Thursday, 13 October 2016

WATUMISHI 928 WAHITAJIKA MLOGANZILA



WATUMISHI 928 wa awali wanahitajika katika Hospitali ya Kisasa ya Taaluma na Tiba ya Mlongazila, iliyoko nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, kwa ajili ya kutoa huduma hospitalini hapo.

Kwa sasa serikali imeshatoa vibali vya kuajiri watumishi wapya 50 na wa uhamisho 213.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Profesa Ephata Kaaya, alisema hayo juzi, alipokuwa akizungumza kwenye ziara ya mabalozi wa Tanzania walioko nchi za nje, walipotembelea hospitali hiyo.

“Kati ya maandalizi ambayo chuo kimeyafanya kuhakikisha hospitali hii inaanza kazi mara moja, ni pamoja na kufanya mikakati ya upatikanaji wa watumishi,”alisema.

Alisema pamoja na serikali kutoa kibali cha kuajiri, mahitaji kamili ya watumishi wa hospitali sio chini ya 1,300, ili vitengo na idara zote zifanye kazi kwa asilimia 100.

“Hii yote ni kwa sababu ya uhaba wa watumishi katika baadhi ya fani za afya na kutokuwepo kwa watumishi hao katika soko la ajira hapa nchini,”alisema.

Profesa Kaaya alisema wataalamu wa kigeni waliobobea katika fani za afya, ambazo kuna upungufu, wanaweza kuja chuoni na kutoa mafunzo kwa wanafunzi na madaktari bingwa wa hospitali katika fani za magonjwa ya dharura na tiba ya wagonjwa mahututi.

Alitaja wataalamu wengine wanaohitajika kuwa ni wa upasuaji wa mishipa ya fahamu na ubongo, moyo na mishipa ya damu, tumbo na ini na njia ya chakula.

Wengine ni wa upasuaji wa figo na kibofu cha mkojo, dawa ya usingizi wakati wa upasuaji, masikio, pua na koo, macho, mifupa na ajali.

Wataalamu wengine ni wa viungo bandia, viungo na tina ya ukarabati, afya ya kinywa na meno, uchunguzi na tina ya magonjwa ya damu, ugunduzi wa magonjwa na kugundua magonjwa kwa kutumia mionzi.

“Wataalamu hawa watahitajika ili kupanua wigo wa kufundisha na kutoa huduma zitakazotolewa katika hospitali hii.  Wanaweza wakaja kwa muda mfupi au wakaja kwa kujitolea kwa muda mrefu,”alisema.

Alisema wataalamu hao pia wanaweza wakaja kwa mpango maalumu wa kambi za tina kama vile kambi za upasuaji za fani mbalimbali ikiwemo upasuaji wa moyo, matumbo, macho, masikio, pua na koo.

Aidha, aliwaomba mabalozi hao kuwasaidia upatikanaji wa watalaamu hao ili waweze kushirikiana nao na kuanza kutoa huduma bora za afya pamoja na kufundisha wataalamu wa hapa nchini.

“Mipango endelevu ya chuo ni kujijengea uwezo kwa wataalamu wake wa kutosha, kwani hospitali hii ya kisasa na ya kipekee hapa nchini inahitaji wataalamu wenye weledi wa hali ya juu katika fani zote,”alisema.

Akizungumzia ujenzi wa nyumba za watumishi, wanafunzi wa uzamili, mabweni na hosteli za interns, alisema chuo kimeandaa andiko sabili kwa ajili ya ujenzi huo.

Profesa Kaaya alisema ujenzi huo unatarajia kugharimu dola za Kimarekani 320,199,835.

“Ingawa chuo kimefanya juhudi mbalimbali za kutafuta fedha hizi, bado hazijapatikana. Chuo kinawaomba waheshimiwa mabalozi kusaidia serikali kutafuta wafadhili pamoja na wawekezaji au wabia katika mradi huu,”alisema.

Hata hivyo, alisema ili kampasi hiyo ya Mlongazila iweze kukamilika pia inahitaji majengo na miundombinu ya utawala, maabara za kufundishia na tafiti, madarasa, maktaba na kumbi za mihadhara.

Alisema gharama za ujenzi wa miundombinu hiyo inakadiriwa kuwa dola za Kimarekani 510,696,243.

Kuhusu ujenzi wa Jengo la Kituo cha Umahiri katika Ukanda wa Afrika Mashariki cha Utafiti, mafunzo na tina ya magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, unatarajia kuanza Mei, mwakani.

Alisema mradi huo unafadhiliwa na serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).

Profesa Kaaya alisema makubaliano ya mkopo wa riba nafuu wa takribani dola za Kimarekani 9,500,000, kutoka AfDB ulitiwa saini Desemba, 2014.

Alisema katika mradi huo, serikali itatoa kiasi cha dola za Marekani 755,000.

“Kupitia mradi huu, jumla ya wataalamu 24, wa kada mbalimbali za magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, watapewa mafunzo katika vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi,”alisema.

No comments:

Post a Comment