Saturday, 10 October 2015
URAIS KWA MAGUFULI NI DHAHIRI
NA KHADIJA MUSSA, ILEMELA
MJUMBE wa Kamati ya Ushindi ya CCM, Christopher ole Sendeka, amesema urais kwa mgombea urais kupitia CCM, Dk. John Magufuli, hauepukiki kutokana na wananchi wengi kumkubali.
Amesema hatua hiyo inatokana na idadi kubwa ya wananchi kumkubali katika maeneo mbalimbali ya nchi, yakiwemo ambayo wapinzani wanaona ni ngome yao kama mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Mwanza.
Sendeka aliyasema hayo jana katika mkutano wa kampeni wa Mgombea Mwenza wa Urais kupitia CCM, Samia Suluhu Hassan, uliofanyika kwenye jimbo la Ilemela na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa wananchi.
"Dk Magufuli haepukiki kuwa rais kwani hadi sasa wananchi wamesema wanataka kazi tu na kinachoshindanishwa kwa sasa ni mkoa gani utakaoongoza kwa kumpigia kura nyingi,” alisema.
Alisema kazi ya kiongozi ni kuonyesha njia na watu wanafuata na imani ya kweli ni kuonyesha kwa vitendo na Dk. Magufuli ameonyesha hilo katika nafasi mbalimbali alizopewa kuongoza tofauti na wagombea wengine.
Ole Sendeka alisema Dk. Magufuli na Samia ni kielelezo cha uchapakazi, uaminifu, uadilifu na kujenga mshikamano wa taifa, hivyo aliwaomba wananchi kuhakikisha wanamchagua ili aweze kuwaletea maendeleo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Afrika Mashariki, Angela Kizigha, aliwataka wananchi kutochagua chadema kwa kuwa kiliwaahidi ahadi za uongo ikiwemo ya mikopo isiyokuwa na riba kwa wanawake na bodaboda kwa vijana ahadi ambazo hakuna iliyotekelezwa.
Mgombea Mwenza, Samia amesema suala la migogoro kati ya wananchi na kiwanda cha nondo cha Nyakato ambacho kinatoa moshi mchafu wenye sumu ambao unawaathiri wananchi hivyo aliahidi kuhakikisha tatizo hilo analisimamia na kulimaliza.
Samia alisema kwa kuwa yeye anafanyakazi Ofisi ya Makamu wa Rais ambayo ndiyo inalishughulikia masuala la mazingira hivyo atazungumza na wamiliki wa kiwanda hicho ili wadhibiti hiyo hali na wasiporekebisha hali hiyo hatua zaidi zitachukuliwa.
Pia kuhusu tatizo la wananchi wa mkoa huo kupewa viwanja karibu viwanda litafanyiwa kazi ili kuepusha migogoro kama hiyo kupitia ilani ambayo imeelekeza kupima upya ardhi yote na kutenga maeneo kwa ajili ya matumizi mbalimbali kama ya viwanda, makazi, ufugaji na kilimo.
KIBOKO YA MAFISADI
Awali akizungumza katika mkutano uliofanyika Magu, Samia alisema Chama kiliamua kumkabidhi Dk. John Magufuli dhamana ya kugombea urais kwa kuwa ataondoa wabadhirifu wa mali za umma ambao wanataka kuhalalisha uovu.
Kutokana na hali hiyo, aliwaomba wananchi kumchagua Dk. Magufuli kwa sababu akiingia madarakani atalinda mali za umma hivyo kuwanufaisha wananchi wote.
“Tumchague Dk. Magufuli awe rais kwa sababu ana uwezo mkubwa wa kufanya kazi pia ataondoa wala rushwa na wabadhirifu wa mali za umma kwani suala hili limekithiri na linaonekana kama jambo la kawaida," alisema Samia.
Pia alisema serikali ijayo imepanga kufanya sensa ya wazee ili kujua idadi yao na sehemu waliko kwa sababu inataka kuwalipa mafao kama namna ya kuthamini mchango walioutoa katika taifa.
Samia pia aliwaomba wananchi wachague CCM kwa kuwa itaendelea kuuenzi na kuutunza Muungano wa Tanzania ambao ni tunu ya taifa.
Kuhusu vijana, aliwataka kutokubali kudanganyika na kutumika katika kufanya mambo yasiyo na tija kwao na kuwataka wajithamini na kujitambua kuwa ni rasilimali inayopaswa kutumika kwa ajili ya maendeleo yao na si bomu linalosubiri kulipuka kama wanavyodhani wapinzani.
Alisema serikali ijayo utajikita katika kuwawezesha vijana kupata ajira kupitia sekta ya viwanda na kutoa elimu ya ujasiriamali, hivyo kujikwamua kiuchumi na kuondokana na utegemezi na umasikini wa kipato.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment