Monday 5 September 2016

WANANDUGU WATOZWA FAINI KWA KUKWEPA KODI



WAFANYABIASHARA wawili, ambao ni wamiliki wa Kampuni ya Nagrii Hardware and Tools, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kukubali makosa manne ya kushindwa kulipa kodi ya sh. milioni 184.

Kutokana na wafanyabiashara hao Enayat Nagrii (65), anayefanya biashara kwa jina hilo la kampuni na Hussein Nagrii (37), kukiri makosa hayo, mahakama hiyo iliwapa adhabu ya kulipa faini ya  sh. milioni 1.2, kila mshitakiwa, wakishindwa watatumikia kifungo cha miezi sita.

Pia, Hakimu Mkazi Mkuu, Emmilius Mchauru, aliyesikiliza shauri hilo, aliwaamuru wafanyabiashaara hao kulipa kodi hiyo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kutokana na wao wenyewe kukubali makosa.

Wafanyabiashara hao, ambao ni wakazi wa mtaa wa Lumumba na Narung'ombe, Dar es Salaam,  walinusurika kutumikiaa kifungo cha miezi sita jela, baada ya kufanikiwa kulipa faini.

Awali, akiwasomea mashitaka, Wakili wa Serikali, Simon Wankyo, alidai washitakiwa wanakabiliwa na mashitaka manne ya kushindwa kulipa kodi, ambayo wanadaiwa kuyatenda kati yaMei na Agosti, 2014.

Wankyo alidai Mei 31, 2014, katika barabara ya Mbozi, Chang'ombe, wilayani Temeke, Dar es Salaam, washitakiwa wakiwa wamiliki na waendeshaji wa kampuni hiyo, walishindwa kulipa kodi ya TRA, Ilala ya sh. 16,079,867.

Pia, wanadaiwa Juni 30, 2014, katika maeneo hayo, walishindwa kulipa kodi ya sh. 54,071,121. Aidha, wanadaiwa Julai 31, 2014, walishindwa kuilipa mamlaka hiyo kodi ya sh. 55,473,186.

Shitaka la nne, washitakiwa hao walikuwa wakidaiwa Agosti 30,2014, katika maeneo hayo,walishindwa kuilipa mamlaka hiyo kodi ya sh. 60,542,089.

No comments:

Post a Comment