Sunday, 6 November 2016

MBOWE ACHAFUA HALI YA HEWA BUNGENI

NAIBU Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Tulia Ackson, amemtaka Kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, ambaye pia ni mbunge wa Hai (CHADEMA), Freeman Mbowe, kupeleka mahakamani tuhuma za rushwa zinazowahusisha baadhi ya wabunge.

Dk. Tulia alimtaka Mbowe afanye hivyo, baada ya kutoa tuhuma dhidi ya baadhi ya wabunge kupewa rushwa, wakati wa kipindi cha maswali ya papo hapo kwa Waziri Mkuu.

Naibu Spika alitumia mamlaka yake kwa kumtaka Mbowe, kuuliza maswali kwa Waziri Mkuu, ambayo ni ya kisera kama kanuni za kudumu za bunge zinavyotaka.

Aidha, Dk. Tulia alisisitiza kuwa ataendelea kusimamia kanuni hizo wakati akiongoza kikao cha bunge na atalifanya hilo kwa wabunge wote bila kujali wadhifa wa mbunge ndani ya bunge.

Katika swali lake Mbowe, Mbowe alidai kuwa wabunge na mawaziri ni viongozi wa umma kwa mujibu wa sheria ya maadili ya viongozi wa umma namba 13 ya mwaka 1995, lakini kuna taarifa kwamba,
Jumanne ya Oktoba 25, mwaka huu, saa mbili usiku, kiliitishwa kikao cha wabunge wa CCM, Waziri Mkuu akiwa mwenyekiti na
kuhudhuriwa na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana.

Mbowe alikwenda mbali zaidi kwa kudai kuwa katika kikao hicho, wabunge na mawaziri hao walipewa zawadi ya pesa ili wapitishe Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2017/18 na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2017/18, uliowasilishwa bungeni Jumanne iliyopita.

Baada ya Mbowe kuuliza swali hilo, Dk. Tulia alisema kuwa maswali kwa waziri mkuu ni yanapaswa kuwa anayohusu sera na kuwakumbusha wabunge kuzingatia hilo.
“Mheshimiwa Mbowe naomba swali lako liwe linahusu sera,”alisema Naibu Spika.

Baada ya kauli hiyo ya Naibu Spika, Mbowe alisema masuala ya rushwa na masuala ya maadili ya viongozi ni sehemu ya sera hivyo alisisitiza kuwa ni muhimu swali hilo lijibiwe na Waziri Mkuu.

Hata hivyo, Dk. Tulia aliendelea kusisitiza kuwa atamruhusu Waziri Mkuu kujibu maswali yanayohusu sera, kama ambavyo atamzuia mbunge mwingine yeyote.

“Mheshimiwa Mbowe, nadhani kwa hapa sasa tulipofika kama wewe unaona hili swali ni la sera, kanuni ndizo zinaniongoza mimi kwa maana hiyo nitaendelea na maswali mengine,"alisema Dk. Tulia na kumpa nafasi mbunge mwingine kuuliza swali.

MIONGOZO
Baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu, baadhi ya wabunge waliomba miongozo kwa Naibu Spika kuhusu tuhuma zilizotolewa na Mbowe.

Mbunge wa Chemba (CCM), Juma Nkamia alitaka kujua kama Mbowe anaweza kuthibitisha ndani ya bunge kwamba ni kweli wabunge wa CCM walipewa fedha na kama hawezi kuthibitisha, ni hatua gani atachukuliwa na bunge.

Akijibu muongozo huo, Naibu Spika alisema hawezi kumwambia Mbowe athibitishe madai yake hayo ya rushwa kwa wabunge, kwa sababu suala hilo alilizuia kutolewa majibu na Waziri Mkuu.

Alisisitiza kuwa kama Mbowe anao ushahidi kuhusu madai hayo, upelekwe sehemu husika na baada ya chombo hicho kufanya kazi, ikithibitishwa watachukua hatua kwa sababu watakuwa wamevunja sheria.

Dk. Tulia alisema sababu za kumzuia Waziri Mkuu kujibu swali hilo ni kutokana na swali hilo kuongelea mambo ya rushwa, ambapo kwa mujibu wa sheria, vipo vyombo maalumu vya kushughulikia suala hilo, siyo bunge.

Alisema bunge haliwezi kujiweka mahali ambapo linaweza kuanza kusikiliza tuhuma au kesi za rushwa na kushauri kama zipo kesi za rushwa, zipelekwe katika vyombo husika.

No comments:

Post a Comment