Friday, 11 September 2015

MIGOGORO YA ARDHI KUMALIZWA NA SERIKALI YA AWAMU YA TAN0

 Mgombea Mwenza wa Urais kwa tiketi ya CCM, Mama Samia Sukuhu Hassan, akihutubia umati wa wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika leo kwenye Viwanja vya Ikulu, Bagamoyo mkoa wa Pwani
 Mgombea Ubunge jimbo la Bagamoyo, Dk. Shukuru Kawambwa akiomba kura baada ya kutambulishwa na mgombea Mwenza wa Urais kwa tiketi ya CCM, Mama Samia Suluhu Hassan Katika mkutano wa kampeni uliofanyika leo katika Uwanja wa Ikulu mjini Bagamoyo
Mjumbe wa NEC, Livingstone Lusinde akihutubia umati wa wananchi katika mkutano wa kampeni uliofayika leo katika jimbo a Bagamoyo mkoa wa Pwani
 Mjumbe wa NEC, Livingstone Lusinde akipongezwa na Mgombea Ubunge jimbo la Chalinze, Riziwani Kikwete baada ya kuhutubia mkutano wa kampeni uliofanyika leo kwenye viwanja vya Ikulu, Bagamoyo, mkoa wa Pwani.
 Wananchi wakiwa kwenye mkutano wa kampeni wa mgombea mwenza wa Urais kwa tiketi ya CCm Mama Samaia Suluhu Hassan uliofanyika leo kwenye Viwanja vya Ikulu, jimbo la Bagamoyo mkoani Pwani
 Waingizaji wa filamu za Bongo Movie, wakiserebuka uwanjani wakati wa mkutano wa akampeni wa Mama Samia uliofanyika leo kwenye viwanja vya Ikulu mjini Bagamoyomkoa wa Pwani

NA ABDALLAH MWERI, CHALINZE

MGOMBEA Mwenza wa urais wa CCM, Samia Suluhu Hassani amesema dawa ya migogoro ya ardhi nchi mzima itamalizwa na serikali ya awamu ya tano.

Samia alisema serikali ya Dk. John Magufuli, itavalia njuga suala hilo kwa kupima ardhi ya Tanzania ili kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika jana katika Kijiji cha Lugoba, Samia alisema anakerwa na mauaji ya wakulima na wafugaji yanayojitokeza kwenye baadhi ya maeneo nchini.

Samia alisema serikali ya awamu ya tano, imejipanga kupima ardhi katika vijiji vyote na kwamba kila mwananchi atapata haki yake ya kupimiwa eneo lake.

“Natambua migogoro ya ardhi ipo kwenye baadhi ya maeneo, lakini mkitupa ridhaa ya kushika dola tutahakikisha tunaimaliza,” alisema.

Samia alitoa kauli hiyo alipokuwa akijibu ombi la Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete, ambaye alidai wakazi wa Chalinze wanakabiliwa na migogoro mikubwa ya wakulima na wafugaji ambao wamekuwa wakigombea ardhi.

Alisema Watanzania hawana sababu ya kuuana kwa kugombea ardhi kwani kila mmoja ana haki ya kuishi kwa usalama na amani.

Samia alisema serikali ya awamu ya tano imejipanga kuhakikisha kila Mtanzania anapata bima ya afya na kwamba kila mwananchi anajiunga na Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii.

Alisema mpango huo ni mkakati wa CCM katika kuboresha afya za Watanzania ambapo amewataka wakazi wa Chalinze kujiunga na mpango huo.

“Watanzania wote lazima muwe na bima ya afya, serikali ya Dk. Magufuli imejipanga vizuri kuboresha huduma za afya kwa kila mwananchi,” alisema.

Alisema serikali ya awamu ya tano itaongeza nguvu katika ujenzi wa hospitali mpya inayojengwa Chalinze ambayo itaondoa kero inayowakabili wakazi wa Chalinze.

Samia alisema serikali itatoa ajira kwa vijana ambapo asilimia 40 watanufaika ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Alisema katika jimbo la Chalinze kutajengwa viwanda vidogo vidogo vinatavyowanufaisha vijana na wananchi wa eneo hilo.

Mgombea huyo alisema viwanda hivyo vitatokana na mazao ya mihogo, mananasi na ufuta na kwamba serikali itatenga fedha kwa ajili ya kuwakopesha vijana kupitia benki.

Mbunge wa Nkenge anayemaliza muda wake, Asumpta Mshana,  alisema Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe anapaswa kufungwa jela iwapo mgombea urais wa chama hicho, Edward Lowassa, atafariki dunia.

Alisema afya ya Lowassa si mzuri, lakini Mbowe amemuingiza mkenge ili apate fedha, hivyo akifariki baada ya kukosa urais Oktoba 25, mwaka huu, Mbowe atabeba msalaba.Katika hatua nyingine, Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete, amemtaja, Samia kuwa ni mwanamke jasiri na anatosha kuwa mgombea mwenza wa urais katika uchaguzi mkuu ujao.

Salma alisema Samia ni mchapakazi na amewataka wakazi wa Chalinze kumchagua Dk. Magufuli ili afanye naye kazi katika serikali ya awamu ya tano.

Mke wa Rais alitoa kauli hiyo katika mkutano wa kampeni uliofanyika jana katika Kijiji cha Lugoba, Chalinze ambapo mgombea mwenza huyo alizungumza na wakazi wa eneo hilo na vitongoji jirani.

Alisema Samia amekuwa mtendaji hodari katika wizara mbalimbali, hivyo amewataka wakazi wa Chalinze kutofanya kosa katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Salma ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM kupitia Mkoa wa Lindi, alisema Samia ndiye suluhu ya kuwakomboa Watanzania endapo watampigia kura ya ndio Dk. Magufuli.

"Suluhu maana yake ni suluhu anasawazisha kila kitu kwa hiyo naomba Watanzania msifanye makosa kuwachagua watu ambao hawana uchungu na nchi yetu," alisema Salma.

Alisema Samia ana uzoefu wa kutosha katika utendaji wa kazi na amewataka Watanzania kuichagua CCM kwa kuwa ndio chama pekee kinachotekeleza ilani yake.

Pia, aliwataka wakazi wa Chalinze kumchagua Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete kwa kuwa ameleta maendeleo makubwa kwa wakazi wa Chalinze.

"Jamani uchungu wa mwana aujuaye mzazi, Ridhiwani ni mwanangu, nawaomba sana mumpe kura katika uchaguzi mkuu ujao kwa kuwa ni hodari na ameleta maendeleo katika Jimbo la Chalinze," alisema Salma.

Salma aliwataka wakazi wa Chalinze kumchagua Dk. Magufuli kuwa Rais wa Awamu ya Tano, Mbunge Ridhiwani na madiwani wa CCM katika uchaguzi huo.

No comments:

Post a Comment