Thursday 4 August 2016

WENYE MIFUGO MINGI KUHAMISHIWA RANCHI




WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewataka wafugaji wenye mifugo mingi nchini, kujiweka tayari kwa ajili ya kuhamia kwenye maeneo yatakayotengwa na serikali katika ranchi ili waweze kufuga kisasa.
Pia, aliwataka wafugaji hao kushirikiana na serikali katika kuboresha miundombinu ya maeneo hayo, ikiwemo ujenzi wa visima vya maji na majosho ili ufugaji wao uwe na tija.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana, alipotembelea kiwanda cha kusindika nyama cha Nguru Hills Ranch, kilichoko wilayani Movomero.
Majaliwa alisema kitendo cha wafugaji hao kuhamia katika ranchi, kitawezesha mifugo yao kuwa na ubora kwa sababu aina ya ufugaji wa sasa ya kutembeza mifugo umbali mrefu, inasababisha ufugaji wao kuwa na tija ndogo.
Akizungumzia kuhusu uwepo wa kiwanda cha kuchakata nyama wilayani Mvomero, Waziri Mkuu Majaliwa alisema kitamaliza mgogoro wa muda mrefu kati ya wakulima na wafugaji kwa kuwa wafugaji watapata fursa ya kuuza mifugo yao kiwandani hapo.
“Uwepo wa viwanda katika maeneo yetu utatuwezesha kupunguza matatizo tuliyonayo katika maeneo yetu, ikiwemo suala la migogoro kati ya wafugaji na wakulima. Viwanda ndiyo vitakavyotuondoa kutoka katika uchumi wa chini hadi wa kati,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi na Mshauri wa Kiwanda cha Nguru Hills Ranch, Dunstan Mrutu, alisema kiwanda hicho chenye uwezo wa kuchinja ng’ombe 300, mbuzi na kondoo 1,500, kwa siku kinatarajiwa kufunguliwa  Desemba, mwaka huu.
Mrutu alisema takriban asilimia 80, ya nyama itafungashwa na kuuzwa nje ya nchi, hasa Uarabuni, kwa sababu nyama ya mbuzi ya Tanzania imebainika kuwa na mvuto maalumu katika nchi hizo.
“Mbali na uwekezaji huu wa kiwanda cha nyama, pia tunatazamia kuwekeza katika mnyororo wa thamani kuanzia kusindika ngozi inayotoka kiwandani hadi kuzalisha viatu, mikanda na bidhaa zote za ngozi na kupunguza uagizaji wa bidhaa hizo kutoka nje ya nchi,” alisema.
Mrutu alisema nia yao ni kuitikia wito wa Rais Dk. John Magufuli wa kutaka viwanda vizalishe viatu nchini, kuanzia vya majeshi na wananchi wote, ambapo wamepanga kuanzia mwakani wataanza kuuza bidhaa hizo.
Aliongeza kuwa, uwepo wa kiwanda hicho utatoa fursa kwa wafugaji na wakulima kuuza majani, mifugo na mazao ya chakula kama mtama, mahindi, ambapo tayari wameanza kuhamasisha jamii za wafugaji na wakulima wa Mvomero, Ngerengere na sehemu zinazozunguka eneo la kiwanda, kuchangamkia fursa hiyo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa wilaya ya Mvomero kufanya mapitio ya mashamba ili kujua wamiliki wake na kama hawajayaendeleza, wachukue uamuzi wa haraka wa kuyatwaa na kuyarudisha mikononi mwa serikali.
Waziri Mkuu Majaliwa alitoa agizo hilo wakati akijibu ujumbe uliokuwa katika mabango yaliyobebwa na wananchi wa Kijiji cha Maji ya Chumvi, wilayani Mvomero, waliosimamisha msafara wakati ukitokea kwenye kiwanda cha nyama.
Wakati huo huo, Majaliwa juzi, alikataa kupokea msaada wa madawati uliotolewa na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), baada ya kubaini yametengenezwa chini ya kiwango.
“Ofisa Elimu njoo kagua haya madawati, yaliyo mazuri nitayapokea na yaliyobaki yarudishwe karakana yakatengenezwe upya, huu si wakati wa kupokea vitu vibovu,“ alisema.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo alipowasili katika Kiwanja cha Mabau, Mtibwa kwa ajili ya kuzungumza na wananchi, ambapo alikabidhiwa madawati hayo na Meneja wa TFS.
Alisema anatambua dhamira ya TFS ya kuunga mkono jitihada za serikali za kumaliza tatizo la upungufu wa madawati, lakini hawezi kupokea madawati yaliyotengenezwa chini ya kiwango.
Baada ya Ofisa Elimu (Msingi) wa Wilaya ya Mvomero, Michael Ligola kukagua madawati 102 yaliyoletwa uwanjani hapo, madawati 84, yalibainika kuwa ni mabovu na 14,  ndiyo yalikuwa mazima.
Waziri Mkuu alisema hawezi kupokea madawati hayo yaliyotolewa na Meneja wa Msitu wa Mtibwa, Hamza Kateti na kuuagiza uongozi wa wilaya ufuatilie suala hilo kwa kuwa walitakiwa kuyakagua kabla ya yeye kukabidhiwa.
Katika hatua nyingine, aliwasisitiza wazazi na walezi wa wilaya hiyo kuhakikisha wanawapeleka watoto wao shule na atakayeshindwa atachukuliwa hatua kali za kisheria.

No comments:

Post a Comment