Friday, 14 October 2016

BUTIAMA, KIJIJI KILICHOPEWA HADHI YA KUWA WILAYA



Kijiji hiki kipo katika wilaya ya Musoma Mjini. Kutoka Musoma Mjini kwenda Butiama, ni mwendo wa takriban saa moja na nusu hadi mbili kwa kutegemea aina ya usafiri. Gari zinazotumika kwenda kijiji hicho ni aina ya Noah ama Toyota Hiace. Nauli ni sh. 2500.

Butiama ni kijiji chenye nafasi kubwa kwa wakazi wake kuendesha shughuli mbalimbali za kimaendeleo, kwani kina wakazi wasiozidi 100,000, wanawake wakiwa wengi zaidi kwa wastani wa asilimia kama 60 hivi.

Wakazi wa kijiji hiki zaidi ni wakulima, hasa wa mazao ya muhogo, mtama, maharage, mahindi, viazi vikuu, ulezi, ndizi na nyanya. Ardhi ya kijiji hiki ni yenye rutuba ndio sababu mazao hayo hustawi vyema. Pia wapo wafugaji, japokuwa kwa sasa ni wachache ikilinganishwa na miaka ya nyuma. Wanafuga ng'ombe, mbuzi na kuku kidogo.

Wenyeji hasa wa Butiama ni Wazanaki. Lakini kutokana na mwingiliano wa maisha, kijiji hiki kwa sasa kimejaa watu wa makabila mbalimbali kama vile wakurya, wagita, wajaluo na hata wasukuma. Baadhi ya watu wa makabila haya wamefika Butiama kikazi, hasa  polisi na walimu na wengine wamekwenda huko kibiashara.

Usafiri unaopatikana katika kijiji hiki ni wa pikipiki, ambao ni maarufu kwa jina la bodaboda. Nauli yake hutegemea umbali wa safari. Kama si ndefu sana, utatozwa kati ya sh. 500 na sh. 1000.

Unapopita na basi kwenda stendi ya Butiama, upande wa kushoto, eneo la kijiji cha Mwitongo, ndipo ilipo nyumba ya Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Ni eneo lililozungukwa na mawe makubwa na baadhi ya nyumba zimejengwa juu ya mawe, zikiwepo nyumba mbili za Baba wa Taifa.

Mita chache kutoka nyumbani kwa Mwalimu Nyerere, upo msikiti mkubwa wa Butiama. Msikiti huu ulijengwa na Mwalimu Nyerere kutokana na fedha za msaada kutoka kwa kiongozi wa zamani wa Libya, Kanali Muamar Ghadhafi.
Pembeni ya msikiti huo, imejengwa hosteli ya ghorofa moja kwa ajili ya malazi kwa wageni mbalimbali wanaofika Butiama.

Mbali na msikiti, umbali wa mita zipatazo 300 kutoka nyumbani kwa Baba wa Taifa, lipo kanisa kubwa la Mtakatifu Maria wa Damu Azizi. Kanisa hili pia lilijengwa kwa msaada mkubwa wa Mwalimu Nyerere na pembeni yake upo ukumbi mkubwa kwa ajili ya sherehe mbalimbali.

Ukishuka stendi, umbali wa kilometa kama mbili hivi, ndipo ilipo nyumba aliyoanzia maisha Baba wa Taifa. Nyumba hii, ambayo haikaliwi na mtu, ipo mita chache kutoka ilipo nyumba aliyokuwa akiishi mama yake Bi Mgaya, ambayo nayo ipo tupu. Nyuma ya nyumba ya mama huyo, kuna nyumba aliyokuwa akiishi dada yake Nyerere, Bi Nyangeta, ambayo kwa sasa imepangishwa kwa walimu wa shule ya sekondari ya Wanzagi.

Katika eneo hilo pia zipo nyumba kadhaa za ukoo wa Chifu Wanzagi. Nyumba hizo zimejengwa kwa mpangilio mzuri, kukiwa na umbali mkubwa kutoka nyumba hadi nyumba. Nyumba aliyokuwa akiishi Chifu Edward Wanzagi Nyerere, kaka mkubwa wa Mwalimu Nyerere, ndiyo kubwa kuliko zote. Pembeni ya nyumba hiyo ndipo lilipo kaburi lake.

Nyumba ya Chifu Japhet Wanzagi, ambaye alirithi wadhifa huo mwaka 1997 kutoka kwa baba yake, ipo mwanzoni mwa eneo hilo, ikiwa imezungukwa na michongoma mirefu, mbele yake kukiwa na geti dogo kwa ajili ya kuingilia watu na magari. Ni nyumba ya kawaida, lakini uwepo wa geti na michongoma unaweza kumfanya mtu ahisi ndani yake kuna nyumba ya kifahari.

Baadhi ya wazee wa kijiji hicho waliozungumza na mwandishi wa makala hii wamesema, ipo tofauti kubwa ya kimaisha hivi sasa ikilinganishwa na miaka ya nyuma, wakati kilipokuwa kikikaliwa na jamii ya Wazanaki pekee.

"Zamani tuliishi kama jumuia moja. Tulishirikiana katika kulima mashamba ya ujamaa na kugawana mazao na pembejeo zilikuwa zikipatikana kwa wingi, yakiwemo matrekta,"anasema Mzee Pius Simon Zorwa (50), ambaye amekuwepo Butiama tangu miaka ya 1970.

"Hata wanakijiji waliweza kutambuana kirahisi na kushirikiana kwa kila kitu. Huduma ya tiba ilikuwa ikitolewa bure kwa wanakijiji na watoto wadogo walikuwa wakipatiwa chakula sehemu moja," anaongeza mzee huyo.

Kwa mujibu wa Zorwa, kwa sasa kijiji hicho kimepanuka, majengo yameongezeka, zimeanzishwa taasisi nyingi za misaada na kumekuwepo na mchanganyiko wa watu wa makabila tofauti.

"Usafiri wetu zamani ulikuwa wa matoroli ya kusukumwa na ng'ombe, yaliyotengenezwa na Wakorea. Lakini kwa sasa usafiri wa pikipiki upo mwingi, barabara nzuri, nauli yake watu wengi wanaweza kuimudu na mawasiliano ya simu pia yanapatikana kirahisi, "anasema.

"Hata sehemu za starehe nazo zimeongezeka. Hivi sasa zipo baa nyingi, maduka yameongezeka na hata huduma za M-Pesa zinapatikana. Tunachokikosa ni huduma za benki pekee, ambazo zamani zilikuwepo, lakini zikafungwa kutokana na uchache wa watu," anaongeza.

Zorwa anasema shule za sekondari na msingi nazo zimeongezeka kijijini Butiama. Amezitaja baadhi ya shule za sekondari, ambazo zimejengwa kwa msaada mkubwa wa Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono kuwa ni Ikizu, Chifu Wanzagi, Osward Mang'ombe, Busegwe na Bumagi.

Mzee mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Peter Marwa (55) anasema, kuanzishwa kwa wilaya mpya ya Butiama kumeongeza chachu ya maendeleo ya kijiji hicho kwa vile kimepanda hadhi na ongezeko la watu na huduma imekuwa kubwa.

Marwa anasema pia kuwa, kwa sasa Butiama hakuna soko maalumu la kuuzia mazao na bidhaa mbalimbali. Anasema soko maalumu hufanyika kila siku ya Jumatano katika eneo la Mtera na mazao yanayouzwa siku hiyo ni nguo, pembejeo, mboga, samaki, mitungi, mikeka, majiko na bidhaa zinginezo.

"Wakati wa soko hilo, akina mama ntilie nao hunufaika zaidi kwa kuuza vyakula na kujipatia kipato," anasema mzee huyo.

Ameielezea huduma ya maji kuwa inapatikana kwa shida na kuongeza kuwa, maji yanayopatikana ni ya visima, lakini havitoshelezi. Pia anasema vipo visima vichache vya kiasili, vilivyochimbwa miaka kadhaa iliyopita na kuendelea kutumika hadi sasa.

"Wakati wa uhai wa Mwalimu Nyerere tulikuwa tukipata huduma ya maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria, yakipitia Mgango, ambako kumejengwa tanki kubwa, lakini kwa sasa inapatikana kwa shida sana," anasema.

Kijana Andrew Mujuni (45) anasema, anasikitishwa kuona karakana kubwa ya kutengeneza magari, matreka na vipuri iliyojengwa na Wakorea kijijini hapo miaka ya 1970 kwa sasa imekufa na kubaki gofu. Anasema karakana hiyo ilikuwa mkombozi mkubwa kwa wakazi wa Butiama kwa vile mbali ya kutoa ajira kwa vijana, iliwasaidia katika shughuli za kilimo.   

"Wakorea walitusaidia sana katika kilimo na umwagiliaji mashamba, lakini hivi sasa karakana yao haipo imekufa. Pia kulikuwepo na kiwanda cha uselemala cha kijiji na cha mafundi cherehani, navyo vyote vimekufa," anasema kijana huyo.

Mujuni anasema idadi ya wageni kutoka nje ya nchi waliokuwa wakitembelea kijiji hicho nayo imepungua sana, tofauti na wakati wa uhai wa Mwalimu Nyerere. Anasema ilikuwa kawaida kwa wageni hao kufika mara kwa mara nyumbani kwa Baba wa Taifa, lakini hivi sasa wamepungua.

Anaongeza kuwa, huduma ya hospitali hivi sasa ni ya kulipia, tofauti na miaka ya nyuma, ambapo ilikuwa ikitolewa bure. Anasema gharama ya kulipia kadi hivi sasa ni sh. 2,000 na malipo ya dawa hutegemea aina ya ugonjwa na tiba yake.

Pamoja na kuwepo kwa mabadiliko hayo kimaisha, wakazi wengi wa Butiama wameelezea kufurahishwa na maendeleo yaliyopo kijijini hapo hivi sasa huku wakiwa na imani kubwa kuwa, kuanzishwa kwa wilaya kutachochea zaidi maendeleo yao.

No comments:

Post a Comment