Friday 14 October 2016

MWALIMU NYERERE ALIILEA FAMILIA YAKE KATIKA MAISHA YA KAWAIDA





Mwalimu Nyerere hakuwa mtu wa kujikweza. Kutokana na nafasi aliyokuwa nayo, angeweza kuishi maisha ya kifahari na kujilimbikizia mali lukuki, lakini kamwe hakuwahi wala kuthubutu kufanya hivyo.

Aliishi maisha ya kawaida na kuwalea watoto wake sawa na watoto wengine wa Kitanzania. Pia hakuwahi kujihusisha na biashara ama kununua hisa kwenye kampuni za kibiashara, ziwe za ndani ama nje.

Akizungumzia maisha hayo, mke wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere, alisema siku zote falsafa ya Mwalimu Nyerere ilikuwa ni kuiona familia yake sawa na watoto wengine wa Kitanzania.

"Mwalimu alikuwa na majukumu mengi mazito. Pia hakukuwa na pesa wakati huo. Na hata kama zingekuwepo, asingeweza kufanya hivyo,"alisema Mama Maria, alipozungumza na Uhuru miaka mitatu iliyopita.

"Kwa miaka yote niliyoishi naye, alikuwa anasema sisi ni watoto wa masikini, ndiyo misamiati aliyokuwa anatumia. Tumepata bahati tumetumwa na taifa kuongoza, si kwamba sisi ni wafalme, hivyo tunapaswa kuwaona watoto wetu wapo katika ngazi sawa na wengine.
 "Na hata angependa kuwapeleka kusoma nje, hakukuwa na pesa za kuwapeleka huko. Katika awamu ya kwanza, hata pesa za kuendesha serikali ilikuwa matatizo, hivyo hatukuwa na mawazo ya kuwasomesha watoto wetu nje. Tuliona ni vema wapate elimu ya kawaida kama watoto wengine,"alisema Mama Maria.

Aliongeza kuwa pesa kidogo zilizokuwepo wakati huo, Mwalimu alizielekeza katika kusomesha madaktari na wataalamu wengine mbalimbali kwa ajili ya kufanyakazi hizo hapa nchini na wakati mwingine kuomba msaada kwa nchi wahisani.

Mtoto wake wa tatu, Magige Nyerere anasema kamwe hajutii malezi waliyolelewa na baba yao kwa sababu alikuwa rais wa Watanzania wote, hivyo angewalea tofauti na watoto wengine, angepoteza uhalali wa kuwa kiongozi wa nchi.

Magige alisema bila kuwa baba wa familia yako, ni vigumu kuwa baba wa taifa na kwamba, watoto wa rais wanapaswa kuwa sawa na watoto wengine wa Kitanzania, haipaswi kuwepo tofauti.

"Hiyo ndiyo sifa ya uongozi, sio unakuwa rais, lakini maisha ya familia yako yanakuwa ya juu kuliko ya unaowaongoza," alisema mzee huyu mcheshi na anayependa kucheka kila anaposisitiza jambo fulani.

Aliongeza kuwa sababu hizo pia ndizo zilizomfanya Mwalimu Nyerere asijihusishe na mambo ya biashara ama kujilimbikizia mali kwa vile angepoteza heshima ya kuwa kiongozi wa nchi.

Anasisitiza: "Mzee Nyerere alikuwa baba wa taifa, sasa ajilimbikizie mali ama kufanya biashara ili iweje?"

Kwa mujibu wa Magige, siku moja Mwalimu Nyerere aliwaeleza kwamba, Gavana wa Benki Kuu wakati huo, Anthony Nyirabu, alikuwa akimzidi mshahara, lakini alikuwa na uwezo kila alipokuwa na shida, kumwelekeza afanye chochote anachokitaka.

Alisema kamwe Mwalimu Nyerere hakuwahi kujiwa na wazo la kufikiria njia za pembeni ili kuongeza mapato. Anasema kwake hilo halikuwa jambo rahisi, licha ya ukweli kwamba, rushwa ilikuwa ngumu kuepukika kwa viongozi wengine wa serikali.

"Kiongozi anayeendekeza mambo haya, lazima atambue kwamba ipo siku ataondoka madarakani. Na raslimali za nchi lazima ziendelezwe na mwenye mamlaka ya kuzimilikisha ni rais wa nchi, sasa akiweka mbele maslahi yake ni hatari," alisema Magige.

"Cheo ni dhamana ya nchi. Unaweza kuamrisha mambo ya ajabu na yakafanyika. Ni makosa makubwa kuchagua viongozi wa aina hii kwa sababu watatupeleka pabaya," aliongeza.

Japhet Nyerere, ndugu wa Baba wa Taifa, anasema maisha aliyokuwa akiishi Mwalimu Nyerere yalikuwa ya ajabu kwa vile hakuwa akipenda
kujiweka kimbelembele na kwamba hivyo ndivyo hulka yake ilivyokuwa.

"Hakuna anayefahamu ni kwa nini alikuwa mtu wa aina hiyo," alieleza huku akionyesha mshangao.

"Hata maisha ya watoto wake yalikuwa ya kawaida. Yalikuwa sawa na maisha ya watoto wengine wa Tanzania. Hakupenda kuwadekeza watoto wake. Pia hakupenda kujilimbikizia mali. Hiyo ilikuwa sumu kwake.

"Kusema nataka niishi hivi au vile (kifahari), jambo hilo halikuwepo kabisa kichwani mwake. Alikuwa mtu wa ajabu. Hakuwahi hata kuwa na mradi wowote ama kufanya biashara. Alitegemea zaidi nafasi yake ya urais na kilimo,"alisema mzee huyo, anayeishi jirani na nyumba ya Baba wa Taifa iliyoko Butiama.

"Na hata alipokuwa akirejea Butiama kwa mapumziko, shughuli yake kubwa ilikuwa kilimo. Alipenda sana kulima. Alikuwa na shamba kubwa sana," anaongeza mzee huyo mwenye watoto 18.

Mtoto mwingine wa Baba wa Taifa, Makongoro Nyerere anasema wapo viongozi wengine, ambao walijiangalia vizuri kwa nafasi zao, iwe waziri au yeyote na kuishi vizuri na watoto wao kuwafikisha mahali wanajitegemea huku wengine wakitumia mwanya huo kufanya balaa, lakini haikuwa hivyo kwa Mwalimu Nyerere.

“Mwalimu alikuwa anaishi kwa kufundisha kwa vitendo maisha yake yote. Usichanganye bahati aliyopata yeye ya kupendwa na kuheshimiwa na wananchi baada ya kifo chake kutokana na matendo yake na alivyojiweka.

“Waswahili wanasema imani huzaa imani, chuki huzaa chuki na upendo huzaa upendo. Yeye alipata bahati hiyo. Wenzake aliowaachia walipanga utaratibu wa kumuenzi, siyo kila nchi inapanga hivyo, ilikuja kutokana na tabia zake.

“Mwalimu amepata bahati, nchi hii imeendelea kumpenda hadi sasa na nchi hii inamtunza mjane wake, haitunzi wanawe. Ni bahati kwamba heshima yake ni nzuri na mazingira yanaonyesha hiyo ni kamali mbaya, angeweza kuondoka hana nyumba.

“Ameacha nyumba mbili, moja kajengewa na chama kwa lazima, nyingine alijengewa na jeshi. Angebaki na nyumba yake binafsi ya Butiama, hali ingekuwa mbaya.

“Tusimsifu Mwalimu kwa kuwa ameondoka, alikuwa mwadilifu. Huyo mwingine umemtayarishia utaratibu gani? Mwalimu alifanya hivyo kwa sababu aliishi kwa imani na Watanzania wanamrudishia imani hiyo,”alisema Makongoro.

No comments:

Post a Comment