Tuesday, 24 May 2016

SAMIA: HAKUNA UTANI VITA DHIDI YA RUSHWA


MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amesema serikali haitanii kwenye mapambano dhidi ya rushwa na kwamba, kasi itaendelea kuwa hiyo hiyo kwa ajili ya kukabiliana na ufisadi.

Amewaonya wafanyabiashara wakubwa wanaotumia rushwa kukwepa kodi stahiki na kwamba, hivi sasa serikali inafuatilia nyendo za kila mmoja ili kuhakikisha kila senti inayostahili kuingia serikalini inapatikana.

"Tumedhamiria kupambana na rushwa hatutanii, kila mmoja ajitambue na ahakikishe anashirikiana na serikali kuipinga. Tunatekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), hatutarudi nyuma,"alisema.

Aliitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupamabana na Rushwa (TAKUKURU), kushughulikia taarifa za rushwa mara zinapowafikia na kwamba, wakati huu si wa kuzikalia, bali kuzifanyia kazi.

Samia alisema hayo jana, mjini Dar es Salaam, wakati akizundua kampeni ya TAKUKURU ya 'Longa Nasi', inayolenga kuvunja ukimya kuhusu rushwa nchini.

Alisema bila jitihada za pamoja za kuzuia na kupambana na rushwa na ufisadi, serikali ya awamu ya tano haitawaletea mabadiliko yaliyokuwa na kiu ya muda mrefu ya Watanzania, ikiwemo sekta ya elimu, afya na mishahara mizuri ya watumishi.

"Katika jambo hili la mapambano dhidi ya rushwa, yameanza kuonekana baadhi ya mafanikio, ambapo ongezeko la ukusanyaji wa kodi, ufuatiliaji na udhibiti wa watumishi hewa, uwajibishwaji wa watumshi wazembe na uwajibishwaji wa watumishi wabadhirifu,mafisadi na ufuatiliaji na usimamizi makini wa fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo," alisema.

Alisema wakati umebadilika na kwamba kwa sasa kila Mtanzania anapaswa kuwa na tabia ya kuhoji pale ambapo mazingira yanaonekana kutia wasiwasi au kuashiria kuwepo kwa vitendo vya rushwa.

Alisema ipo haja kwa viongozi, watumishi, wafanyabiashara, wanasiasa na wananchi, kutumia fursa ya kampeni hiyo ya mapambano dhidi ya rushwa, kuibua na kufichua vitendo hivyo na hatimaye wahusika wafikishwe mahakamani. 

"Ni dhahiri mapambano haya ya rushwa yanakwenda sambamba na llani ya CCM ya uchaguzi ya mwaka 2015 hadi 202 ya kudhibiti rushwa nchini ili Watanzania wafaidi rasilimali za taifa na serikali inamaanisha inachokisema,” alisema.

No comments:

Post a Comment