Sunday 6 November 2016

WAPAKISTAN WATOZWA FAINI MIL 126/-



NA FURAHA OMARY

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewahukumu raia watatu wa Pakistan, kulipa faini ya jumla ya sh. milioni 126, kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), baada ya kukiri kosa la kuingiza nchini vifaa vya mawasiliano na kuendesha biashara hiyo bila leseni.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage, baada ya washitakiwa hao, Hafees Irfan, Mirza Irfan  Baig na Mirza Rizwani Baig, kukiri mashitaka yanayowakabili na kukubali maelezo ya awali.

Hakimu Mwijage alisema kutokana na washitakiwa kukubali makosa kama walivyoshitakiwa na kukubali maelezo ya awali, mahakama inawaona wana hatia.

Kabla ya kutolewa kwa adhabu, Wakili wa Serikali Mkuu, Johannes Kalungura, akishirikiana na Wakili wa Serikali, Ester Martin, walidai washitakiwa ni wakosaji wa mara ya kwanza.

Hata hivyo, waliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa kuwa makosa kama hayo yanahatarisha usalama wa nchi na  yanaisababishia hasara.

Pia, walidai nchi ipo katika wimbi, ambalo makosa kama hayo yanajirudia na serikali ipo katika mkakati wa kuyakomesha, ikiwezekana yasiendelee tena.

Kwa upande wa mawakili wa upande wa utetezi, Mohammed Majaliwa na Samwel Shadrack, walidai washitakiwa ni wakosaji wa mara ya kwanza wa kosa la kuendesha shughuli za mawasiliano bila ya leseni, hivyo wanastahili kupewa adhabu kulingana na kosa hilo.

Aidha, walidai washitakiwa hao wana watoto na wazazi wanaowategemea na wamekaa gerezani kwa takriban miezi 13, ambayo ni adhabu tosha kwa makosa waliyofanya.

Baada ya kusikiliza maelezo hayo ya utetezi, Hakimu Mwijage alitoa adhabu, ambapo alisema mahakama imezingatia maelezo ya pande zote mbili, hivyo inawaadhibu washitakiwa katika shitaka la kwanza kwa pamoja kama walivyoshitakiwa, kulipa faini ya sh. milioni tano na wakishindwa watakwenda jela mwaka mmoja.

Katika mashitaka ya pili, tatu na nne,  Hakimu alisema washitakiwa hao kwa pamoja katika kila shitaka, watalipa faini ya sh. milioni tano na wakishindwa watatumikia adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja jela.

Aidha, aliamuru kwamba kila mshitakiwa atalipa sh. milioni 35, kama hasara waliyoisababishia nchi, hususan mamlaka husika (TCRA).

Awali, upande wa jamhuri uliwakumbusha washitakiwa hao mashitaka manne yanayowakabili, ambayo walikiri kuyatenda.

Akiwasomea maelezo ya awali, ambayo washitakiwa waliyakubali, Ester alidai washitakiwa ni raia wa Pakista, ambao wana uhusiano wa karibu na kwamba, tarehe isiyofahamika wakiwa Pakistan na watu wengine, walikubaliana kutenda kosa Tanzania.

Washitakiwa hao walikubali kwamba kutokana na makubaliano hayo, walitafuta na kununua vifaa, ambavyo watavisimika kwa ajili ya mawasiliano ya kimataifa bila ya kutumia njia halali ya TCRA.

Pia, walikubali ili kufikia malengo yao, waliamua kusafiri kwenda nchi mbalimbali, ikiwemo Tanzania na waliingia tarehe tofauti na kwenda kuishi katika Hoteli ya Butterfly, iliyoko Kariakoo, wilayani Ilala, Dar es Salaam.

Washitakiwa hao walikubali katika hoteli hiyo walikuwa wakiishi katika chumba kimoja, chenye namba 905, ambako walianza kuendesha shughuli hizo za mawasiliano bila ya kuwa na leseni ya TCRA.

Ilielezwa mahakamani hapo kwamba, TCRA ilibaini juu ya hilo, hivyo walitoa taarifa kwa maofisa wa polisi, ambapo walianza uchunguzi wa pamoja.

Oktoba 5, mwaka jana, maofisa wa olisi na wa TCRA, wakati wakiendelea na uchunguzi wao, walienda katika hoteli hiyo kwenye chumba cha washitakiwa na kuwakuta na vifaa mbalimbali vya mawasiliano.

Washitakiwa hao walikiri kukutwa na vifaa hivyo, vikiwemo kadi za  simu za Airtel, kompyuta mpakato na kwamba, waliisababishia TCRA hasara ya sh. 140, 049,000.

No comments:

Post a Comment