Wednesday 20 July 2016

KINANA ASEMA ANANG'ATUKA CCM



KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, amesema anatarajia kustaafu wadhifa huo baada ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa mwenyekiti mpya wa CCM.

Kinana amesema uamuzi wake huo ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa mwaka 2012 ya kutogombea nafasi yoyote ya juu ya uongozi ndani ya Chama, baada ya kukitumia kwa miaka 25.

Amesema hakuweza kuitekeleza ahadi yake hiyo mwaka huo, kutokana na viongozi wastaafu kumuomba  na kumsihi aendelee kukitumikia Chama katika wadhifa wa katibu mkuu hadi baada ya uchaguzi mkuu.

"Kutokana na mazingira ya wakati ule, wazee wa Chama wastaafu na mwenyekiti wa CCM (Jakaya Kikwete), waliniomba niendelee kukitumikia katika wadhifa wa katibu mkuu. Sikuona sababu ya kuwakatalia. Nikakubali kubeba dhamana ya kukitumia Chama,"amesema.

"Nadhani wakati sasa umefika wa mimi kung'atuka na kuwapa nafasi wengine waweze kukisaidia Chama katika nafasi za juu. Uchaguzi ukimalizika nitapumzika. Mwanasiasa ni lazima ujue wakati wa kuingia kwenye uongozi na kutoka,"amesisitiza.

Kinana alielezea msimamo wake huo jana, alipozungumza na Uhuru, kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu Chama na serikali, ofisini kwake mjini hapa.

Amesema wapo wanachama wengi, wakiwemo vijana na wenye rika la kati, wenye sifa na uwezo wa kukiongoza Chama katika ngazi mbalimbali, kutokana na kulelewa vizuri na pia kuwa na mapenzi makubwa na Chama.

"Sio vizuri kuendelea tu na uongozi. Mwalimu (Nyerere) aling'atuka na mimi nang'atuka,"amesema Kinana.

Ameongeza kuwa mara baada ya mwenyekiti mpya wa CCM kuchaguliwa katika mkutano mkuu maalumu, unaotarajiwa kufanyika Jumamosi wiki hii mjini Dodoma, ataandika barua ya kujiuzulu nafasi hiyo ili kumpa nafasi ya kuteua sekretarieti mpya.

Kinana amesema katika miaka mitatu aliyokitumikia Chama akiwa katibu mkuu, amekumbana na changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na kukikuta kikiwa hakina mshikamano baina ya viongozi na wanachama na pia kuwepo kwa uhasama miongoni mwao.

Amesema baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo, alijipa kazi ya kukiimarisha na kukipeleka kwa wananchi ili kiwe kimbilio lao na pia kukisemea na kukifanya kiwe na uwezo na nguvu ya kuisimamiia serikali katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi.

Amezitaja kazi zingine alizozifanya katika kukiimarisha na kurejesha uhai wa Chama kuwa ni pamoja na kupunguza uhasama na kuimarisha umoja miongoni mwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM na Kamati Kuu ya CCM.

"Wanachama walikuwa wakilalamika sana kwa nini viongozi wenyewe kwa wenyewe hawaelewani na kama mnavyojua, kichwa kikiyumba katika mwili na chini nako kunayumba. Hivyo hiyo ndio kazi kubwa niliyoanza kuifanya katika kukifufua na kukiimarisha Chama,"amesema Kinana.

Aidha, Kinana amesema Chama kilikuwa mbali na wananchi, hasa wa maeneo ya vijijini, hivyo ilibidi wakirudishe kwao kwa kufanya ziara mikoa, wilaya na majimbo yote ya uchaguzi hapa nchini. Amesema ziara yake hiyo pia ilimwezesha kufika katika nusu ya kata zote nchini.

"Kwa muda wa miaka mitatu, nimesafiri umbali wa kilometa laki moja na tisini alfu, nilifanya zaidi ya mikutano 3,700, hakuna sehemu ambayo sijafika.

"Nimekutana na wananchi, nimejua kero zao, niliwapa nafasi ya kuuliza maswali, nikachukua hoja zao na kuzipeleka serikalini. Nilikutana na rais, waziri mkuu na  mawaziri ili kuzitatua. Nilikuwa kiungo kati ya wananchi na serikali kwa kuwasikiliza na kuwasemea,"amesema.

Ameyataja baadhi ya mafanikio aliyoyapata wakati wa uongozi wake kuwa ni pamoja na kukiwezesha Chama kupata mgombea urais, wabunge na udiwani katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana na kupata ushindi wa kishindo.

No comments:

Post a Comment