Saturday 10 October 2015

MAGUFULI AAHIDI NEEMA BAGAMOYO


 NA CHARLES MGANGA, BAGAMOYO
MGOMBEA urais wa CCM, Dk. John Magufuli amesema gesi iliyopatikana Bagamoyo, itasaidia kujenga viwanda vidogo, vya kati na vikubwa katika jimbo la Chalinze na wilaya ya Bagamoyo kwa ujumla.
Akizungumza na wananchi katika maeneo ya Mbwewe na Msata, Dk. Magufuli alisema gesi hiyo ikitumika ipasavyo itainua uchumi wa Chalinze.
Alisema kutokana na kugundulika nishati hiyo, ni wazi kuwa umeme utakuwa wa uhakika, hivyo kuwezesha ujenzi wa viwanda katika maeneo hayo.
"Bahati nzuri kuna gesi imepatikana, itasaidia kwa kiasi kikubwa kujenga uchumi wa Chalinze, " alisema Dk. Magufuli.
Aidha, alisema barabara ya kutoka Makurunge mpaka hifadhi ya taifa ya Saadani, itakamilishwa kwa kiwango cha lami. Alisema tayari upembuzi yakinifu umefanywa hivyo shughuli ya ujenzi itaanza wakati wowote kuanzia sasa.
Kwa mujibu wa Magufuli, barabara hiyo itakapokamilika, itawawezesha wasafiri kuamua barabara kwa wataotaka kwenda Tanga kutoka Dar es Salaam na maeneo mengine.
"Nataka watu waamue wenyewe, kutumia barabara ipi kwa ajili ya kwenda Tanga," alisema Dk. Magufuli.
Alisema changamoto za maji na umeme, zitatatuliwa na serikali yake  kama alivyoahidi katika maeneo mengine.
Dk Magufuli alisema fedha za Shirika la Changamoto za Milenia (MCC), kiasi  cha sh. bilioni 992 zitatumika katika usambazaji umeme nchini. Alisema fedha hizo alizopewa Rais Jakaya Kikwete hivi karibuni, zitaongeza kasi ya usambazaji umeme maeneo ya vijijini.
Pia alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa awamu ya nne anayemaliza muda wake, Dk. Kikwete kwamba amefanya mambo makubwa kwa maendeleo ya taifa.
Alisema katika kipindi cha miaka 10 ya utawala wa Kikwete, yamepatikana mafanikio mengi ya kujivunia na kwamba akichaguliwa atayaendeleza yote yaliyoanzishwa na mtangulizi wake kwa manufaa ya Watanzania wote.
"Kwa kweli niwapongeze na ninyi wakazi wa Jimbo la Chalinze kwa kutoa Rais wa awamu ya nne. Rais Kikwete amefanya makubwa. Naamini  mkinichagua, nitayaendeleza mafanikio yake,” alisema.
Aliwataka wananchi wa jimbo la Chalinze, wamchague Ridhiwani Kikwete, awe mbunge wao kwa ajili ya maendeleo.
"Ridhiwani ni mtoto wa Rais, lakini hana majivuno.  Ni mtu wa kawaida, anapenda watu wa jimbo lake, nawaomba mumchague tena," alisema.
Dk. Magufuli alimruhusu Ridhiwani kuchukua majengo yaliyokuwa yakitumiwa na mkandarasi ili yaweze kutumika kwa ajili ya huduma za kijamii.
Akiwahutubia wakazi wa Bagamoyo katika uwanja wa Majengo, Dk. Magufuli alisema atahakikisha serikali yake itatumia uwezo wake kutatua tatizo la uhaba wa maji katika mji huo.
Alisema Bagamoyo ni mji wa kihistoria, hivyo lazima urejee katika umaarufu wake.
"Bagamoyo ni lango la Kihistoria enzi za watumwa. Nataka tatizo la maji liishe ili hata watalii wakizuru, wasikose maji," alisema.
Alisema anaamini Bagamoyo utakuwa mji wa aina yake barani Afrika katika sekta ya utalii.
"Bagamoyo itakuwa kitovu cha uchumi, nataka uwe mji wa mfano," alisema Dk. Magufuli.
Katika hatua nyingine, Dk. Magufuli alisema suala la wananchi wa zinga kuchelewa kulipwa fidia za EPZ, taratibu zinakamilishwa kwa majibu wa sheria.
Aliwataka wananchi wa Bagamoyo kumchagua Dk. Shukuru Kawambwa kuwa Mbunge wa jimbo hilo kwa ajili ya kuharakisha maendeleo.
Dk. Magufuli alisema serikali yake itaangalia uwezekano wa kupanua daraja la Wami kwa kuongeza njia zaidi, kwa lengo la kupunguza ajali.
Mpaka sasa, Dk. Magufuli ameshafanya mikutano ya kampeni katika mikoa 23 huku uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, ukitarajia kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.
AKONGA NYOYO SAME
Akiwa jimbo la Same Mashariki, Dk. John Magufuli aliwaahidi wananchi kukiboresha kiwanda cha Tangawizi kiweze kuongeza uzalishaji.
Pia serikali yake itaboresha skimu ya umwagiliaji ili wananchi waweze kufanya kilimo chenye tija.
Aidha licha ya ahadi hizo, Dk Magufuli alimwagiza Mkuu wa Polisi Wilaya ya Same, kuwasaka na kuwakamata waharibifu wa miundombinu mbalimbali, wanaofanya hivyo kwa makusudi ambao wanasemekana ni vijana wa vyama vya upinzani.
Katika mkutano huo, uliofanyika Ndungu wilayani humo, aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema Same, Kapongo Sonda, alikihama chama hicho na kujiunga CCM.
Alisema Chadema ya sasa imekuwa ya kupokea mafisadi tofauti na zamani wakati Dk. Wilbroad Slaa akiwa Katibu Mkuu.
Dk. Magufuli aliwataka wananchi wa Same kumchagua tena Anne Kilango Malecela kuwa mbunge.
"Hii barabara ya kuja jimboni kwenu, nitaiweka lami kwa heshima ya John Malecela, ambaye ana historia kubwa katika nchi hii," alisema.

No comments:

Post a Comment