Friday, 11 September 2015

MEMBE: CCM ITAPATA USHINDI WA KISHINDO

NA MUSSA YUSUPH
WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitaibuka na ushindi wa kishindo kwa kuwa kina mgombea urais bora kushinda vyama vya upinzani.
Pia, aliwataka waangalizi wa uchaguzi wa ndani na nje ya nchi kutojihusisha kisiasa na kutoingia nchini na kiasi kikubwa cha fedha pasipo matumizi yake kutolewa ufafanuzi.
Amewahakikishia wananchi na mabalozi kutoka nchi za kigeni kuwa, vyombo vya ulinzi na usalama havitajihusisha na masuala ya kisiasa bali jukumu lake litakuwa kulinda usalama wa raia na mali zao.
Membe aliyasema hayo jana, Dar es Salaam wakati alipokuwa akizungumza na mabalozi na wawakilishi wa mataifa mbalimbali kuzungumzia mchakato wa uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Alisema CCM ina misingi mikuu mitatu inayokiongoza ambayo haipatikani kwenye vyama vingine siasa.
Waziri huyo wa Mambo ya Nje, alisema misingi hiyo ni kumbukumbu ya kuwajenga viongozi bora wenye kuliletea taifa maendeleo, mipango ya utekelezaji na utendaji kazi kwa serikali zake inazoziongoza.
Msingi mwingine alisema, mgombea urais wa CCM, Dk.  John Magufuli, ana historia nzuri ya utendaji kazi ambayo haiwezi kulinganishwa na wagombea wanane wa nafasi hiyo kutoka vyama vya upinzani.
Hivyo, alisema CCM itaibuka na ushindi wa kishindo kwa sababu ya kusimamia misingi yake ipasavyo.
ATOA MASHARTI KWA WAANGALIZI
Waziri Membe alisema waangalizi hawapaswi kujihusisha na masuala ya kisiasa kwa mujibu wa sheria na kanuni za uchaguzi.
Alisema wapo baadhi ya waangalizi wenye malengo ya kuegemea upande fulani wa kisiasa, lakini serikali itahakikisha wanafanya kazi zao kwa mujibu wa sheria.
Aliongeza kuwa waangalizi hao hawapaswi kuingia nchini na kiasi kikubwa cha fedha pasipo kuzitolea ufafanuzi wa matumizi yake.
“Kwenye viwanja vya ndege au mipakani waangalizi watahojiwa kama wakikutwa na kiasi kikubwa cha fedha, matumizi ya fedha hizo yanapaswa kuthibitishwa kinyume na hapo watarudishwa,” alisema.
"Fedha za uchaguzi kuna njia maalum ambayo inatumika katika kuzipokea ambapo wahisani na serikali wanachangia fedha hizo kupitia Shirika la Maendeleo ya Umoja wa Mataifa (UNDP) na kisha fedha hizo zinasambazwa kwenye tume za uchaguzi” alisisitiza.
Aliongeza kuwa Marekani, Uingereza, Norway, Jumuia ya Ulaya, Jumuia ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) zimethibitisha kutuma waangalizi wao.
Alisema waangalizi hao  watatakiwa kujaza fomu maalum za utambuzi zinazotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ili kuwawezesha kufanya kazi hiyo.
Membe aliendelea kusema kuwa Watanzania milioni 23.7 wanatarajiwa kushiriki kwenye mchakato huo wa kuwachagua madiwani, wabunge na rais.
Alisema zaidi ya sh. bilioni 265 zimetumika katika kufanikisha uchaguzi huo huku waangalizi kutoka nchi za kigeni na mashirika ya kimataifa zaidi ya 400 wanatarajiwa kushiriki.
Membe alisema waangalizi wa uchaguzi hawatoruhusiwa kutoa tamko lolote kuhusiana na mwenendo wa uchaguzi hadi uchaguzi mkuu utakapomalizika.
Baada ya kumalizika kwa uchaguzi, Membe alisema kutatangazwa matokeo na waangalizi hao wataruhusiwa kuzungumzia mwenendo mzima wa uchaguzi pamoja na kupewa siku 30 hadi 60 kuandika ripoti husika.
“Endapo wakibaini mambo yanayokwenda kinyume na taratibu za uchaguzi wanahaki ya kuandika na kuwasilisha taarifa hizo kwenye mamlaka husika,” alifafanua.
Alibainisha kuwa wapo watu wenye kutofautiana na vyama vya ukombozi ambavyo vimekaa madarakani kwa kipindi kirefu, lakini hawawezi kubadili maamuzi ya wananchi.
VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA
Akizungumzia majukumu ya vyombo vya ulinzi na usalama, Waziri Membe alisema havitajihusisha na masuala ya kisiasa.
Alisema majukumu yake yatakuwa kuhakikisha ulinzi na usalama wa wananchi na mali zao unakuwepo katika kipindi chote cha uchaguzi.
Membe aliongeza kuwa kuna baadhi ya watu wenye kuhusisha suala la mabadiliko na vurugu, hivyo nchini ipo imara kukabiliana nao.
Alisisitiza kuwa serikali itaimarisha amani na utulivu ikiwemo ulinzi wa wananchi.
“Vyombo vya ulinzi na usalama vipo imara kuhakikisha usalama unakuwepo hivyo mabalozi na wananchi wanapaswa kuvisaidia ili azma hiyo ifanikiwe,” alisema.
Waziri Membe alisisitiza kuwa uchaguzi mkuu utafanyika kwenye mazingira huru na haki kwa kuheshimu maamuzi ya wananchi.

No comments:

Post a Comment