Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo
MGOMBEA ubunge wa jimbo la Bagamoyo kupitia CCM, Dk. Shukuru Kawambwa, amesema endapo atachaguliwa kuongoza jimbo hilo, atasimamia utekelezaji wa barabara kutoka Makofia-Matimbwa-Yombo hadi Mlandizi kwa kiwango cha lami.
Amesema utekelezaji wa barabara hiyo kuwa kwa kiwango cha lami upo katika Ilani ya CCM ya 2015-2020.
Pia, Dk.Kawambwa amewahakikishia wakazi wa Kata ya Yombo na maeneo ambayo hayajafikiwa na umeme kuwa, atashirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Umeme Vijijini (REA), kuondoa tatizo hilo.
Dk. Kawambwa alitoa ahadi hizo juzi katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika katika Kata ya Yombo.
Alisema barabara ya Makofia-Matimbwa-Yombo hadi Mlandizi kwa kiwango cha lami, itafungua milango ya kimaendeleo na kiuchumi .
Alisema kwa sasa barabara ya Bagamoyo-Makofia hadi Msata ipo kwenye hatua za mwisho za ukamilishwaji na itakapoanza ya Makofia-Mlandizi na kukamilika, itanufaisha wananchi kibiashara.
Dk. Kawambwa alieleza kuwa kwasasa upembuzi yakinifu umefanyika na kilichobakia ni tathmini ya watakaolipwa fidia katika maeneo ambako itapita barabara pamoja na hatua nyingine ili kupisha mpango lengwa.
Alisema wale wote watakaopisha njia hiyo watalipwa kwa haki kulingana na tathmini inayofanywa.
Akizungumzia suala la ukosefu wa umeme kwenye baadhi ya maeneo, alisema amejipanga kusimamia mipango iliyopo ndani ya serikali ili kuondoa adha hiyo.
"Nitahakikisha
nasimamia mipango yote na Ilani ya CCM ili niweze kupunguza makali ya kero
zinazowakabili wapigakura wangu katika sekta za afya, maji, nishati ya umeme,
elimu na miundombinu," alisema Dk. Kawambwa.
No comments:
Post a Comment