Thursday, 25 August 2016

MBOWE KUFILISIWA? ANADAIWA BIL. 1.150 ZA KODI YA PANGO NA NHC



MALI za Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, ziko hatarini kukamatwa iwapo atashindwa kulipa deni la sh. bilioni 1.150 anazodaiwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Mbowe ambaye ametajwa kuwa miongoni mwa wadaiwa sugu wa NHC na anatakiwa kulipa deni la pango la nyumba ya umma iliyopo Club Bilicanas, Dar es Salaam.

Awali, Mbowe alikuwa na ubia na NHC kuhusu nyumba hiyo, lakini hivi sasa ubia huo umevunjwa, hivyo itabaki kuwa ya umma na kama atashindwa kulilipa deni lake ndani ya mwezi huu, atachukuliwa hatua za kisheria, ikiwa ni pamoja na mali zake kukamatwa.

Mbali na Mbowe, wadaiwa wengine sugu wa NHC ni Wizara ya Uchukuzi ambayo inadaiwa sh. bilioni 2.7, Wizara ya Afya, sh. bilioni 1.3, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, sh. bilioni 1.1, Tume ya Utumishi wa Umma, sh. milioni 109.9 na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa sh. milioni 631.8.

Wengine wanaodaiwa na shirika hilo ni Benki ya Azania sh. milioni 161.9, A. D. Investment Limited sh. milioni 155.4, Palace Hotel LTD sh. milioni 128.1.

Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu, alisema hayo jana mjini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumzia namna shirika hilo litakavyosaidia upatikanaji wa nyumba za watumishi wa serikali wanaohamia Dodoma.

Alisema shirika hilo linaunga mkono wazo la serikali la kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM inayoelekeza serikali kuhamishia shughuli zake Dodoma na kwamba wamepanga kuufanya mji huo kuwa wa kisasa na wenye fursa nyingi.

Mchechu alisema shirika hilo linadai sh. bilioni 15 kutoka kwa taasisi za serikali na sekta binafsi na kwamba wako kwenye mikakati ya kudai madeni hayo, ikiwa ni pamoja na kutoa notisi kwa wote wanaodaiwa.

Alisema miongoni mwa waliopewa notisi za kulipa madeni yao haraka ni Mbowe Hotels LTD, ambaye anadaiwa sh. bilioni 1.150.

Mchechu alisema notisi ya Mbowe itamalizika mwezi huu na kwamba asipolipa deni hilo, atachukuliwa hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kunyang’anywa jengo hilo la umma.

“Pale Bilicanas mwanzo tulikuwa na ubia, lakini tumeuvunja na sasa NHC tutaendeleza wenyewe eneo hilo, hivyo kama Mbowe hatalipa basi sheria zitachukuliwa,” alisema.

Aliongeza kuwa: “Kama atalipa ataachwa aendelee kuwa mpangaji na deni hilo anatakiwa kulipa lote kwa mkupuo na si kidogo kidogo.”

Mchechu aliwataka wadaiwa wote, zikiwemo taasisi za serikali, kulipa madeni yao ndani ya mwezi mmoja kuanzia leo ili kuepuka adha ya kuondolewa katika nyumba wanazopanga.

Aidha aliwataka waliopewa notisi za kulipa kodi, walipe kodi zao ndani ya muda wa notisi walizopewa na watakaoshindwa watatolewa kwenye nyumba na kuchukuliwa hatua nyingine za kisheria ikiwa ni pamoja na kukamata mali zao.

KUHAMIA DODOMA

Mchechu alisema shirika linaunga mkono uamuzi wa serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Magufuli wenye lengo la kuharakisha maendeleo ya nchi kwa sababu utatoa fursa mbalimbali.

Alizitaja fursa hizo kuwa ni pamoja na ujenzi wa nyumba katika Mji wa Dodoma kwa ajili ya watumishi wa serikali watakaohamia mkoani humo.

Alisema fursa nyingine ni kuliongezea shirika soko la nyumba inazojenga kwa ajili ya kuwauzia wananchi na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi kupitia sekta ya ujenzi wa nyumba.

Mchechu alisema fursa nyingine ni kuongeza ajira kutokana na shughuli za ujenzi wa nyumba zitakazofanyika Dodoma.

Alisema tayari shirika hilo limejenga nyumba za makazi 153 eneo la Medeli, Dodoma kwa ajili ya kuuza na kwa sasa nyumba 97 zinaendelea kuuzwa kwa wananchi.

“Nyumba hizi kwa sasa zimepangishwa kwa wananchi na kipaumbele kitapewa kwa wapangaji waliopo ndani na wakishindwa zitauzwa kwa Watanzania wengine,” alisema.

Alisema wamejenga nyumba 44 za gharama nafuu katika Wilaya ya Kongwa, nje kidogo ya mji mkuu wa Dodoma na zitauzwa kwa wananchi.

Mkurugenzi Mkuu huyo alisema shirika limenunua ekari 236 za ardhi katika eneo la Lyumba, karibu na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na kwamba katika eneo hilo wanawakaribisha wawekezaji wengine.

Alisema kutokana na akiba ya ardhi, shirika linajiandaa kuanza ujenzi wa nyumba 300 hadi 500 ndani ya miezi 12 kwa ajili ya kusaidia makazi ya watumishi wa serikali.

Mchechu alisema ili kutekeleza kwa haraka ujenzi wa watumishi mjini Dodoma, shirika hilo linatarajia kuwa na sh. bilioni 60 zitakazopatikana kutoka katika vyanzo mbalimbali vya fedha.

Alisema uamuzi wa serikali wa kuhamishia makao makuu Dodoma, unalenga kulifanya jiji la Dar es Salaam kuwa kitovu kikuu cha shughuli za biashara.

“Mpango kabambe wa Dar es Salaam mpya unaandaliwa na serikali na utakuwa tayari Oktoba mwaka huu,”alisema na kuongeza kuwa kwa vyovyote mpango huo unalenga kuifanya Dar es Salaam iweze kubeba shughuli nyingi za kiuchumi na kibiashara.

Alisema shirika limejipanga kuendelea na ujenzi wa nyumba bora za kuuza na majengo makubwa kwa ajili ya wafanyabiashara katika jiji la Dar es Salaam kwani litaendelea kubaki kitovu cha biashara.

No comments:

Post a Comment