Wednesday, 30 September 2015
VIGOGO WA UKAWA KUWEKANA KITIMOTO
NA MWANDISHI WETU
VIONGOZI wa vyama vinavyounda kundi la UKAWA wanakutana leo kujadili mwenendo wa kampeni za mgombea urais wa CHADEMA, Edward Lowassa na mgombea mwenza wake, Juma Duni Haji.
Kikao hicho kinafanyika wakati Lowassa akilalamikiwa na wananchi kushindwa kukata kiu yao kwenye mikutano ya kampeni, ambapo hutumia muda mfupi tofauti na wagombea wote hivyo kupoteza mvuto kwa wananchi.
Pia, kushamiri kwa mvutano kuhusiana na mgawanyo wa majimbo miongoni mwa vyama hivyo, ambapo wagombea na viongozi wamekuwa wakikutana na changamoto na kulazimika kutatua migogo ya wagombea wa vyama hivyo.
Tangu kuanza kwa mikutano ya kampeni za urais Agosti 29, mwaka huu, Lowassa ambaye alijiuzulu wadhifa wa Waziri Mkuu kwa kashfa ya kampuni tata ya kufua umeme ya Richmond, hajawahi kutumia zaidi ya dakika 20, kuhutubia kwenye mikutano yake.
Habari za kuaminika ndani ya UKAWA zimesema kuwa, viongozi hao pia wapo kwenye msuguano mkali kutokana na msuguano wa majimbo na baadhi yao kutengwa kwenye shughuli za kampeni za urais na mgawanyo wa wabunge wa viti maalumu.
Mtafaruku huo umejitokeza, baada ya kubainika mpango wa CHADEMA wa kuhodhi nafasi za ubunge wa viti maalum kwa madai kuwa chama hicho ndicho chenye mamlaka na nguvu ndani ya UKAWA.
Chanzo hicho kimesema kuwa CHADEMA kimekuwa kikikataa kujadiliwa kwa mgawanyo huo pamoja na ruzuku kwa kudai, vyama vingine ni dhaifu na vimekuwa vikibebwa bila kuwa na mchango ndani ya umoja huo.
Mvutano huo ulionekana wazi baada ya viongozi wa NCCR Mageuzi, wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti (Bara) Leticia Mossore kudai kuwa, umoja huo umeshindwa kuweka kanuni za kujiendesha.
Alidai kuwa licha ya kukubaliana kuundwa kwa kamati zitakazoshughulikia migogoro ya kuachiana majimbo lakini hakuna kilichotekelezwa.
Chama hicho licha ya kupewa majimbo ya Kasulu Vijijini, Kigoma kusini, Muhambwe,Kasulu Mjini, Vunjo, Ileje, Mbinga Mjini, Manyovu, Buyungu, Ngara, Nkenge na Korogwe Mjini, lakini baadhi ya majimbo CHADEMA imesimamisha wagombea wake.
Hali hiyo ilijitokeza pia, baada ya mpango unaodaiwa kusukwa na CHADEMA na CUF kumtosa mwenyekiti mwenza wa UKAWA, kupitia Chama cha NLD, Emmanuel Makaidi, kuwania nafasi ya ubunge jimbo la Masasi Mjini.
Wakati Lowassa akiwa jimboni humo, hakumtambulisha Makaidi kama mgombea ubunge na kusababisha mwenyekiti huyo kususia mkutano.
Licha ya jimbo hilo kupewa NLD, Lowassa alimtaka Makaidi kuliachia ili ichukuliwe na Ismail Makombe “Kundambanda” kupitia CUF kinyume na makubaliano ya UKAWA.
Masuala mengine yatakayojadiliwa ni madai kwa baadhi ya vigogo wa CHADEMA kuomba fedha za kuendeshea kampeni kwa kutumia jina la UKAWA, bila ridhaa ya vyama husika.
Chanzo hicho kiliongeza kuwa, licha ya kukusanywa kwa fedha hizo inadaiwa kuwa vyama vingine vimekuwa vikinyimwa fedha na wafadhili kwa madai kuwa CHADEMA walishachukua kwa niaba ya UKAWA.
Hali hiyo imesababisha vyama vingine kukosa nguvu ya kufanya kampeni hata kwa wagombea udiwani wake huku CHADEMA kikiwa kimya bila kuwajulisha washirika wake.
“Ukata umekuwa tatizo ndani ya UKAWA vyama vingine haviwezi kuomba fedha za kampeni kwa sababu CHADEMA wanatumia jina la UKAWA, kukusanya fedha pasipo ridhaa kutoka vyama wenza. Kila tunapojaribu kupeleka maombi tunajibiwa na wahusika kuwa tayari wamesaidia na tukifuatilia wapokeaji tunakuta ni wenzetu, lakini hakuna taarifa,” kilisema chanzo hicho na kuongeza: “Haya ni matumizi mabaya ya jina la UKAWA katika kunufaisha wachache kwa maslahi binafsi na ya vyama vyao.”
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment