Friday, 11 September 2015

CHADEMA WAJERUHI 10 KWA MAPANGA MKUTANO WA CCM



NA MWANDISHI WETU, TARIME
WATU wanaosadikiwa ni wafuasi wa CHADEMA wamevamia mkutano wa kampeni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na kuwakata mapanga watu zaidi ya 10 ambao hali zao ni mbaya.

Tukio hilo la kinyama lilisababishwa na mgombea udiwani wa CHADEMA, Mangenyi Ryoba, kufyatua risasi hewani na kusababisha vurugu.

Mkutano huo wa CCM ulikuwa unafanyika katika jimbo la Tarime Vijijini, lakini uliingia dosari baada ya wafuasi hao wanaodhaniwa ni wa CHADEMA kuuvamia mkutano huo na kuwajeruhi watu kwa mapanga.

Tukio hilo la kusikitisha lilitokea jana katika Kata ya Nyanungu Tarafa ya Ingwe wilayani Tarime mkoani Mara na kusababisha mapigano.

Mkutano huo ulikuwa unafanyika katika Kijiji cha Kegonga ambapo risasi za moto zilitumika na kusababisha baadhi ya watu kujeruhiwa ambapo wamelazwa wakiwa mahututi.

Wakizungumza waandishi wa habari katika Hospitali ya Wilaya Tarime baadhi ya majeruhi ambao walikuwa wakipatiwa matibabu walisema tukio hilo ni la kinyama na kusikitisha.

Nyaitati Maranya ambaye amejeruhiwa kichwani, mkononi na mgongoni baada ya kuchomwa na kitu chenye ncha kali alisema anajisikia maumivu makali.

Majeruhi wengine katika tukio hilo ni Chacha Mwita aliyekatwa kwa panga mgongoni na kichwani, Marwa Maricho aliyekatwa kichwani mara tatu, mgongoni na miguuni na hali yake ni mbaya.

Aidha katika tukio hilo, Kimunye Chacha (55), ambaye amekatwa kichwani, mgongoni na mikono yake yote miwili. Majeruhi hao wote ni wanachama wa CCM.

Wakizungumza kwa shida katika hospitali hiyo,  walisema walikuwa katika mkutano wa kampeni wa CCM uliokuwa unafanyika maeneo ya Shule ya Mangucha, Kata ya Nyanungu.

Kwa mujibu wa majeruhi hao, mkutano huo ulikuwa wa kumnadi mgombea udiwani wa CCM, Ngicho   Marwa, ambaye alikuwa anazindua kampeni zake.

Walisema katika mkutano huo pia alihudhuria mgombea ubunge wa CCM katika jimbo la Tarime Vijijini, Christopher Kangoye.

Hata hivyo, walisema katika hali isiyokuwa ya kawaida wafuasi wa CHADEMA walifika katika eneo hilo wakiwa na bendera za chama chao.

Walisema CHADEMA walikuwa na mkutano jirani na maeneo jirani na mkutano wa CCM ambapo kulitokea mwingiliano na mgombea udiwani wa CHADEMA, Mangenyi Ryoba.

Aidha walisema Ryoba alifyatua risasi hewani na kusababisha vurugu kati ya wafuasi CHADEMA na CCM.

Walisema kitendo cha mgombea udiwani huyo kufyatua risasi hewani kilisababisha wafuasi wa CHADEMA kuanza kuwashambulia wafuasi wa CCM kwa mapanga na kuwajeruhi vibaya.

Walisema majeruhi wengine wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Misheni ya Masanga.

Mganga  wa zamu Dk. Mwita Kemenya, alisema hali za majeruhi ni mbaya na baadhi wanahitaji uangalizi wa daktari.
Tukio hilo limetokea ikiwa ni siku moja baada ya mgombea ubunge wa CHADEMA katika jimbo la Bunda Mjini, Ester Bulaya, kueneza habari za uzushi kuwa alimuokoa asichomwe moto mtoto wa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika ambaye pia ni mgombea ubunge wa jimbo hilo, Stephen Wasira, Kambarage Wasira.

Imeelezwa kuwa, Ester ameanza mkakati wa kuwachafua viongozi wa CCM wilayani hapa baada ya kutoungwa mkono na wananchi katika kuwania nafasi hiyo ya kisiasa.

Inadaiwa kuwa katika tukio hilo, Ester aliongoza kundi la mabaunsa wa CHADEMA kuvamia mkutano wa ndani wa CCM.

Kundi hilo lililokuwa na silaha za jadi yakiwemo mapanga, sime na marungu, walianza kuwashambulia wanachama wa CCM waliokuwa katika mkutano huo.

Katika uvamizi huo, mwanachama wa CCM, Chenge Joseph, amelazwa katika Hospitali teule ya Wilaya ya Bunda baada ya kujeruhiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari, jana, Kambarage alisema baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya aliomba msaada polisi ambapo polisi waliwaokoa.

Alisema katika kikao hicho cha ndani alikuwa akikutana na wanachama kujadili masuala mbalimbali pamoja na kutoa mashati ya CCM kwa ajili ya shughuli za kampeni.

Kamanda wa polisi mkoani Mara, Philipo Kalangi, alisema watu watatu wamekamtwa na watafikishwa mahakamani wakati wowote.

No comments:

Post a Comment