Friday, 11 September 2015

LOWASSA, SUMAYE WAMECHANGANYIKIWA- WARIOBA

Mgombea wa Urais kupitia CCM Dk. John Pombe Magufuli akiweka saini kwenye kitabu cha wageni nyumbani kwa Baba wa Taifa Julius Kambarage Nyerere,kulia ni Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Sinde Warioba na kushoto ni Chief wa Wazanaki Japhet Wanzagi
DK. Magufuli akijiandaa kuweka shada la maua kwenye kaburi na hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, nyumbani kwake, Butiama mkoani Mara.
 Mgombea wa Urais kupitia CCM Dk.John Pombe Magufuli akisalimiana na Mtoto wa Baba wa taifa ambaye pia ni Mbunge wa Afrika Mashariki Makongoro Nyerere mara baada ya kuwasili mkoani Mara
DK. Magufuli akisalimiana na Steven Wassira, ambaye ni miongoni mwa makada waliojitokeza kuomba kuteuliwa kuwania urais kwa tiketi ya CCM.
Add caption
DK. Magufuli akiteta jambo na mgombea ubunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono
DK. Magufuli akihutubia wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye kijiji cha Butiama mkoani Mara.
 Mgombea wa Urais kupitia CCM Dk. John Pombe Magufuli akitoa wasifu wa mgombea ubunge jimbo la Bunda mjini Stephen Wasira (kushoto) na mgombea ubunge wa jimbo la Mwibala, Kange Lugola (kulia) kwenye mkutano wa kampeni za CCM uliofanyika Bunda mjini
KADA maarufu wa CCM, Gachuma akihutubia wananchi kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Butiama

NA SELINA WILSON,BUNDA

WAZIRI Mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba, amewaponda  mawaziri wakuu wenzake kwa kuhama CCM wakidai hakuna kilichofanyika katika miaka 54 ya Uhuru, wakati wenyewe ndio walikuwa watendaji wakuu wa serikali.

Amesema wanapaswa kujitafakari na anajua wazi huenda hata wanachokifanya hawajui wajibu wao walipokuwa katika madaraka hayo kama washauri wakuu wa Rais.

Warioba ambaye aliibukia katika mkutano wa hadhara wa mgombea Urais wa CCM, Dk. John Magufuli  wilayani Butiama mkoani Mara ambapo alisema  umefika wakati wa watu wanaomtumia kama dira Baba wa Taifa katika kampeni zao wajitafakari zaidi.

Akizungumza bila kutaja jina la mtu, Jaji Warioba, alisema wakati wa mchakato wa urais ndani ya CCM kila mgombea alikwenda katika kaburi la Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliyezikwa katika Kijiji cha Mwitongo kuomba dua kabla ya kuanza mikakati yao.

Jaji Warioba alisema  licha ya kufanya hivyo lakini bado walipotoka hapo na kuhama  CCM wamejikuta wakishindwa kujua wajibu wao walipokuwa kwenye uwaziri mkuu na sasa wanasema hakuna kilichofanyika.

"Wagombea wengi walipita Mwitongo kuomba dua, lakini baada ya kumalizika baadhi yao kwa kushindwa kutambua mchango wa Mwalimu Nyerere wanasema miaka 54 ya Uhuru hakuna kilichofanywa,”alisema.

Alisema wengine katika kampeni zao wanatumia maneno ya Mwalimu kama wamechanganyikiwa. ”Huwezi kumtumia Mwalimu kama dira, halafu unasema hakuna kilichofanyika. Wakati aliijenga Tanzania kwenye misingi na wote walimfuata wanapita kwenye misingi yake," alisema Jaji Warioba

Jaji Warioba alilazimika kutoa somo la uwajibikaji katika nafasi ya waziri mkuu ni ya juu ambayo hupewa mtu anayeaminiwa na mara zote huwa mshauri wa karibu wa rais.

Alisema alikuwa Waziri Mkuu alifanyakazi kwa karibu chini ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi ambaye alimshauri vizuri wakati wote katika utawala wake.

"Nashangaa ninaposikia kuna wenzangu wanasema hakuna kitu kilichofanyika. Waziri Mkuu ni mshauri mkuu wa rais hakuna kitu kinachoweza kufanyika bila kushiriki.

"Nasema hili hata Mwinyi(Rais Mstaafu), alikuwa hafanyi jambo bila kushauriana nami kwa ajili ya kusimamia, sasa leo hawa wenzangu wanasema hakuna mafanikio kwenye miaka 54 ya uhuru basi na wao hakuna walichofanya walipokuwa katika uwaziri mkuu," alisema

Alisema Tanzania inahitaji kiongozi mzalendo mwenye kujali watu na kuwaunganisha kama anavyofanya Dk. Magufuli.

Akizungumzia maadili, Jaji Warioba alisema hatua ya nchi kupoteza maadili ilitokana na  uamuzi wa baadhi ya viongozi kuwa na uhusiano na matajiri.

"Niliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Rushwa na taarifa tuliandika katika ripoti ile, chanzo ni uhusiano wa viongozi na matajiri na ukishakuwa hivyo mawazo yako yatakuwa ni utajiri badala ya kuwatumikia watu," alisema.

Alisema pamoja na kuwa msaidizi wa Mwalimu kwa kipindi kirefu, lakini katika utawala wake hakuwahi kuchukua fedha za Watanzania na kujilimbikizia mali.

Dk.Magufuli asema hataacha
kuzungumzia amani, utulivu


Akizungumza katika mikutano ya kampeni iliyofanyika katika Wilaya za Butiama, Bunda na Serengeti, Dk. Magufuli, alisema katu hatoacha kuzungumzia amani japo kuna watu wanachukizwa na hilo.

Alisema hatoweza kuacha kuhubiri amani ya nchi na kama ni hivyo, ni bora asichaguliwe kuwa rais wa awamu ya tano.

"Nimeanzia Butiama kutokana na historia yake ya amani ya nchi hii. Ninajua wapo watu eti wanasema nisihubiri amani ya nchi nitaendelea kuisemea amani wakati wote. Iwe usiku ama mchana na hata wakati wote nitazungumzia amani ya nchi yetu na Watanzania  kwa ujumla. Nisipohubiri amani basi sistahili kuwa rais."

"Mama Maria Nyerere yupo Namibia anapokea tuzo ya amani  kwa sababu ya amani ya nchi yetu ambayo misingi imara iliyowekwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere," alisema.

Kauli hiyo ya Dk.Magufuli imekuja siku moja baada ya Kituo cha Haki za Binadamu na Msaada wa Kisheria (LHRC), kumtaka mgombea huyo kuacha kutumia mifano ya nchi za Libya na Misri katika kampeni zake.

Dk. Magufuli alisema amedhamiria kuwatumikia Watanzania kwa vitendo huku akisisitiza haja yake ya kuwa na mawaziri wachache wenye uadilifu kabla na baada ya kuapishwa.

Alisema anatambua suala la kero ya maji na huduma za afya ambayo  amejipanga kuiondoa baada ya kuingia madarakani.

Akizungumza na wananchi wa Kata ya Nyamuswa, Dk Magufuli aliahidi ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami Nyamuswa/Ikoma /Ngorongoro mapaka Arusha kilometa 100.

Dk. Magufuli alisema ujenzi wa barabara hiyo ulichelewa kutokana na serikali kuchelewesha fedha za malipo ya awali ya mkandarasi, lakini sasa kwa kuwa atakuwa Rais atakuwa anaagiza.

Alisema waziri wa ujenzi atakayemteua atamuagiza kazi ya barabara hiyo iwe ya kwanza na aliwahakikishia wananchi kwamba itajengwa na serikali ya Magufuli.

No comments:

Post a Comment