Friday, 11 September 2015

MAHAKAMA YAPOKEA BEGI LA GWAJIMA KAMA KIELELEZO



 
NA FURAHA OMARY
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepokea kama sehemu ya kielelezo begi lililopelekwa katika Hospitali ya TMJ, Dar es Salaam, alikokuwa amelazwa Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, likiwa na vitu mbalimbali vikiwemo bastola, risasi na nguo ya ndani.
Begi hilo lilipokelewa jana mahakamani hapo pamoja na vitu vilivyomo ndani mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha, baada ya ofisa wa polisi, Sospeter kuiomba kufanya hivyo, wakati alipokuwa akitoa ushahidi.
Ofisa huyo wa polisi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalumu ya Dar es Salaam (ZCO), alikuwa akitoa ushahidi katika kesi inayomkabili Gwajima na viongozi wengine wa kanisa hilo.
Katika kesi hiyo, Gwajima anakabiliwa na shitaka la kushindwa kuhifadhi silaha ya moto na risasi anazomiliki kihalali katika usalama, huku Askofu Msaidizi Yekonia Bihagaze , mfanyabiashara George Mzava  na Mchungaji Geofrey Milulu, wakikabiliwa na mashitaka ya kukutwa na silaha na risasi hizo bila ya kuwa na kibali.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro kutoa ushahidi, ofisa huyo wa polisi, alifungua begi hilo la kijani ambalo linadaiwa kupelekwa hospitalini hapo Machi 29, mwaka huu, saa tisa usiku na Bihagaze, Mzava na Milulu huku akionyesha kitu kimoja badala ya kingine.
Shahidi huyo alionyesha mahakamani hapo fulana, fulana ya ndani, suruali na makoti mawili, bastola moja ikiwa na risasi tatu ndani ya magazine, IPad, soksi mbili, nguo ya ndani, CD mbili, risasi 17 za shotgun na leseni za kumiliki silaha.
Pia, shahidi huyo alidai katika begi hilo kulikuwa na hati ya kusafiria ya Gwajima na vitabu vitatu vya hundi ambavyo kwa mujibu wa maelezo ya mabosi wake aliomba arejeshewe.
Katika ushahidi wake, shahidi huyo alidai kwamba Machi 28, mwaka huu yeye na ofisa wa polisi, Benny walipangiwa kazi ya ulinzi katika Hospitali ya TMJ, Mikocheni, ambapo aliingia lindoni hapo saa 11.30 jioni kwa ajili ya kumlinda mtuhumiwa Askofu Gwajima, aliyekuwa amelazwa hospitalini hapo kwenye chumba namba 213.
Shahidi huyo alidai hospitalini hapo kulikuwa na walinzi wawili binafsi wa Gwajima ambao walikuwa wakibadilishana kila baada ya saa mbili.
“Siku hiyo ilipofika saa sita usiku, lilikuja kundi la watu 12 akiwemo mkewe Gwajima, ambapo baada ya kuwahoji kwa nini wanakuja hospitalini muda huo, niliamua kumuita mlinzi wa hospitali na kumwambia awaondoe.”
“Mke wa Gwajima aliingia ndani kumuona mumewe ambapo alipotoka aliondoka na watu watano ambao walikaidi kutoka katika korido. Ilipofika saa tisa usiku (Machi 29, mwaka huu), walitokea watu watatu mmoja wao akiwa anaburuza begi,” alidai shahidi huyo.
Aliendelea kudai kuwa aliwauliza watu hao juu ya begi hilo kabla hawajafika katika mlango wa chumba alicholazwa Gwajima, hata hivyo mmoja wao ambaye alikuwa akiburuza begi hilo alimjibu kwamba ‘usitake kujua mambo yetu.’
Shahidi huyo alidai begi hilo lilikuwa likiburuzwa na mshitakiwa wa tatu na walipofika mlangoni alimkabidhi mshitakiwa wa pili.
Alidai baada ya kutafakari, alijua kuna kitu sio cha kawaida hivyo, aliamua kujifanya ananyoosha miguu kwa kusogea hatua tano, ambapo aliwasiliana na ZCO ili aweze kumwongezea nguvu ya ziada.
Shahidi huyo alidai baadae walikuja askari ambapo waliamua kuwaweka washitakiwa hao kuanzia namba mbili hadi nne chini ya ulinzi na kukagua begi hilo ambalo walilikuta na vitu hivyo.
Akihojiwa na wakili wa utetezi, Peter Kibatala, shahidi huyo alidai ukaguzi wa begi ulifanyika mlangoni hapo na kwamba hafahamu hadi leo nguo zilizokuwa katika begi hilo zilikuwa za nani.
Kesi hiyo imepangwa kuendelea kusikilizwa Oktoba 6, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment