Thursday, 10 September 2015

GWAJIMA KITANZINI, VIONGOZI WA DINI WAMSHUKIA KAMA MWEWE




NA SOLOMON MWANSELE, MBEYA

ASKOFU wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima (Mshenga), ametakiwa kuwaeleza Watanzania kuhusu tuhuma za rushwa dhidi ya maaskofu anaodaiwa kuwakusanya na kuwapa fedha kwa ajili harakati za kisiasa.

Pia, ametakiwa kueleza watu wanaompatia fedha hizo ambazo inadaiwa amekuwa akizitumia kuwahonga baadhi ya viongozi wa dini kwa maslahi ya kisiasa ya kundi la watu wachache.

Kauli hiyo imetolewa na Askofu wa Tanzania Acts Church, Pius Ikongo, wakati akizungumza na UHURU kuhusiana na hali ya kisiasa nchini na tuhuma zilizoibuliwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk.Willibrod Slaa, kuhusu tuhuma dhidi ya baadhi ya maaskofu kudaiwa kupewa rushwa.

Askofu Ikongo alisema mwaka tangu juzi, Askofu Gwajima alikuwa ameshajiingiza kwenye masuala ya kisiasa na kuhoji iwapo Katiba ya Kanisa la Ufufuo na Uzima inaruhusu viongozi wake kujihusisha na siasa.

“Askofu Gwajima hapaswi kukanusha kuwa, baadhi ya maaskofu hawajapokea rushwa ama hawatumiwi. Hawezi kukanusha hilo kwa sababu ni jambo ambalo limekuwa wazi siku nyingi,” alisema.

Alisema Dk. Slaa sio wa kwanza kuzungumzia tuhuma hizo kwa baadhi ya maaskofu kupokea rushwa kwani, hata Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, liliwahi kuweka wazi majina ya baadhi ya maskofu waliohusika katika kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow.

Kwa mujibu wa Askofu Ikongo, maaskofu hao walitajwa hadi akaunti zao na kiasi cha fedha walichopewa kila mmoja, lakini hakuna mtu, askofu au mwanasiasa aliyesimama kutetea suala hilo.

Alisema watu wanaowatetea baadhi ya maskofu licha ya kuhusishwa na vitendo vya rushwa, walipaswa kwanza kulikosoa bunge ambalo awali liliwahi kuanika uozo huo.

Alisema Dk. Slaa hakusema kwamba maaskofu wamepokea rushwa, bali amewaeleza Watanzania kwamba ameambiwa na Askofu Gwajima na kama ameambiwa yeye (Ikongo), anao uhakika kuwa Gwajima amemuambia.

“Dalili zote za rushwa sio lazima upewe fedha. Mwezi Julai, mwaka huu, Gwajima alitoa gari lake namba za usajili ninazo, kwa kuwakusanya baadhi ya maaskofu kutoka Dar es Salaam na kuwasafirisha mkoani Arusha kwenye mkutano wa kisiasa,” alisisitiza.

Aliongeza kuwa, maaskofu waliosafirishwa na Gwajima, walilipiwa fedha za safari, gharama za malazi na chakula hivyo kitendo hicho kinaashiria rushwa ya wazi.

Askofu Ikongo alisema maaskofu hao hawakupelekwa Arusha kwenye mkutano wa kidini bali kwenye mkutano wa kisiasa na kwa muktadha huo hiyo ni rushwa ya moja kwa moja.

Alisema Askofu Gwajima anachojitahidi ni kujaribu kukusanya maaskofu, viongozi wa dini na kuwalaghai ili kwamba na wao wamfuate kwenye siasa kwa kuwa yeye (Gwajima) anajua anashabikia upande gani wa kisiasa.

“Gwajima anataka maaskofu wote waende upande ule anaokwenda yeye, na ndio maana alitumia hila kubwa sana kuwadanganya viongozi wetu wa CPCT,” alisema Askofu Ikongo.

Alisema Wapenkoste nchini wanafahamu kuwa wanasiasa wa pande zote ni waumini wao na ndani ya makanisa kuna wanachama wenye itikadi za vyama tofauti hivyo, viongozi hawawezi kujionyesha wala kuwaongoza waumini waende upande gani.

“Askofu Gwajima amewagawa Wapentekoste kwa kuanzisha kikundi chake cha baadhi ya maaskofu ambao walikuwa wakikutana mara kwa mara kwenye hoteli moja ya kifahari Dar es Salaam. Huko mengi huzungumzwa na fedha hutolewa ili kuweka mikakati sawa na jinsi ya kuiunga mkono CHADEMA,”alisema.

Alisema serikali inapaswa kuchunguza Katiba ya Kanisa la Gwajima kama inaendana na matendo yanayofanyika kwani, sheria za nchi zinakataza dini kuchanganywa na siasa na tayari hali ya hatari imeanza kuonekana.

“Kila mmoja dhehebu lake likiwemo kanisa la Ufufuo na Uzima limesajiliwa serikalini, hivyo viongozi wa serikali wanapaswa kuchukua katiba ya kanisa hilo na kuisoma ili kuona anayoyaongea Gwajima na kwenye katiba yake ni sahihi,” alisema.

Dk. Kamani amtaka Gwajima kujitambua
MWENYEKITI wa CCM mkoa wa Simiyu, Dk Titus Kamani, amempasha Askofu Gwajima asitumikie ‘mabwana’ wawili, harakati za siasa na dini.

Mshenga huyo na ‘muoaji’ anayemtuma, wasidhani Tanzania inatawaliwa kwa zamu za udini na kama walitarajia CCM kitateua mgombea urais kwa misingi ya udini, walikuwa wakiota ndoto, Serikali ya CCM si ya kidini, anayeomba kura za upendeleo wa udini anataka kuleta janga nchini.

Amedai, inashangaza wakati viongozi wa dini wamekuwa wakiaswa kutochanganya dini na siasa, kuwahimiza waumini wachague viongozi bora na kuombea taifa liwe na amani, mshenga huyo ameingia katika mahaba ya Edward Lowassa na kutumia kila njia kushawishi Watanzania wamchague.

Dk Kamani, ambaye pia ni Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, alisema hayo jijini Mwanza jana, wakati akizungumza na Uhuru na kuwaomba Watanzania wasidanganyike kwa ushawishi wa watu wanaotaka kuchagua kiongozi wa nchi kwa maslahi yao na si kwa maslahi ya umma.

“Kitendo cha kumshawishi Dk. Slaa na mkewe ambaye Gwajima anadai ana mapepo, warudi kwenye ulingo wa siasa za Chadema ni dhahiri anatumikia mabwana wawili, harakati za siasa na dini,” alieleza Dk Kamani.

Alifafanua kuwa, CCM hakijawahi kuchagua mgombea yeyote kwa ajili ya udini maana Tanzania haitawaliki kwa udini au zamu za udini, kitendo alichoanza kufanya Lowassa ni hatari kubwa kwa mustakabali wa taifa.

Mwenyekiti huyo alihoji “Nani mwenye mapepo kati ya Askofu Gwajima anayetumiwa kufanya harakati za siasa na kushawishi watu kwa rushwa au Josephine Mshumbusi anayemshawishi mume wake kuachana na siasa za unafiki na kukumbatia ufisadi ?”

Alhad: Gwajima hana maadili
SHEIKH wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, amemueleza Askofu Gwajima kama kiongozi wa kiroho aliyekosa maadili kwa kuweka hadharani siri za watu anaopaswa kuwaongoza katika misingi ya imani.

Amemtaka Askofu Gwajima kujirekebisha na kurejea kwenye misingi ya uongozi wa kiimani kwa kufanyakazi za dini badala ya kujiweka mbele katika siasa.

“Hivi sasa Askofu Gwajima anaonekana hana uwezo wa kuhifadhi siri za wanakondoo anaowangoza, ambao wanamfikishia matatizo yao ili awasaidie kama kiongozi wa kiimani,” alisema.

Alhad Salum aliyasema hayo jana, wakati akizungumza na Uhuru kuhusiana na hatua ya Askofu Gwajima, kuweka hadharani kile alichodai ni siri za ndani kabisa kuhusiana na Dk. Slaa.

“Ukweli ni kuwa ameonyesha hana maadili na huruma kwa waumini wake. Kiongozi wa dini lazima uhifadhi siri unazopewa, aliyoyasema yawe ya kweli au la, kikubwa amefanya jambo baya,” aliongeza.

Aliongeza kuwa kitendo cha Askofu Gwajima kujitokeza hadharani na kutoa kauli zile kimedhihirisha ukosefu wake wa maadili na kwamba, anaweza kupoteza heshima mbele ya jamii.

Alisema kitendo alichokifanya kiongozi huyo hakina sura nzuri mbele ya jamii kwa sababu, wao hufanya kazi kama za manabii ambao walikuwa wakisikiliza matatizo ya watu na kuyatafutia ufumbuzi bila kuyaanika.

Sheikh Alhadi alisema, kitendo cha kutoa aibu za watu waliomuamini si cha kiungwana na kinadhohofisha imani ya wananchi waliyonayo kwa viongozi wa dini.

No comments:

Post a Comment