Monday 5 September 2016

CCM Z'BAR YAMPA TANO RAIS MAGUFULI


CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, kimepongeza hotuba ya Rais Dk. John Magufuli, aliyotoa katika ziara yake visiwani humo, iliyosisitiza dhamira ya serikali kuharakisha maendeleo kwa wananchi bila ya kujali tofauti za kisiasa.

CCM imesema inaunga mkono na kupongeza kwa dhati hotuba hizo mbili, zilizotolewa Unguja na Pemba, zilizosisitiza dhamira ya serikali zote mbili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Zanzibar, kuwaletea wananchi maendeleo bila ya kujali itikadi za kisiasa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) wa Idara ya Itikadi na Uenezi Zanzibar, Waride Bakari Jabu,  alisema  viongozi na wananchi kwa ujumla wanatakiwa kushirikiana katika ujenzi wa maendeleo ya nchi ili Zanzibar iweze kufikia hadhi ya kuwa nchi yenye uchumi mkubwa Afrika.

Alisema ziara hiyo imetoa muongozo imara wa kuwakumbusha watendaji na viongozi nchini juu ya dhamana na mambo ya msingi wanayotakiwa kuyatekeleza kwa wananchi.

“CCM tunaunga mkono kwa nguvu zote hotuba ya Rais wetu Dk. Magufuli kwa kuwa imezungumzia na kugusia mambo ya msingi yanayogusa maisha ya wananchi, hasa wa kipato cha chini na kutoa muongozo wa namna gani serikali zetu zinaendelea na mikakati imara ya kuimarisha uchumi na maendeleo ya nchi kwa ujumla.

"Pia, tunatakiwa kuendelea kuwa wamoja na wazalendo bila ya kujali tofauti zetu za kidini, siasa na makabila kwa kulinda amani na utulivu wa nchi zetu kwani ndio siri ya mafanikio ya nchi zetu,”alisisitiza Waride.

Katibu huyo alisema Dk. Magufuli ameonyesha nia ya dhati ya kuendelea kutafuta fursa mbalimbali za miradi ya maendeleo itakayoweza kuharakisha maendeleo ya Zanzibar.

Alisema miongoni mwa mambo ya msingi yaliyosisitizwa na Dk. Magufuli, ambayo pia yanaungwa mkono na CCM Zanzibar, ni dhamira ya kuhakikisha Zanzibar inakuwa nchi ya viwanda vya kusindika samaki wanaotokana na uvuvi wa kisasa katika bahari kuu, vitakavyotoa fursa za ajira kwa vijana na wananchi.

Waride alipongeza juhudi zinazofanywa na serikali ya muungano kwa kufungua milango ya wawekezaji wakubwa kuwekeza Zanzibar, huku wakitafuta wahisani kutoa mamilioni ya fedha za kuendesha miradi ya kijamii,  ukiwemo mradi wa maji safi Unguja, unaotekelezwa kwa fedha za mkopo kutoka India.

Alisema kwa ushirikiano wa Rais Dk. Magufuli na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, CCM inaamini Tanzania Bara na Zanzibar kwa ujumla zitakuwa nchi za kupigiwa mfano duniani katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo, kisiasa na kijamii.

Alifafanua kwamba, CCM Zanzibar inaungana na Dk. Magufuli kupinga siasa za misimamo mikali na utengano zinazofanywa na baadhi ya vyama vya kisiasa kwa kuwa haziwezi kuleta maendeleo ya nchi, badala yake zitajenga migogoro isiyo ya lazima.

Alisema CCM inasifu msimamo wa Dk. Magufuli wa kulinda Muungano na Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, huku akiahidi kuendelea kulinda amani na utulivu wa nchi kwa gharama yoyote.

Pamoja na hayo, Waride aliahidi kuwa CCM itaendelea kuwa balozi mzuri wa kuwasihi wafuasi wa CCM na wananchi kwa ujumla, kufanya siasa za maendeleo zitakazoweza kwenda sambamba na malengo ya serikali.

Aidha, alipongeza juhudi za Rais wa Zanzibar, Dk. Shein za kuongoza nchi kwa ufanisi mkubwa, licha ya kuwepo na changamoto mbalimbali za kisiasa.

Waride alieleza kuridhishwa kwa CCM Zanzibar na kauli ya Dk. Shein  ya kuwataka wapinzani kusahau serikali ya mpito kama inavyodaiwa na baadhi ya viongozi, huku akisisitiza hakuna sababu ya kuwa na aina hiyo ya serikali kwa sababu uchaguzi umefanyika kwa njia ya huru na haki.

Dk. Shein alisema kazi kubwa inayofanywa kwa sasa ni kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015, huku Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwa katika hatua ya mwisho ya kuanza kazi za kuchimba mafuta na ges ili kutoa hatua pana ya ajira kwa wananchi.

Alisema muswada wa mafuta na gesi tayari umewasilishwa katika Baraza la Wawakilishi na kusomwa kwa mara ya kwanza, ambapo katika kikao kijacho cha Baraza kitakachofanyika Septemba 26, mwaka huu, utasomwa kwa mara ya pili na kusubiri saini yake.

Ziara ya Dk. Magufuli ya kuwashukuru wananchi wa Zanzibar kwa kumchagua kuwa Rais wa Tanzania, kupitia uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana, ilifanyika katika maeneo mbalimbali Pemba na Unguja.

No comments:

Post a Comment