Na waandishi wetu
MWENYEKITI wa UWT Mkoa wa
Singida, Diana Chilolo, amewaponda wanachama wa CCM waliohama na kukimbilia
upinzani baada ya kuangukia pua kwenye kura za maoni kuwa wanafanya siasa za
kitoto.
Diana, ambaye alikuwa akimuunga
mkono Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa, alisema
kushinda ama kushindwa kwenye uchaguzi ni jambo la kawaida.
“Asiyekubali kushindwa huyo si
mshindani, katika kitu jambo kushinda na kushindwa ni mambo ya kawaida,”
alisema Diana, ambaye amekuwa mbunge wa Viti Maalumu mkoani hapa kwa vipindi
vitatu kabla ya kuanguka.
Alikuwa akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika viwanja vya
Soko la Kijiji cha Makiungu, Wilaya ya Ikungi. Mkutano huo ulikuwa maalumu kwa
mgombea mwenza wa urais, Samia Sahuhu Hassan, kuomba kura.
Diana, alisisitiza kuwa wana- CCM walioangushwa kwenye uchaguzi wa
kura za maoni wakakichukia Chama na kukiona hakifai na kukimbilia upinzani,
muda wote walipokuwa CCM, hawakuwa wanachama wa kweli , walikuwa wana-CCM
maslahi.
“Kwa upande wangu, kwenye uchaguzi wa kura za maoni hivi karibuni,
kura zangu hazikutosha na kwa kitendo hicho nilifeli kutetea nafasi yangu. Tukio
hilo kwangu niliona ni la kawaida kabisa, lakini nilitoka nje ya ukumbi wa
mkutano na nilikutana na kundi la wajumbe wa UWT, wananililia kisa mimi
nimeshindwa kutetea nafasi yangu,” alisema.
Aidha, Diana alitumia nafasi hiyo kukanusha vikali uvumi unaooenezwa
kwamba, wakati wowote atahama CCM na kukimbilia upinzani.
“CCM binafsi imenijengea umaarufu na heshima kubwa, siwezi
kukikimbia asilani. Kwanza sina uroho wa madaraka, kwangu kupata kura ambazo
hazikukidhi mahitaji, naliona tukio hilo limetokana na mapenzi ya Mungu,”
alisisitiza.
Kwa upande wake, mbunge wa zamani wa Jimbo la Nkenge mkoani
Kagera, ambaye pia ameshindwa kwenye kura za maoni, Assumpta Mshama, amewataka
wakazi wa Singida Mashariki, kufanya uamuzi sahihi ifikapo Oktoba 25, mwaka huu.
Alisema lengo liwe ni kuliletea maendeleo jimbo hilo ambalo
kwa miaka mitano iliyopita lilidorora katika maendeleo.
Alisema wakazi wa jimbo hilo kwa kipindi cha miaka mitano
walichagua mbunge, ambaye kazi yake kubwa ilikuwa ni kususia vikao vya bunge
wakati shughuli zikiendelea na kutumia muda mwingi kwa kubishana.
“Kwa miaka mitano ya Tundu Lissu bungeni, hakuweza kupata nafasi
ya kuwakilisha kero zenu, kazi yake ilikuwa ni kususia vikao na kuanzisha
mabishano yasiyo na tija kwa wapiga kura,” alisema huku akishangiliwa na umati
uliofurika.
Aliwataka wananchi kutumia fursa hiyo kuziba ‘tundu' kwa kumchagua
Jonathan Andrew Njau wa CCM, ambaye tayari ameanza kuwatumikia vema kupitia
nafasi yake ya UNEC.
WAFUASI UKAWA WAZUSHA VURUGU
WATU wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa
UKAWA, juzi waliwashambulia kwa magongo, ngumi na visu baadhi ya wafuasi
wa CCM, waliokuwa wakifanya mkutano wa
hadhara Kata ya Jangwani, Dar es Salaam.
Uhuru, ambalo lilishuhudia
varangati hilo, lilishuhudia vijana hao, wakitumia nguvu kutaka kupita katikati
ya mkutano na kukaidi amri ya vijana wa
CCM waliokuwa wakiwazua kwa madai kuwa
eneo hilo lilikuwa limefungwa kwa muda kutokana na mkutano uliokuwa ukiendelea.
Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa CCM, akiwemo
mbunge wa jimbo hilo, Mussa Azan ‘Zungu’, wagombea wote wa udiwani jimbo la ilala na
vuiongozi wa Chama Wilaya ya Ilala.
Katika hali ya kushangaza, vijana
hao walianza kutoa maneno ya kejeli
dhidi ya CCM na kwamba hawatambui Chama hicho bali UKAWA, hivyo hawawezi kuzuiliwa kufanya
lolote mahali hapo.
Huku wakionekana dhahiri kutaka
kuvuruga mkutano huo, vijana hao walianza kupambana na walinzi ili waweze kujipenyeza kwenda sehemu ya
katikati ya mkutano, ambako mbele yake kulikuwa na meza ya viongozi.
Kufuatia hatua hiyo, vijana wa CCM
walisimama imara kuwazuia na ndipo vijana hao walipoanza kuwashambulia vijana
wa CCM kwa ngumi, mateke na vipande vya
mbao kabla ya kuchukua visu na mapanga.
Vurugu hizo zilisababisha mkutano
huo kusimama kwa muda, ambapo wafuasi wa CCM walianza kujitetea huku wengine
wakiwanusuru vijana hao ambao walianza
kuzidiwa kwa kipigo.
Polisi walifika muda mfupi na
kutuliza ghasia, hivyo mkutano kuendelea kama kawaida huku wafuasi wa CCM
wakilaani vibaya tukio hilo.
“Hawa vijana wa UKAWA wana matatizo sana. Muda wote
wao wanataka kujiona ndiyo wanaoongoza
nchi kwa sasa na huyo Lowassa (Edward)
wao. Wanatudharau sana watu wa CCM.
“Wanataka hapa mjini kila kitu
wafanye wao. Wao ndiyo wana haki ya kuzungumzia uchaguzi na kufanya mikutano.
Ukizungumza mtu wa CCM basi hawachelewi
kurusha ngumi,”alisema Othma Faki, mkazi wa kata hiyo.
Mkazi mwingine wa kata hiyo mwenye
asili ya kiasia, alilaani vurugu
hizo na kueleza kwamba huenda vijana hao walijipanga kuvuruga
mkutano huo wa kata.
“Hawa vijana wa
UKAWA hawaelewi lolote la maana
na hawajui kanuni za uchaguzi wala
kampeni, ndiyo maana wamekuwa wakitutukana wanachama wa CCM mitaani, lakini wao
wanajiona wasafi. Huu ujasiri wa
kushambulia mkutano wameutoa wapi?” Alihoji mtu huyo.
Wananchi hao walioomba serikali
kuwachunguza vijana ambao wanajifanya
wana msimamo mkali kiasi cha kutishia usalama katika mikutano ya kampeni inayoendelea nchini hivi sasa.
No comments:
Post a Comment