Wednesday 20 July 2016

WANAFUNZI 382 WA UALIMU WAREJESHWA UDOM



NA EMMANUEL MOHAMED
 
HATIMA ya wanafunzi 7,805 waliorejeshwa nyumbani ambao walikuwa wanasoma Stashahada Maalum ya Ualimu wa Sayansi na Hisabati Chuo Kikuu Dodoma(UDOM), imetimia, baada ya serikali kuwarudisha 382 kumalizia mafunzo hayo.

Aidha, wanafunzi 290 kati yao, hawakuwa na sifa za kujiunga na masomo hayo maalum na wanafunzi 6,305 wamehamishiwa kwenye vyuo vikuu vya ualimu, ambapo 4,586 wa mwaka wa kwanza wa mafunzo hayo ya ngazi ya sekondari wamehamishwa vyuo vya ualimu vya Morogoro, Butimba, Mpwapwa, Songea na Tukuyu ili kuendelea na masomo yao.

Akizungumza jana mjini Dar es Saalam,Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia,Profesa Jocye Ndalichako, alisema wanafunzi 1,337 wa mwaka wa pili katika ngazi hiyo ya sekondari watahamishiwa Chuo cha Ualimu cha Korogwe na Kasulu kumalizia masomo hayo na kwamba masomo hayo maalum yamesitishwa.

Mbali na uamuzi huo, serikali imesitisha utoaji wa mikopo kwaya vitendo kutokana na kuwepo kwa dalili za wanafunzi hewa wa uombaji wa mkopo huo hadi watakapojiridhisha na uhakiki.

Profesa Ndalichako alisema kuna baadhi ya vyuo hivyo vimewasilisha orodha ya wanafunzi ambao majina mengine ni wanafunzi waliokwishakufa miaka iliyopita, wengine wamefukuzwa na wengine wameacha masomo na kwamba utoaji huo umesitishwa.

Alisema Mei 28,mwaka huu, serikali iliwarejesha wanafunzi 7,805 kutoka UDOM ambao walikuwa wanachukua stashahada maalum ya ualimu wa sayansi na hisabati kutokana mgomo wa walimu uliodumu kwa wiki tatu.

“Wanafunzi waliosimamishwa masomo walikuwa wamegawanyika katika makundi makuu mawili, ambapo kundi la kwanza lilikuwa ni wanafunzi 6,595 waliodahiliwa katika stashahada maalum ya ualimu wa elimu ya sekondari na lingine ni la wanafunzi 1,210 walidahiliwa mafunzo ya stashahada ya elimu ya msingi,”alisema.

Ndalichako alifafanua kuwa baada ya serikali kuchukua hatua ya kuwaondoa wanafunzi wa chuo hicho, ilifanya uchambuzi wa wanafunzi hao kwa lengo la kujiridhisha na sifa zao, ambapo walipaswa kwa na ufaulu wa daraja la kwanza hadi la tatu na alama mbili au zaidi ya ufaulu wa masomo ya sayansi na hisabati.

“Katika kundi la stashahada maalum ya ualimu wa elimu ya sekondari, uchambuzi umebaini wanafunzi wenye ufaulu wa daraja la kwanza na la pili ambao wamefaulu masomo mawili ya sayansi kwa kiwango cha alama C na A ni 382, ambapo mwaka wa kwanza waliopata daraja la kwanza 134 na mwaka wa pili ni 248 ambapo wanafunzi hao tu ndio watakarudishwa chuoni hapo,”alisema Ndalichako.

Alisema mchanganuo wa uchambuzi unaonyesha kulikuwa na wanafunzi 52 waliopata daraja la nne kinyume na matakwa ya programu hiyo, ambapo wanafunzi walitakiwa wawe na ufaulu wa daraja la kwanza hadi la tatu na kwamba uchambuzi huo umefanyika zaidi kwa wanafunzi wenye ufaulu katika masomo mawili kwa kiwango cha alama A hadi C.

Profesa Ndalichako alidai wanafunzi 6,595 walidahiliwa kusoma masomo ya stashahada maalum ya ualimu wa elimu ya sekondari kwa masomo ya hisabati na sayansi, kati yao 6305 walikuwa na sifa stahiki ambazo ni ufaulu kwa daraja la kwanza hadi la tatu kwa kiwango cha gredi C na A katika masomo mawili ya sayansi.

“Uchambuzi unaonyesha wanafunzi 4,720 walikuwa mwaka wa kwanza, waliofanikiwa katika ufaulu huo ni wale wa daraja la kwanza ambao ni wanane na waliopata daraja la pili ni 126, huku waliopata daraja la tatu 4,586, wanafunzi 1,585 wa mwaka wa pili waliopata kufanikiwa kuwa na sifa za ufaulu ni wale wa daraja la kwanza ambao walikuwa 29, wa daraja la pili 219 na wa daraja la tatu 1,337 hao ndio waliokuwa na sifa za kufanikiwa kusoma masomo hayo maalum,”alisema.

Alisema kwa upande wa wanafunzi ambao hawakuwa na sifa za kudahiliwa katika masomo hayo maalum ya ualimu wa shule za sekondari ni 290, huku uchambuzi ukionyesha kuwa waliopata daraja la kwanza hakuna hata mmoja,waliopata daraja la pili ni tisa na daraja la tatu 260 na daraja la nne ni 21 na kwamba hao ndio hawakuwa na sifa stahiki, hivyo serikali imewaruhusu kuomba mafunzo yanayolingana na sifa.

Aliongeza kuwa uchambuzi wa sifa hizo ulifanyika pia kwa wanafunzi 1,210 waliokuwa wamedahiliwa katika stashahada ya ualimu wa elimu ya msingi na kubaini kuwa wanafunzi 29 wa mwaka wa pili walikuwa ni walimu wa shule za msingi ambao walikuwa wamehitimu kidato cha nne na kuhudhuria mafunzo ya ualimu wa cheti ambao walikuwa na uzoefu kazini kwa miaka miwili au zaidi.

“Wanafunzi hao 29 wa mwaka wa kwanza hakukuwa na aliyepata daraja la kwanza na daraja la pili, lakini kwa upande wa daraja la tatu ni mmoja na daraja la nne ni wanne na kwa wanafunzi wa mwaka wa pili aliyepata daraja la kwanza ni mmoja, daraja la pili ni wawili, daraja la tatu ni saba na kwa daraja la nne ni 14, hivyo wanafunzi hao watahamishiwa katika Chuo cha Ualimu Kasulu wamalizie masomo kwa gharama zao,”alisema Ndalichako.

Alifafanua kuwa wanafunzi 1,181 ambao walikuwa wahitimu wa kidato cha nne, waliokuwa mwaka wa kwanza hakuna aliyepata daraja la kwanza, huku waliopata daraja la pili ni wanne, waliopata daraja la tatu ni 1,011 na daraja la nne hakuna na kwa upande wa mwaka wa pili hakuna aliyepata daraja la kwanza, daraja la pili ni wawili, daraja la tatu ni 151 na daraja la nne ni 13 na kwamba wanafunzi hao waombe mafunzo yanayolingana na sifa walizonazo mahali wanapotaka wao.

Aidha, alisema serikali itaendelea kuwapatia mikopo wanafunzi watakaorejeshwa UDOM na wanafunzi ambao watakahamishwa kwenye vyuo vya ualimu vya serikali watapewa mkopo wa sh.600,000 kwa mwaka ambayo ni ada ya mafunzo ya ualimu itakayolipwa moja kwa moja chuoni.

Profesa Ndalichako alisema wanafunzi wanaorejeshwa UDOM wataanza masomo Oktoba, mwaka huu,huku wanafunzi watakaohamia katika vyuo vya ualimu wataendelea na mafunzo yao Septemba mwaka huu na kwamba wanafunzi hao watatakiwa kuripoti wakiwa na vyeti vyao halisi vya kidato cha nne ambavyo vitahakikiwa kabla hawajapokelewa rasmi kwenye vyuo walivyopangiwa.

Profesa Ndalichako alisema kwa wale wanafunzi ambao wamehitimu kidato cha nne na kuhudhuria mafunzo ya ualimu wa cheti (Daraja la tatu A)ambao wenye uzoefu kazini miaka miwili na zaidi watawekewa masharti ya mkataba wa kulipa mkopo huo kabla ya kumaliza utumishi wao kwa kipindi kifupi kwa amana ya kutazama upya umri wa muombaji.

Ndalichako alitoboa siri ya kusimamisha udahili kwa Chuo cha Mtakatifu Joseph kuwa ni kutokana na kuwa walimu hawana sifa zinazotakiwa ikiwemo PHD huku uwiano wa sifa hizo hazifanani na chuo chenyewe.

Pia, alisema mitaala ya chuo hicho imekuwa haiendani na mazingira halisi na wanafunzi hao hawana uhuru na serikali ya chuo na kwamba adhabu za chuo hicho haiendani na sheria za chuo.

“Yaani chuo hicho kimefanyiwa ukaguzi na timu tano na mezani kwangu kuna ripoti tano ambazo zinaonyesha wanafunzi hawana uhuru wa kuanzisha serikali yao ya kuzungumzia maslahi yao na tumewaambia kuanza kufanya marekebisho, lakini hakuna utekelezaji, hivyo tumesitisha hadi watakaporekebisha kwa mfano vifaa havitoshelezi na miundombinu,”

Alisema kwa sasa chuo hicho hakitachukua wanafunzi hadi watakaporekebisha mapungufu yao yaliyoelekezwa katika timu hizo ndipo wataanza kudahili hivyo kwa mwaka 2016/2017 haitafanya udahili wa wanafunzi.

No comments:

Post a Comment