Sunday 6 November 2016

MAHAKAMA YAAMURU TUNDU LISSU AKAMATWE, LEMA ATIWA MBARONI DODOMA, AREJESHWA ARUSHA KUHOJIWA



MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imetoa hati ya kukamatwa kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA), anayekabiliwa na kesi ya uchochezi, kutokana mahudhurio yake katika shauri hilo kuwa na matatizo.

Mbali na hati ya kukamatwa kwa Lissu, ambayo ilitolewa jana,  Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, ameamuru kutolewa kwa hati za wito kwa wadhamini wa  Lissu,  ili wafike kujieleza kwa nini wasilipe fungu la dhamana walilotia saini, ambalo ni sh. milioni 10.

Hatua hizo zinatokana na Lissu kushindwa kufika mahakamani hapo, huku mdhamini wake Robert Kapula, akieleza kuwa amekwenda kusikiliza kesi mkoani Mwanza.

Baada ya mdhamini huyo kueleza hayo, Hakimu Simba alihoji: “Kwanini akuomba ruhusa na kwa sababu gani mahudhurio yake yamekuwa na matatizo.”

Wakili wa Serikali, Patrick Mwita, aliitaarifu mahakama kwamba, kabla ya kuanza kusikilizwa kwa shauri hilo, washitakiwa walipeleka rufani Mahakama Kuu.

Mwita aliiomba mahakama kutoa hati ya kumkamata Lissu, ambaye hakuwepo.

Kutokana na hilo, Hakimu Simba alisema mshitakiwa huyo, ambaye alikuwa akitetewa na Wakili Faraja Mangula, angetumia busara kuomba ruhusa mahakamani.

“Kuna misingi ya busara tungeiangalia vizuri. Hati ya kumkamata Lissu, itolewe na hakuna msamaha na hati ya wito itolewe kwa wadhamini, waje kujieleza kwanini wasilipe fungu la dhamana,” aliamuru Hakimu Simba.

Hakimu huyo aliahirisha shauri hilo hadi Novemba 21, mwaka huu, litakapofikishwa mahakamani kwa kutajwa.

Mbali na Lissu, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mhariri wa gazeti la Mawio, ambalo lilifungiwa na serikali  kwa muda usiojulikana, Simon Mkina, mwandishi Jabir Idrisa na  mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob.

Hii ni takriban mara ya tatu kwa Lissu, kutokufika mahakamani, ambapo mara ya kwanza, Hakimu Simba alimtaka mshitakiwa huyo kufika kujieleza kwanini asifutiwe dhamana kwa kushindwa kuhudhuria kesi.

Hata hivyo, baada ya hakimu kueleza hayo, siku iliyopangwa walifika wadhamini wake Ibrahim Ahmed na Kapula, ambao walieleza kwamba Lissu alipata safari ya dharula kwenda nchini Ujerumani kwa matibabu.

Kutokana na taarifa hizo, Hakimu Simba alitoa onyo kwa wadhamini kuhakikisha kitendo cha mshitakiwa huyo kutohudhuria mahakamani bila ya taarifa hakijirudii tena.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka ya kula njama ya kuchapisha chapisho la uchochezi na kuchapisha taarifa ya uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.

Washitakiwa  hao wanadaiwa kutenda makosa hayo, kati ya  Januari 12 na 14, mwaka huu, jijini Dar es Salaam, ambapo kwa pamoja waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar’

LEMA MBARONI DODOMA

Katika hatua nyingine, mbunge wa jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA), ametiwa mbaroni tena na polisi mkoa wa Arusha.

Tukio la kukamatwa kwa mbunge huyo, limekuja siku chache baada ya  kukamatwa na kuhojiwa, Novemba Mosi, mwaka huu na kisha kuachiwa kwa dhamana.

Lema, alikamatwa juzi jioni, katika viwanja vya bunge mjini Dodoma na kisha kusafirishwa usiku kwenda Arusha kwa ajili ya kuhojiwa tena. Lema alikuwa akihudhuria vikao vya bunge vinavyoendelea mjini Dodoma.

Akithibitisha kukamatwa kwa Lema, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alisema ni kweli kwamba mbunge huyo alikamatwa akiwa Dodoma na kusafirishwa hadi Arusha.

Kamanda Mkumbo alisema Lema amekamatwa kwa ajili ya kuhojiwa kuhusu suala moja la msingi, ambalo hakuhojiwa alipokamatwa kwa mara ya kwanza Novemba Mosi, mwaka huu.

"Ni kweli tumemkata Lema, juzi akiwa  Dodoma, kwa kushirikiana na polisi wa mkoa wa Dodoma na kusafiri naye usiku kucha.Yupo rumande hapa kituo kikuu cha polisi na makachero wa wangu wanaendelea kumhoji," alisema.

Alisema baada ya mbunge huyo kuhojiwa, atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.

Juzi, akizungumza na waandishi wa habari mjini Arusha, Kamanda  Mkumbo, alisema Lema amekuwa akitoa kauli mbalimbali za uchochezi katika mikutano yake ya hadhara maeneo ya Arusha mjini.

No comments:

Post a Comment