Thursday, 10 September 2015

MAGUFULI KUBORESHA MASLAHI YA MAJESHI





MGOMBEA urais wa CCM, Dk. John Magufuli, ameahidi kuimarisha majeshi ya ulinzi na usalama ili kuhakikisha yanatekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa.
Aliyasema hayo jana kwa nyakati tofauti katika mikutano ya kampeni katika majimbo ya Bumbuli, Korogwe Mjini, Korogwe Vijijini, Mkinga na Lushoto, alipohutubia maelfu ya wananchi.
Alisema suala la msingi ni kwa serikali kuendelea kuboresha maslahi na vitendea kazi kwa majeshi, ikiwemo kujenga nyumba za kisasa kwa ajili ya makazi katika kambi mbalimbali nchini.
“JWTZ, Magereza, Polisi na Jeshi la Zimamoto yote haya nitahakikisha tunajenga nyumba bora kwa makazi ya askari na kuboresha maslahi ili wafanye kazi kwa moyo,”alisema.
Akiwa wilayani Mkinga, Dk. Magufuli alisema  anatambua kuna kambi ya JWTZ na serikali ya awamu ya nne imejenga nyumba nzuri kwa ajili ya askari hivyo, serikali yake itaendelea kuboresha majeshi.
Pia, alisisitiza haja ya wananchi juu ya ulinzi wa amani ya nchi na kuwataka wasikubali kuvurugwa kwa kuwa gharama za kuirejesha ni kubwa na wakati mwingine haiwezekani kabisa.
“Ndugu zangu mimi nimewahi kukaa Libya kwa wiki tatu…ilikuwa nchi ya amani, watu waliishi maisha bora, lakini walitokea watu wachache wakavuruga na mpaka leo Libya haikaliki,” alisema.
Aliwataka wananchi wasikubali Tanzania iingie kwenye machafuko kama ilivyotokeza nchi jirani wakati wa ghasia za uchaguzi ambapo watu wengi walipoteza maisha.
Dk. Magufuli alisema pia atajenga serikali yenye nidhamu ya watu kufanya kazi na kila mmoja akitekeleza majukumu yake, Tanzania itakuwa na mabadiliko makubwa kwa kuwa hata maandiko yanasema asiyefanya kazi na asile.
Katika hatua nyingine, Dk. Magufuli aliahidi kuboresha sekta ya kilimo na kupandisha bei ya zao la chai ili wananchi wanufaike na kilimo hicho ili kukuza uchumi wao.
“Najua kuna changamoto ya kiwanda cha chai cha Mponde kilichochukuliwa na mwekezaji, ahadi yangu kwenu nikiingia madarakani nitahakikisha kinafufuliwa na kufanya kazi,” alisema.
Mbali na kiwanda hicho, Dk. Magufuli aliahidi kwamba akiingia madarakani serikali yake itajenga barabara ya kutoka Soni hadi Bumbuli, umbali wa kilometa 22.89, kwa kiwango cha lami ili kuwawezesha wananchi kufanya shughuli zao.
Akizungumzia kero kwa wafanyabiashara ndogo ndogo, Dk. Magufuli, alisema kwenye serikali yake wataweka utaratibu mzuri ili wafanye biashara zao bila kugubudhiwa.
“Mama ntilie, wauza mbogamboga, bodaboda mambo ya kukamatwa kamatwa na kudaiwa kulipa ushuru kwenye serikali yangu haitakuwepo na badala yake wafanyabiashara wakubwa ndio watalipa kodi,” alisema.
Kwa nyakati tofauti, Dk. Magufuli aliwanadi wagombea ubunge wa Korogwe Mjini, Marya Chatanda, Korongwe Vijiji, Stephen Ngonyani, Mkinga, Dustani Kitandula na Lushoto, Shaban Shekilindi.

NABII AMTABIRIA USHINDI MKUBWA
NABII wa Kanisa la Ufunuo na Maono, Paul Bendera, amesema Dk. Magufuli ndiye atakuwa Rais wa Awamu ya Tano na kwamba, ameoteshwa kuwa ataibuka na ushindi wa kishindo.
Amesema Dk. Magufuli atamshinda vibaya mpinzani wake Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa, ambaye hana ushawishi mkubwa na usio na makandokando.
Pia, amewashukia baadhi ya viongozi wa dini wanaotumika kwa nguvu ya fedha, akieleza kuwa ni hatari na amewataka kuacha kuwagawa Watanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Dar es Salaam, Bendera alisema katika ndoto hiyo kulikuwa na mito miwili kutoka katikati ya bahari na sauti ya Mwenyezi Mungu ikimwambia atazame kwa makini mito hiyo miwili.
“Baadaye nikaona kati ya mito hiyo miwili, mto mmoja ulikuwa mkubwa sana, lakini haukuwa na mkondo wa maji na hauna pa kupita, unapita juu ya ardhi na umepoteza mwelekeo.
“Mto mwingine kutoka baharini ukiwa umetengenezewa mkondo na unapita sehemu sahihi na kusambaa na nikaambiwa maana kuu ya ile mito miwili ni wagombea urais na bahari ni wananchi,” alisema.
Alisema katika ndoto hizo akaambiwa ni utabiri wa taifa na mbele kuna wagombea wawili, Lowassa na Dk. Magufuli na sauti ilimwambia mto usio na mwelekeo ni Ukawa na mto wenye mwelekeo ni CCM.
Bendera alisema wagombea hao wote wana nyota ya urais, lakini kwa sasa UKAWA hauwezi kupata nafasi ya kuongoza nchi na rais atakuwa ni Dk. Magufuli.

No comments:

Post a Comment