Tuesday, 24 May 2016
KASHFA ZAENDELEA KUMUANDAMA LOWASSA
WAZIRI Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa, ameendelea kutuhumiwa kujimilikisha rasilimali, ambapo juzi, alilipuliwa bungeni kwa kujimilikisha na kutengeneza hati miliki kupitia shamba la wananchi lililoo Makuyuni mkoani Arusha.
Serikali imesema itamnyang’anya shamba hilo na kuwarudishia wananchi ili kuondoa mgogoro uliopo hivi sasa.
Lowassa, ambaye pia aligombea urais kwenye uchaguzi mkuu uliopita kupitia UKAWA, katika Bunge hili la 11, ameibuka katika kashfa mbili, ikiwemo ya kuwa miongoni mwa viongozi waliouziwa nyumba za serikali.
Hoja hiyo ya Lowassa kuuziwa nyumba ya serikali katika serikali ya awamu iliyopita, ilitolewa bungeni mjini hapa jana na Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Rita Kabati, wakati wa majadala wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, iliyopitishwa wiki iliyopita.
Juzi, wakati Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, akihitimisha hoja ya wizara hiyo na kujibu hoja zilizotolewa na wabunge wakati wakichangia, alisema Lowassa amejimilikisha shamba la wananchi la Makuyuni lililoko jijini Arusha.
Lukuvi alisema Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, aliagiza wananchi kukabidhiwa shamba hilo, lakini Lowassa aliwageuka na kutengeneza hati, ambayo inaonyesha kuwa yeye ndiye mmiliki wa shamba hilo.
“Mgogoro wa shamba la Makuyuni nitaumaliza, hapa ninayo hati ambayo Lowassa alisaini kuwa yeye ndiye mmiliki,”alisema huku akiionyesha hati hiyo.
Lukuvi alisema yeye ndiye waziri na kwa kuwa Lowassa, alimdanganya rais na mbunge huyo anamlalamikia bosi wake, hivyo atahakikisha hati hiyo inafutwa na shamba hilo linarudishwa kwa wananchi.
Alisema wakati Mbunge wa Monduli, Julias Laizer (CHADEMA), akichangia, alifoka sana kuhusu kurejeshwa kwa wananchi shamba hilo la Makuyuni.
Lukuvi alisisitiza kuwa anachokisema mbunge huyo anakubaliana nacho: “Lakini ujue kuwa itakula kwako kutokana na kuwa aliyejimilikisha hilo shamba kutoka kwa mwekezaji ni Lowassa.”
“Hilo shamba liliishatolewa kwa wananchi na lilipangwa litolewe kwa wananchi na lazima litarudi kwao kutoka kwa aliyejimilikisha kinyemela,”alisema.
Lukuvi alisema alichokuwa anakitaka ni kumpa hiyo taarifa mbunge huyo kwa kuwa ameingia pagumu kutokana na kuwa shamba hilo lilidhaminiwa na Rais Benjamini Mkapa, wapewe wananchi.
Alisema shamba hilo lilikuwa la mwekezaji wa shamba la Stein, aliyefukuzwa nchini na ndege zake na kila kitu na Lowassa, akiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, ambapo Rais Benjamin Mkapa alisisitiza shamba hilo wapewe wananchi, lakini bahati mbaya hati aliyonayo imesainiwa na Lowassa.
"Nakusaidia wewe kuwa hati hii tutairekebisha, yeyote aliyesaini hapa tutarekebisha na ardhi itarudi kwa wananchi. Nashukuru sana hili tutalimaliza kwa kushirikiana na Halmashauri ya Monduli,"alisema.
Awali, akichangia mjadala wa makadirio ya wizara hiyo, Jumamosi iliyopita, Mbunge wa Monduli, Lazier (CHADEMA) alisema sehemu kubwa ya ardhi ni hifadhi na iliyosalia imehodhiwa na vigogo, hivyo wananchi wameapa kutoruhusu tena ardhi yao kutwaliwa.
Laizer alisema ardhi hiyo ilipangwa kugawiwa kwa wananchi waliokuwa wameondolewa katika maeneo ya jeshi, lakini wamekuwa wakipokea taarifa mbalimbali kutoka wizarani wakitaka eneo hilo.
Katika hatua nyingine, Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Shaaban Mdoe, amemuonya Lowassa na wafuasi wake kuacha tabia ya kuwatisha watendaji wa serikali waliokataa kumuunga mkono alipoihama CCM na kujiunga na upinzani.
Mdoe, alitoa onyo hilo jana, alipokuwa akizungumza katika mkutano wa viongozi wa CCM wa ngazi mbalimbali wilayani Monduli, katika kata ya Engaruka, kufuatia malalamiko yaliyotolewa na Katibu Tarafa ya Kisongo, Paulo Kiteleki, kuwa amekuwa akitishwa kutokana na misimamo yake katika kazi.
Kiteleki katika maelezo yake alidai kuwa, katika mikutano ya hivi karibuni ya Lowassa na viongozi wa wilaya hiyo, akiwemo mbunge Julius Kalanga na Mwenyekiti wa Halmashauri, Isack Joseph, walikuwa wakitoa kauli za udhalilishaji na vitisho kutokana na misimamo yake ya kuiunga mkono serikali ya Rais Dk. John Magufuli.
“Hivi kiongozi kama anashuhudia uongo na vitisho vinavyotolewa na viongozi wenzako kwangu kuwa ameninunulia suti, gari na kunijengea nyumba, hayo yana mahusiano gani na maendeleo ya wananchi na alikuwa akininunulia mimi kama nani wake,”alihoji Kiteleki.
Alisema katika mikutano hiyo, kumekuwa na vitisho dhidi ya maisha yake kutokana na misimamo yake dhidi ya kuunga mkono juhudi za serikali ya sasa na kwamba, bado ataendelea kushikilia msimamo wake huo kutokana na kuridhishwa na utendaji kazi wa serikali.
Akijibu malalamiko hayo, Mdoe alisema viongozi wa CCM hawako tayari kuona kiongozi au mtu yeyote akikwamisha juhudi za viongozi waadilifu katika kuwatumikia wananchi, kwa kuwa uchaguzi ulishakwisha na sasa ni kuchapa kazi tu.
Aliwataka viongozi hao kutokatishwa tamaa wala kuogopeshwa na vitendo wala kauli za viongozi waliofilisika kimawazo, ambao wameshindwa kutekeleza ahadi walizozitoa kwa wananchi na kuanza kutafuta sababu au mchawi kwa kushindwa kwao.
Alisema wataendelea kushikilia na kutekeleza agizo la Rais Dk. Magufuli wakati alipokutana na wenyeviti na makatibu wa mikoa na wilaya wa CCM la kuwasimamia viongozi wa serikali katika kufanya kazi za utekelezaji wa Ilani, kwa kuwa usimamizi huo si tu katika kuwaadhibu wanaokosea, bali hata kuwahakikishia mazingira mazuri ya utendaji wao wa kazi.
Aidha, alimtaka katibu tarafa huyo pamoja na viongozi wengine wa serikali na CCM, ambao wamekutana na vitisho na kauli mbalimbali, kutokaa kimya, badalaa yake waende kutoa taarifa hizo katika vyombo vya usalama kwa ajili ya kumbukumbu na hata hatua zaidi kuchukuliwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment