SERIKALI imeahidi kuendelea kubana matumizi na kupambana na
uvujaji wa mapato kwa lengo la kuwapunguzia makali ya maisha wananchi na kwa
kuanzia, imepunguza makato ya mshahara wa mfanyakazi kutoka asilimia 11 hadi 9
katika mwaka wa fedha 2016/2017.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Rais John Magufuli, alipokuwa
akiwahutubia wafanyakazi katika kilele cha siku ya wafanyakazi duniani (Mei
Mosi), ambayo kitaifa ilifanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini hapa.
Alisema nia ya kupunguza kodi hiyo ni kuhakikisha wafanyakazi
wanapata nafuu katika kipato. Pia alisema watakaa na Shirikisho la Wafanyakazi
Tanzania (TUCTA) ili kuangalia namna watakavyoweza kuboresha mishahara ya
wafanyakazi kadri mapato yatakavyoongezeka.
Rais Magufuli alisema ingawa kutakuwa na upungufu wa mapato ndani
ya serikali, lakini ni vyema wafanyakazi wakapewa unafuu huo kwani hawana
sehemu ya kukwepa kulipa kodi.
’”Ni mategemeo yangu kuwa Bunge litapitisha kiwango hiki katika
bajeti ya serikali ijayo ili kutoa nafuu kwa wananchi na hasa wafanyakazi,’’alisema.
Alisema baada ya kupungua kodi hiyo, serikali inajipanga kuona ni
jinsi gani itaweza kuongeza kiasi cha mishahara kwa wafanyakazi kwani nia ni
kuhakikisha watumishi wanapata mishahahara inayolingana na kazi wanayofanya.
“Wafanyakazi hawana njia ya kukwepa kodi kwani wakipata tu misharaha
yao kodi imeshakatwa, hivyo ni muhimu kuwaangalia katika hili,” alisema.
Rais Magufuli alisema ni lazima kuangalia uwiano wa
mishahara miongoni mwa watumishi wa serikali.
Alisema hivi sasa kima cha juu kwa watumishi hakipaswi kuzidi sh.
milioni 15 na yeyote, ambaye hataki mshahara huo aache kazi.
Kwa mujibu wa Rais Magufuli, yapo baadhi ya mashirika ambayo watendaji
wake wamekuwa wakihonga bodi za na kujiwekea mishahara mikubwa huku watendaji
kazi wakipewa mishahara midogo.
“Nasikia kuna watu wanalalamika kuwa kima cha mishahara cha
sh. milioni 15 ni kidogo, waaache kazi hata leo. Haiwezekani mtu mmoja anapokea
shilingi milioni 30 huku mwingine anapokea shilingi 300,000, hii si sawa,”alisema.
Rais Magufuli alisema binafsi hawaonei wivu wanaopokea kiasi
kikubwa cha mishahara, lakini ni vyema wakawa na tofauti ndogo na wengine.
“Hata mimi nataka mshahara mkubwa, lakini ni vyema kuwa na
mshahara unaoendana na uzito wa kazi unayoifanya,” alisisitiza.
Aidha, Rais Magufuli alisema kumeundwa bodi mbili ambazo
zitashughulika na kupendekeza kima cha chini cha mishahara hapa nchini.
WAFANYAKAZI HEWA KUENDELEA KUSAKWA
Akizungumzia wafanyakazi hewa, Rais Magufuli alisema kumekuwa na
wafanyakazi hewa na kusisitiza kuwa atawasaka popote walipo.
Alisema hadi kufikia juzi, kulikuwa na wafanyakazi hewa zaidi ya 10.000 kote nchini na kati ya hao, 8,373 wanatokea TAMISEMI na wengine 1,922
wanatoka serikali kuu.
Rais Magufuli alisema watumishi hao hewa wamekuwa wakiigharaimu
serikali kiasi cha sh. bilioni 11.7, kila mwezi kulipa mishahara yao.
“Tanzania imechezewa sana na hawa watu ambao ni wafanyakazi hewa
na kuanzia sasa hakuna sababu ya kuwaonea huruma kwani wapo miongoni mwetu,‘’
alisema .
Rais alisema baadhi ya watumishi hao hewa wamekuwa wakishirikiana
na maofisa utumishi katika kuwezesha upatikanaji wa mishahara hiyo hewa.
KUHAMIA DODOMA
Rais aliwataka wanaoishauri
serikali kuhamia Dodoma, wawe wa kwanza kufanya hivyo badala ya kutoa kibanzi
machoni pa wengine huku boriti ikiwa machoni mwao.
Dk. Magufuli alisema nia ya kuhamia Dodoma iko pale pale ndio maana kila anapokuwa Dodoma, anakaa Ikulu ya Chamwino na hiyo ni moja ya jitihada na maandalizi ya kuhakikishia hilo linatimia.
Alisema hoja ya kuhamia Dodoma iliyotolewa na TUCTA ni ya msingi, lakini alipomuuliza rais wake makao makuu yao yako wapi, alimjibu kuwa yapo Dar es Salaam.
“Pamoja na TUCTA kuiomba
serikali ihamie Dodoma, wao bado wako Dar es Salaam, kazi hizi ndugu zangu ni
ngumu,” alisema.
HIFADHI YA JAMII
Rais Magufuli alisema serikali ya awamu ya tano inalenga kuhakikisha kwamba, wananchi wengi zaidi wanafaidika na mfumo wa hifadhi ya jamii nchini kuliko ilivyo hivi sasa.
Alifafanua kuwa, wanataka wananchi wengi zaidi wajiunge na mfuko wa bima ya afya ili wawe na uhakika wa matibabu.
Alisema wanaendelea na
juhudi za kupanua wigo wa mfuko wa bima ya afya vijijini na kuwezesha
wafanyakazi wengi wa sekta binafsi kujiunga na mfuko huo.
Rais Magufuli alisema mifuko ya hifadhi ya jamii imeanza kusajili wafanyakazi kutoka sekta zisizo rasmi, lengo likiwa kuhakikisha wananchi wengi wanapata huduma za msingi.
Alisema serikali imeielekeza mifuko ya hifadhi ya jamii kuacha kuwekeza kwenye miradi isiyo na tija na miradi ya ajabu ajabu, kama ujenzi wa madaraja.
Alisema ameitaka mifuko hiyo kuwekeza kwenye viwanda, ambapo Watanzania watapata ajira, lakini pia watapata wanachama wengi zaidi kuliko hivi sasa na kuboreka zaidi.
WAAJIRI WANAOKIUKA SHERIA ZA
KAZI
Rais Magufuli pia alisema serikali itaweka utaratibu wa adhabu za papo kwa papo kwa waajiri wanaokiuka sheria za kazi, kila watakapofanya hivyo.
Alisema wamepokea ushauri wa
TUCTA wa kupunguza idadi ya mifuko ya pensheni nchini na matumizi yasiyo
ya lazima.
Aliwahakikishia kuwa kazi ya
kurekebisha mifuko ya hifadhi nchini wataikamilisha ndani ya mwaka 2016/17,
kwani inahitaji umakini mkubwa na kuwataka kutambua kwamba suala la kuwaruhusu
watumishi kujiunga na vyama vya wafanyakazi si la hiari bali ni la lazima na
haipaswi kuwachagulia mfuko wa kujiunga.
Dk. Magufuli alionya watumishi kutotumia mwanya huo wa kujiunga na vyama vya wafanyakazi, kuchochea migogoro ya kikazi, uzembe na uvivu kazini. Pia alitaka visitumike kama vyama vya kisiasa, bali vitumike kuimarisha uhusiano kati ya waajiri na waajiriwa.
Aliizitaka wizara zote kufuatilia ajira kwa wageni na kuhakikisha hawafanyi kazi ambazo zinaweza kufanywa na wazawa, kwa kuwa wageni wengi wanafanya kazi hata za kuchoma chips.
Rais aliiagiza wizara husika kuwafichua wageni ambao wanafanya kazi bila kuwa na vibali vya kufanyia kazi hapa nchini.
Katika salaam za Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana, alitilia mkazo suala la serikali kuhamia Dodoma na kupongeza hatua ya Rais Dk, Magufuli kutumia kati ya siku zake 100, tangu alipoingia madarakani kukaa muda mrefu na kufanyia shughuli zake akiwa Dodoma.
Alisema hali hiyo inadhihirisha dhamira ya dhati ya serikali ya awamu ya tano kuendeleza juhudi zilizofanywa kuanzia serikali ya awamu ya nne za kuhamia Dodoma na wao kuzikamilisha.
No comments:
Post a Comment