Na John Kiroboto
KUANZA kwa
kinyang'anyiro cha uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini kote Oktoba 25,
mwaka huu, kumekuja na matukio, hisia na maono mbalimbali miongoni mwa
wananchi.
Wananchi
wanaofuatilia mikutano ya kampeni hususan baada ya vyama kuzindua kampeni hizo
takriban wiki mmoja sasa, wamekuwa wakihoji wakitaka kujua hali ya kiafya ya
mgombea wa Chadema, anayeungwa mkono na kundi la Ukawa, Edward Lowassa.
Lowassa,
ambaye alijiuzulu uwaziri mkuu Februari, 2008, kutokana na kashfa ya mtambo wa
kufua umeme wa Richmond, amekuwa haonyeshi afya njema si tu majukwaani, hata
katika maeneo mengine ambako amekuwa akipita kwa shughuli za kisiasa au
kibinafsi.
Watu
waliopata kumshuhudia wanasema hayuko katika hali yake ya kawaida ya Lowassa
waliyemfahamu, aliyekuwa mchangamfu na jasiri katika kuzungumza na kukemea.
"Lowassa wa sasa ni mnyonge anayeonyesha sura ya kukata tama, lakini
iliyogubikwa na hasira," anasema Mohamed Sufiani mkazi wa Tabata.
Mwonekano wa
Lowassa anapotembea hivi sasa ni kama mtoto anayejifunza kutembea, huku akivuta
miguu, lakini pia hata anapoongea si mtu wa kujitikisa na hasa awapo jukwaani,
ambapo mara nyingi amekuwa akishindwa kunyanyua mikono juu kama wafanyavyo
wanasiasa wengine.
"Amekuwa
ni kama mtu anayelazimishwa kunyanyua mikono anapotamka kauli mbiu ya Chadema
ya ‘People's Power', lakini hata sauti yake imekuwa inatoka kinyonge, tofauti
na wafanyavyo wengine akiwamo Mwenyekiti Mbowe (Freeman)," anaunga mkono
Sauda Magore wa Tabata Shule.
Hao ni
baadhi ya mashuhuda wengi wa hali ya
kiafya ya Lowassa, ambaye anawania kwa udi na uvumba kuingia Ikulu aongoze
angalau kwa kipindi kimoja cha miaka mitano, ambacho hata akipewa ridhaa,
anaweza asikimalize kutokana na afya inavyozidi kudorora.
Hivi
karibuni alipozungumza na wanawake wa Dar es Salaam, Lowassa alitumia dakika 10
tu, lakini alipokwenda kuzindua kampeni ya Ukawa katika viwanja vya Jangwani,
Dar es Salaam, alimudu kufanya hivyo kwa dakika 13 tu huku akiwaambia wananchi
kuwa hotuba ya Ilani ya Uchaguzi ya Chadema iko kwenye tovuti ya chama hicho.
Kama
alivyosema, yeye alifanya hivyo kwa ushauri wa Mbowe na kuiambia hadhira kuwa ‘nyote
ni wasomi mtaisoma huko,’ bila kuelewa kuwa baadhi ya wananchi vijijini hawana
kompyuta wala umeme.
Akiwa
Iringa, alivunja rekodi aliyotangulia kuiweka Jangwani kwa kuhutubia kwa dakika
18; hali hiyo inaonesha kuwa hamudu kusimama kwa muda mrefu akihutubia mikutano,
hivyo kuhitaji muda mwingi kupumzika.
Wanaotetea
hali hiyo wanasema si hoja kwa Rais, kwani wapo marais wengi waliokuwa wagonjwa,
lakini wakatibiwa wakiwa Ikulu na kuendelea na kazi kama kawaida.
Mtetezi
mkubwa wa hali hiyo ni Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye, ambaye awali
alikuwa mpinzani mkubwa wa Lowassa, akijiapiza kuhama CCM kama Waziri Mkuu huyo
aliyejizulu angesimamishwa kupeperusha bendera ya CCM.
"Wanamchafua
Lowassa kuwa ni mgonjwa kwani Magufuli ni mzima? Mbona kila siku wanakwenda
Ulaya kutibiwa. Mbona Rais Mkapa alikwenda nje kufanyiwa upasuaji mkubwa na
akarudi na kuikuta nchi salama kwani yeye ni mzima?
"Rais
Kikwete alikwenda kufanyiwa upasuaji wa tezi dume, kwani yeye ni mzima?"
Sumaye alikuwa akihoji mashabiki wa Ukawa katika viwanja vya Jangwani na
kushangiliwa huku naye kichwa kikivimba na kuendelea kuhanikiza huku
akihitimisha kwa kusema: "Rais haendi Ikulu kubeba zege bali kutengeneza
serikali ambayo itafanya kazi ya kumsaidia."
Mkewe,
Regina Lowassa, naye alidiriki kuujibu umma wenye hofu na mumewe, akitaka
aulizwe yeye eti ndiye anayemfahamu vizuri, akitumia kauli ya marehemu Rais wa
Kenya, Mzee Jomo Kenyatta, ambaye wananchi walihoji umri (uzee) na afya yake,
lakini akataka aulizwe mkewe, Mama Ngina, kama kweli amezeeka. Mzee alifia
usingizini katika miaka ya baadaye ya sabini.
Wanaosikitikia hali hiyo wanasema si vema kupeleka Rais
mgonjwa Ikulu na kwamba fikra kuwa haendi kubeba zege ni muflisi kwa sababu
kazi ya Ikulu ni nzito inayohitaji fikra pevu na zenye kuwa na dira.
Mshauri Mkuu
wa chama cha ACT-Wazalendo, Profesa Kitilla Mkumbo anasema: "Mtu
anayestahili kuingia Ikulu lazima awe na fikra pana kwa ajili ya kutoa dira na
mwelekeo wa Taifa." Kwa afya aliyonayo Lowassa, anaweza kuwa na dira hiyo
na mwelekeo wa Taifa akaujua vilivyo? Bila shaka ni hapana.
Ingawa
hakuna aliye tayari kusema ni nini hasa kinamsumbua Lowassa kiafya, mwonekano
na mwenendo wake kimwili na kisaikolojia ni vitu vinavyoweza kutoa jibu la
haraka kabla ya uthibitisho wa daktari kuwa ana tatizo ambalo linahusiana na
ubongo.
Lowassa ana
kitetemeshi mikononi, hawezi kuinyanyua na mara nyingi hutetemeka. Anapoongea
kuna wakati anapatwa kigugumizi cha midomo na hata ulimi kuwa mzito, ni mara
chache anatabasamu hata pale anapokuwa anasifiwa na wenzake majukwaani.
Hawezi
kupiga makofi hata kinapofikia kipindi cha kushangilia jambo; mikono haina
nguvu."Ukishikana naye mikono ni ya baridi...haina uhai," anasema
mmoja wa wasaidizi wake wa karibu. Hata akiwa viwanja vya Jangwani siku ya
uzinduzi wa kampeni za chama chake, Lowassa alishindwa kuimba wimbo wa Taifa.
Kwa kuyatambua
yote hayo, amekuwa akipokea ushauri wa Mbowe wa kuhakikisha hatumii muda mwingi
kujishughulisha, na ndipo pia wakati wa mikutano huandaliwa mlolongo wa watu
kuzungumza kabla yake ili muda ukikaribia kuzungumza yeye, asitumie dakika
zaidi ya 20 ambazo hata hivyo hajapata kuzifikisha.
Yawezekana
kabisa Lowassa amekumbwa na ugonjwa kama alionao mwanasumbwi bingwa wa zamani
wa uzani wa juu duniani, Muhammad Ali, wa Parkinson, ambao unahusiana na ubongo
na unanyong'onyeza viungo vya mwili na kumsababishia hata kitetemeshi.
Kadri umri unavyosonga
mbele, ndivyo pia ugonjwa huo unavyoimarika. Itakuwaje mtu kama huyu akiachwa
aingie Ikulu kwa sababu tu haendi kubeba zege? Ikulu ni mahali ambako anatakiwa
kuingia mtu timamu, anayeweza kufikiria mwelekeo wa nchi inavyokwenda.
Si hivyo tu,
Rais ndiye uso wa nchi, kama tutakuwa na Rais wa aina hiyo ina maana ndiye
atakuwa sura yetu hata nje ya nchi. "Kama atakwenda nje akiwa na hali hii
kiafya, inamaana Watanzania wote watakuwa si kama yeye bali dhoofulhali,"
anasema Joseph Kavula wa Kariakoo.
Hivyo kauli
ya Sumaye kuhusu viongozi waliokwenda kutibiwa nje haina maana na ni kama
haizungumzii kiini cha matatizo ya marais hao, ingawa hata hivyo kila mmoja wao
ulijulikana ugonjwa wake.
Mkapa
aliumia mguu, Kikwete alikuwa na tezidume na alikiri mbele ya umma wa Watanzania.
Lowassa atwambie anaugua nini? Au Sumaye awambie Watanzania.
Ugonjwa wa Parkinson ni nini?
Ugonjwa wa
Parkinson ni matatizo endelevu ya mfumo wa neva ambao unaathiri mwendo.
Hushambulia polepole, na wakati mwingine hujitokeza kwa kusababisha mtetemo
kwenye mkono.
Lakini
wakati mtetemo ndiyo dalili inayojulikana ya ugonjwa huo, tatizo hilo kwa
kawaida husababisha kukakamaa au kupungua kwa mwendo wa mwili.
Katika hatua
za awali za ugonjwa wa Parkinson, mwili unaweza kuonyesha uhai kidogo au usionyeshe
kabisa, au mikono inaweza isicheze wakati wa kutembea. Kauli inaweza ikawa
ndogo au ya kukokoteza. Dalili za
ugonjwa huo zinaweza kuwa mbaya zaidi kadri muda unavyozidi kupita.
Ingawa
ugonjwa huo hauwezi kutibiwa, matumizi ya dawa yanaweza kupunguza tu makali
yake. Wakati mwingine, daktari anaweza kupendekeza upasuaji ili kurekebisha
baadhi ya maeneo ya ubongo na kupunguza dalili hizo.
Dalili za
ugonjwa huo zinaweza kutofautiana baina ya mtu na mtu. Dalili za mwanzo
zinaweza kuwa ndogo na zisionekane haraka. Dalili hizo mara nyingi huanzia
upande mmoja wa mwili na kwa kawaida huendelea kushambulia eneo hilo zaidi hata
kama ugonjwa huo utaambukiza upande wa pili.
Dalili hizo zinaweza kuwa pamoja
na:
1. Mtetemo:
Mtetemo au mtikisiko, kwa kawaida huanzia kwenye mkono au mguu, mara
nyingi mkononi au vidoleni. Unaweza kubaini kidole gumba na shahada
vikisuguana. Moja ya tabia za ugonjwa huo ni mtetemo wa mkono hasa wakati umetulia.
2. Mwendo wa polepole: Wakati mwingi ugonjwa wa Parkinson
unapunguza uwezo wa kusogea na hivyo kupunguza mwendo na kusababisha hata kazi
ndogo kuwa ngumu kufanyika na kutumia muda mwingi kuifanya.
Hatua za
kutembea hupungua, au kuwa vigumu kunyanyuka kitini. Pia, unaweza kukokota miguu
unapojaribu kutembea, na hivyo kusababisha ugumu kutembea.
3. Misuli kukakamaa: Ukakamaaji wa misuli unaweza kutokea
katika sehemu yoyote ya mwili. Misuli iliyokakamaa inaweza kupunguza kiwango cha mwendo na kusababisha
maumivu.
4. Mwili kunyong’onyea: Mwili unaweza kunyong’onyea na
wakati mwingine kuonekana kama mwenye kibiongo au kukabiliwa na tatizo la
kukosa mizania ya mwili.
5. Kupoteza msukumo wa mwili: Mgonjwa wa Parkinson anaweza
kukabiliwa na upotevu wa uwezo wa mwili kutenda mambo, ikiwa ni pamoja na
kushindwa kupepesa macho, kutabasamu au kuchezesha mikono wakati wa kutembea.
6. Mabadiliko kwenye sauti: Mgonjwa anaweza kukabiliwa na
matatizo ya kuzungumza. Anaweza kuzungumza kwa sauti ndogo, harakaharaka au
kusita kabla ya kuzungumza. Sauti yake inaweza kuwa ya toni moja tu
isiyobadilika kama ilivyo kawaida kwa msemaji asiye na matatizo.
7. Mabadiliko kwenye hati: Inaweza kuwa vigumu kuandika kwa
mkono, na mwandiko unaweza kuonekana mdogo.
Kiini cha ugonjwa
Ugonjwa huu
husababishwa na upotevu wa seli za neva kwenye ubongo ambao hujulikana kama substantia nigra.
Seli hizo
katika eneo hilo la ubongo ndizo zinawajibika katika uzalishaji wa kemikali
zinazoitwa dopamine. Dopamine
hufanya kazi kama mesenja kati ya sehemu hizo za ubongo na mfumo wote wa neva ambao
husaidia kudhibiti na kuratibu mwendo wa mwili.
Iwapo seli
hizi zitaharibiwa, kiwango cha dopamine
kwenye ubongo hupungua. Hiyo inamaanisha kwamba sehemu hiyo ya ubongo
inayodhibiti mwendo sasa haiwezi kufanya kazi kama kawaida na hivyo kusababisha
mwendo kupungua na kukosa kuwa wa kawaida tena.
Upotevu wa
seli hizo za neva ni mchakato uendao polepole sana. Dalili za ugonjwa huo kwa
kawaida huanza kuonekana pale takriban asilimia 80 ya seli za neva katika substantia nigra inakuwa imepotea.
Nini husababisha seli hizo kupotea?
Haijulikani
ni kwa nini upotevu wa seli hizo unaohusishwa na ugonjwa wa Parkinson hutokea,
ingawa utafiti unaendelea ili kubaini kiini hasa.
Kwa sasa,
inaaminika kwamba mkusanyiko wa mabadiliko ya kinasaba na sababu za kimazingira
vinaweza kuchangia hali hiyo.
Kinasaba
Mabadiliko
mengi ya kinasaba yamebainika kuongeza hatari ya mtu kupata ugonjwa huo, ingawa
hata hivyo ni kwa vipi hiyo ndiyo inaweza kuwa sababu, bado haijawekwa bayana.
Ugonjwa huu
unaweza kutokea katika familia kama matokeo ya matatizo ya kinasaba kwa
kurithishwa kwa watoto kutoka kwa wazazi wao, hata hivyo urithishaji ugonjwa
huu ni adimu sana.
Kimazingira
Baadhi ya
watafiti nao wanahisi kuwa sababu za kimazingira zinaweza kuongeza uwezekano wa
kutokea kwa ugonjwa huu.
Imeshapata kuelezwa
kuwa dawa za kuua wadudu na za mimea zinazotumiwa mashambani na uchafuzi wa
hali ya hewa unaosababishwa na magari au viwanda navyo huweza kuchangia hali
hiyo.
Hata hivyo,
ushahidi unaohusisha sababu za kimazingira na ugonjwa huo bado
haujathibitishwa.
Sababu zingine
'Uparkinsoni'ni jina mwavuli linalotumiwa kuelezea
dalili za mtetemo, kukakamaa misuli na upungufu wa mwendo.
Ugonjwa wa Parkinson ni aina inayojulikana sana ya 'uparkinsoni', lakini zipo aina zingine
adimu ambazo sababu zao zinaweza kutambulishwa.
Hizo ni
pamoja na zile zinazosababishwa na:
1.
Dawa-ambako dalili zinaonekana baada ya kutumia aina fulani ya dawa, kama vile
dawa za magonjwa ya akili na kwa kawaida hali huwa nzuri pale dawa hizo
zinapokuwa zimeacha kutumika.
2. Matatizo
ya ubongo, kama vile ugonjwa wa kupooza na matatizo ya kukosa nguvu mwilini na kiharusi ambacho husababisba
sehemu nyingi za ubongo kufa.
Mmoja wa
watu maarufu wanaokabiliwa na ugonjwa huo kwa sasa ni bingwa wa zamani wa
masumbwi wa uzani wa juu duniani, Muhammad Ali.
No comments:
Post a Comment