Friday 14 October 2016

HISTORIA YA MWALIMU NYERERE



JULIUS Kambarage Nyerere, alizaliwa mwaka 1922, katika kijiji cha Butiama, wilaya ya Musoma, mkoa wa Mara, wakati Tanzania ikijulikana kwa jina la Tanganyika.

Alikuwa mmojawapo kati watoto 26 wa Nyerere Burito, chifu wa kabila la Wazanaki.

Alipokuwa mtoto, Nyerere alichunga mifugo ya baba yake. Katika umri wa miaka 12, aliingia shule akitembea umbali wa kilomita 30 hadi Musoma.

Baada ya kumaliza shule ya msingi, aliendelea kusomea shule ya wamisionari Wakatoliki huko Tabora.

Katika umri wa miaka 20, alibatizwa akawa Mkristo Mkatoliki hadi mwisho wa maisha yake.

Mapadri walimuona kijana huyo kwamba ana akili nyingi, hivyo walimsaidia kusomea ualimu huko Makerere, Kampala, Uganda kuanzia mwaka 1943 hadi 1945.

Akiwa Makerere, alianzisha Tawi la Umoja wa Wanafunzi Watanganyika. Pia alijihusisha na tawi la Tanganyika African Association (TAA).

Baada ya kumaliza masomo ya ualimu alirudi Tabora na kufundisha katika shule ya St.Mary.

Mwaka 1949, alipata nafasi ya kwenda kusoma kwenye Chuo Kikuu cha Edinburgh, Uskoti, Ufalme wa Muungano, akapata M.A. ya historia na uchumi . Alikuwa Mtanganyika wa kwanza kusoma katika chuo kikuu cha Uingereza na wa pili kupata shahada ya elimu ya juu nje ya Tanganyika.

Aliporejea kutoka masomoni, alifundisha Historia, Kiingereza na Kiswahili katika shule ya St. Francis (sasa sekondari ya Pugu), iliyoko nje kidogo ya  Dar es Salaam.

Mwaka 1953 alichaguliwa kuwa Rais wa chama cha Tanganyika African Association (TAA), ambacho alikisaidia kukijenga alipokuwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Makerere.

Mwaka 1954, alibadilisha jina la chama cha TAA kwenda Chama cha Tanganyika African National Union (TANU), ambacho pia kilikuwa cha kisiasa zaidi kuliko TAA. Ndani ya mwaka mmoja, chama cha TANU kikawa tayari chama cha siasa kinachoongoza nchini Tanganyika.

Uwezo wa Nyerere uliwashtua viongozi wa kikoloni, akalazimika kuchagua kati ya siasa na kazi ya ualimu. Nyerere alisikika akijisemea kuwa mwalimu kwa kuchagua na mwanasiasa kwa bahati mbaya.

Alijiuzulu ualimu na kuzunguka nchi nzima ya Tanganyika kuzungumza na watu wa kawaida na machifu ili kuleta umoja katika kupigania uhuru. Pia alizungumza kwa niaba ya TANU katika Trusteeship Council na Fourth Committee ya Umoja wa Mataifa (UN) huko New York.

Uwezo wake wa kuongea na wa kuunganisha watu, ulimwezesha kufanikisha Tanganyika kupata uhuru bila umwagaji wa damu.

Ushirikiano mzuri aliouonyesha aliyekuwa Gavana wa wakati huo, Richard Turnbull, ulisaidia pia kuharakisha upatikanaji wa uhuru.

Nyerere aliingia katika bunge la kikoloni mwaka 1958 na kuchaguliwa kuwa Waziri Mkuu mwaka 1960.

Mwaka 1961, Tanganyika ilipata uhuru wake na tarehe 9 Desemba 1961, Nyerere alichaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika huru. mwaka mmoja baadaye akawa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Tanganyika.

Nyerere alikuwa kiungo muhimu katika muungano wa Tanganyika na Zanzibar katikakutengeneza Tanzania, mara baada ya Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964, yaliyomtoa madarakani sultani wa Zanzibar, Jamshid bin Abdullah.

Tarehe 5 Februari, 1977, aliongoza chama cha TANU kuungana na chama tawala cha Zanzibar Afro Shirazi Party (ASP) na kuanzisha chama kipya cha CCM (Chama cha Mapinduzi), akiwa mwenyekiti wake wa kwanza.

Nyerere aliendelea kuongoza taifa hadi 1985, alipomwachia nafasi hiyo Rais wa pili, Ali Hassan Mwinyi.

Aliacha kuongoza Tanzania ikiwa ni mojawapo kati ya nchi maskini zaidi duniani, ingawa yenye huduma za elimu na afya zilizoenea kwa wananchi wengi.

Hata hivyo, aliendelea kuiongoza CCM hadi mwaka 1990, alipoamua kustaafu na kuwa mwananchi wa kawaida.

Mwalimu Nyerere alikaa muda mwingi kijijini kwake Butiama akilima shamba lake. Pamoja na hayo, alianzisha taasisi yenye jina lake, Mwalimu Nyerere Foundation. Mwaka 1996, aliteuliwa kuwa mpatanishi wa pande zinazopingana nchini Burundi.

Mwalimu Nyerere alifariki dunia Oktoba 14, 1999, katika Hospitali ya St Thomas mjini London baada ya kuugua ugonjwa wa kansa ya damu.

Miongoni mwa mafanikio makubwa yaliyoletwa na Mwalimu Nyerere ni kujenga umoja wa taifa kati ya watu wa makabila na dini tofauti, na hivyo kudumisha amani ya muda mrefu tofauti na hali ya nchi jirani, iliyofanya Tanzania iitwe 'kisiwa cha amani'.

Aidha, alistawisha utamaduni wa Kiafrika pamoja na lugha ya Kiswahili, kushinda ubaguzi wa rangi na kutetea usalama wa taifa katika vita dhidi ya mvamizi Idi Amin wa Uganda.

Pia alitoa mchango kwa vyama vya ukombozi vya nchi za Kusini mwa Afrika kama vile, Zimbabwe (ZANU), Afrika Kusini (ANC na PAC), Namibia (SWAPO), Angola (MPLA) na Msumbiji (Frelimo).

Nyerere bado anakumbukwa na Watanzania hasa wa hali ya chini kutokana na sera zake za kujali utu. Pia ataendelea kukumbukwa na Waafrika barani kote hasa kwa mchango wake mkubwa wakati wa harakati za kupigania uhuru katika nchi mbali mbali barani Afrika.

Ni mmoja wa viongozi wachache waadilifu waliokwepa kujilimbikizia mali pamoja na kutawala kwa miaka zaidi ya 24.

Mwalimu Nyerere ni kati ya viongozi wachache wa Afrika, ambao wameacha madaraka kwa hiari baada ya kutawala kwa muda mrefu, akiwa bado anapendwa na wananchi walio wengi.

Alipostaafu urais mwaka 1985, alirudi kijijini kwake Butiama, ambako aliendesha shughuli za kilimo.

Kwa ruhusa ya makao makuu ya Kanisa Katoliki duniani, Jimbo Katoliki la Musoma linashughulikia kesi ya kumtangaza mwenye heri na hatimaye mtakatifu. Kwa sababu hiyo anaitwa pia 'Mtumishi wa Mungu'.

No comments:

Post a Comment