika kwa majina ya OG, Devil na Malikia wa Pembe za Ndovu.

Kukamatwa kwa vinara hao wa ujangili ni matokeo ya doria zilizofanywa ndani na nje ya mapori ya akiba na mapori tengefu, ambako doria 109,474, zilifanyika na watuhumiwa 1,176, walikamatwa huku kesi 654, zikifunguliwa.

Katika kesi hizo, kesi 161 zimemalizika kwa wahalifu 53, kati yao wanane wakiwa majangili maarufu wenye mitandao ya kimataifa.

Hayo yalielezwa jana, bungeni mjini Dodoma na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake.

Alisema nyara zilizokamatwa kwenye doria hizo ni vipande 253, vya meno ghafi ya tembo yenye uzito wa kilo 634, vipande 34 vya meno ya tembo yaliyochakatwa, vyenye uzito wa kilo mbili, wanyamapori hai wakimemo mijusi 315, kobe 202, tumbili 81 na nyani mmoja.

Aidha, alisema kilo 10,096, za wanyamapori aina mbalimbali na ngozi 39, za wanyama hao na bunduki 85, risasi 1,235 za aina tofauti, zilikamatwa katika kipindi cha mwaka 2015 hadi sasa.

Alisema wizara kwa kushirikiana na wadau wa uhifadhi, ilibaini ujangili unafanyika katika ngazi tano, zikihusisha wananchi wanaoishi kwenye maeneo yanayopakana na hifadhi na watumishi wa maliasili wasio waaminifu.

Profesa Maghembe alisema wengine wanaohusika na vitendo hivyo ni wawindaji haramu, wasafirishaji, madalali, wawezeshaji kwenye nchi zinazonunua nyara na kusambaza vitendea kazi, zikiwemo silaha na mtandao wa kimataifa wa ujangili.

Alisema wizara itaendelea kutekeleza mkakati wa kukabiliana na ujangili kwa mwaka 2014 hadi 2019, kwa kuimarisha doria, intelejensia na upatikanaji wa vifaa vya kisasa vya kudhibiti ujangili.

SEKTA YA UTALII

Akizungumzia sekta hiyo, Profesa Maghembe alisema imeshika nafasi ya kwanza kwa mwaka jana, kwa kuliingizia taifa fedha za kigeni katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo.

Fedha hizo ni sawa na wastani wa dola milioni 2,002, kwa mwaka, ambayo ni asilimia 25 ya fedha zote za kigeni nchini.

Alisema sekta hiyo bado inakabiliwa na changamoto ya kutokuwa na miundombinu bora katika maeneo ya vivutio, ikiwemo huduma za maji, umeme na barabara.

Pia, alibainisha kuwa hakuna shirika la ndege lenye uwezo wa kuleta watalii moja kwa moja kutoka kwenye nchi zenye masoko makuu ya utalii.

“Wizara inaishukuru serikali kwa mpango wake wa kununua ndege tatu katika mwaka ujao wa fedha ili kukidhi haja hii katika kipindi cha mpito, wakati serikali ikiendelea na juhudi za kuliimarisha shirika la ndege la taifa,"alisema.

USIMAMIZI WANYAMAPORI

Kwa upande wa Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori (TAWA), Waziri Maghembe alisema kuanzia Julai, mwaka huu, mamlaka hiyo itaanza kutekeleza majukumu yake rasmi.

Utekelezaji huo ni pamoja na usimamizi wa rasilimali wanyamapori katika mapori ya akiba, tengefu na maeneo ya wazi yenye wanyamapori nje ya hifadhi.

Alisema pamoja na kuanzishwa kwa TAWA, Idara ya Wanyamapori itaendelea kuratibu na kurekebisha sera, sheria na kanuni zinazosimamia sekta ndogo ya wanyamapori.

Pia, alisema idara hiyo itaendeleza juhudi za kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika uhifadhi wanyamapori, kuanzisha, kusimamia jeshi usu na kuunganisha juhudi za utafiti na mafunzo.

MIGOGORO YA MIPAKA

Katika kukabiliana na migogoro ya mara kwa mara baina ya wananchi na maeneo ya hifadhi, Maghembe alisema wizara imefanikiwa kuainisha na kuhakiki mipaka ya maeneo yaliyohifadhiwa yenye migogoro kwa mujibu wa matangazo ya serikali.

Maeneo yaliyohusika ni Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, Serengeti, Tarangire na Pori la Akiba la Mkungunero.

Profesa Maghembe aliongeza kuwa, wizara kwa kushirikiana na Halmashauri za Longido, Sikonge, Kilosa, Manyoni, Kiteto na Monduli, imehakiki mipaka ya vitalu 14 vya uwindaji vyenye migogoro.

Alisema pamoja na tatizo la mipaka, upo mgogoro mkubwa wa mifugo kuingizwa ndani ya hifadhi, unaotokea kwenye mapori ya akiba, tengefu na hifadhi za taifa.

Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Bunge kuhusu makadirio ya wizara hiyo, yaliyosomwa na Sebastiani Kapufi (Mpanda Mjini -CCM), alisema ujangili bado ni tatizo linaloikabili sekta ya wanyamapori kutokana na kupungua kwa wanyama na kusababisha baadhi ya vitalu vya uwindaji kupoteza sifa, hivyo wawekezaji kuvirejesha serikalini.

Kapufi aliitaka wizara kuimarisha kitengo cha Intelejensia cha kupambana na ujangili kwa kukipatia vifaa vya kisasa, ikiwa ni pamoja na kutumia ndege zisizoendeshwa na rubani.

Alisema serikali inapaswa kuhakikisha kesi za ujangili zinasikilizwa haraka na adhabu kali kwa wahusika zitolewe kwa wataokutwa na hatia.

“Tunaipongeza serikali kwa kuwatia mbaroni watuhumiwa wa ujangili waliotungua helikopta katika Pori la Akiba la Maswa, matarajio ya kamati ni kuwa kesi hiyo itasikilizwa kwa haraka na kutolewa maamuzi,” alisema.

Aidha, aliitaka wizara kuweka wazi takwimu za idadi ya tembo nchini ili Watanzania waamue ni jinsi gani wataokoa na kulinda rasilimali hiyo ambayo iko hatarini kutoweka.

Katika kipindi cha mwaka 2016/17, wizara hiyo ililiomba bunge kukubali kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya sh. bilioni 135.7.

Wakichangia makadirio hayo, Catherine Magige (Viti Maalumu – CCM), amevitaka vyombo vya dola kufanya uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazowakabili baadhi ya wabunge, wakihusishwa na mtandao wa ujangili.

Alisema hakuna mtu yeyote aliye juu ya sheria, hivyo ni kazi ya vyombo hivyo vya usalama kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua za kisheria bila kujali nyadhifa walizokuwa nazo.

Alisema bunge limekuwa likiwanyooshea vidole watu walio nje ya chombo hicho kuwa ni majangili, lakini baadhi ya majangili hao wanadaiwa kushirikiana na wabunge.

“Vyombo vya dola lazima vifanye kazi yake, tunataka kuwajua ndani ya bunge hili hao ni kina nani? Kwani hakuna mtu aliye juu ya sheria,” alisisitiza mbunge huyo.

Awali, Catherine alishangazwa kukosekana kwa bodi ya wakurugenzi kwenye Mamlaka ya Taifa ya Hifadhi za Wanyamapori (TANAPA).

Alisema kukosekana kwa bodi hiyo kumeifanya serikali kutoa maamuzi kupitia waziri na katibu mkuu, kitendo kinachorudisha nyuma ufanisi wa mamlaka hiyo.

Dotto Biteko (Bukombe –CCM), aliijia juu wizara hiyo huku akitishia kuondoa shilingi kwenye mshahara wa waziri, kama hatopatiwa majibu ya kutosha kuhusu vitendo vya unyanyasaji vinavyofanywa na askari wa wanyamapori.

Alisema kwenye Kijiji cha Kidosere, kinachopakana na Hifadhi ya Kigosi-Muyowosi, nyumba zaidi ya 40, zilichomwa moto na mazao ya wakulima kufyekwa na askari hao.

“Katika kijiji hicho, wananchi wameshi kwa miaka mingi, wamelima, wamepiga kura, lakini leo iweje waonekane wavamizi?” Alihoji.

Aliongeza kuwa ng’ombe 215 waliuawa kwa kupigwa risasi huku wengine 603 wakitaifishwa.

Alisema licha ya wamiliki wa mifugo hiyo kujitokeza, askari wanyamapori walitoa taarifa kuwa baadhi ya ng’ombe walikamtwa kwa kutokuwa na wamiliki.

“Haiwezekani nikae humu bungeni kwenye kiti cha kuzunguka, halafu wananchi wa Bukombe waendelee kunyanyaswa. Sitaunga mkono mpaka nipate majibu ya kina, vinginevyo nitakufa na wewe,”alisema Biteko.

Kwa upande wake, Magdalena Sakaya (Kaliua – CUF), alihoji kuweko kwa tetesi za serikali kutaka kuiendesha TANAPA na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Alisema kama kuna wazo hilo, ni vyema serikali ikaachana nalo kwani kufanya hivyo ni kuyaua mashirika hayo, ambayo yana mchango mkubwa kwenye uhifadhi.

Alisema mashirika mengi yalikufa baada ya kurejeshwa serikalini kutokana na kukosa usimamizi wa kina.

No comments:

Post a Comment