Monday, 13 February 2017

HOJA NA HAJA YA KUFANYA MAGEUZI NDANI YA CCM


 


Na Pius Msekwa

KATIKA hotuba yake kwenye sherehe za kutimiza miaka 34, ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete alisema maneno yafuatayo kuhusu haja ya kufanya mageuzi ndani ya Chama chetu:

“Ndugu wana-CCM, jambo jingine muhimu sana la kufanya ni kuanza mchakato wa mageuzi ya ndani ya Chama chetu, ili kujiweka katika nafasi nzuri zaidi ya kushindana na kushinda katika uchaguzi ujao.  Chama chetu ni cha siku nyingi, jambo ambalo lina faida na hasara zake.  Kwa sababu ya kujulikana sana na pia uzoefu wake, kinaweza kuwa na fursa ya kupata ushindi, hasa pale ambapo watu wameridhika na matendo yake au wana hofu na mabadiliko.

"Lakini kwa upande mwingine wa sarafu, kuwapo kwa muda mrefu inaweza kuwa ndiyo hatari yetu.  Wakati mwingine watu wanaweza kutaka mabadiliko tu hata kama Chama kinafanya vizuri, kwa sababu tu ya kukinai na kutaka kuwajaribu wengine.

"Hatari inakuwa kubwa zaidi pale Chama kitakaposhindwa kuwaridhisha watu au kuwaudhi kwa baadhi ya mambo pamoja na matendo ya viongozi.  Kwa sababu hiyo, CCM lazima wakati wote ibaki kuwa ni Chama cha matumaini ya kupata mambo mapya na mazuri kwa wananchi. Kitoe matumaini ya kuwa Chama cha kuleta mabadiliko yenye tija na Chama kinachotenda mema.

"Kwa maneno mengine, Chama cha Mapinduzi kiige tabia ya nyoka ya kila baada ya muda fulani hujivua gamba lake na kupata jipya..  Hatuna budi kufanya hivyo, na kufanya hivyo sasa.

"Wakati wa vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa  vijavyo  vya tathmini, tutajadili pia suala zima la mageuzi katika Chama. Nitapenda tuelewane juu ya namna tutakavyotekeleza agenda hii muhimu kwa uhai wa Chama chetu.  Hili ndugu zangu, haliepukiki.  Lazima tukihuishe Chama ili kukiongezea mvuto mbele ya watu.
Tuutazame muundo wetu  kuona kama unakidhi haja hiyo.
Tuwatazame viongozi watendaji kama wanakidhi haja hiyo, na siyo mzigo unaokipaka matope Chama chetu.  Wale tunaoweza kuachana nao, tuachane nao kwa maslahi mapana ya Chama chetu”.

Ujumbe wa hotuba hiyo ni kama ifuatavyo:

Muhtasari wa ujumbe uliomo katika hotuba hiyo ni kama ifuatavyo:-
(i) Ni lazima tufanye mageuzi ndani ya Chama na tuyafanye sasa.
(ii) Lengo la mageuzi hayo liwe ni kukiongezea Chama chetu mvuto mbele ya wananchi.
(iii) Mageuzi hayo yajielekeze kwenye muundo wa Chama kuona kama unakidhi haja; na pili yajielekeze kwenye viongozi watendaji wake,  kuona kama wanakidhi haja hiyo. Wale ambao ni mzigo kwa Chama, tuachane nao.

Madhumuni ya waraka huu ni kufanya uchambuzi wa mambo  na mazingira ya kimataifa na ya kitaifa, ambayo inabidi tufanye mageuzi makubwa ndani ya Chama chetu, ili kukipatia uwezo wa kumudu kuendelea kuwa na mvuto kwa wananchi katika mazingira hayo.

HAJA YA KUFANYA MAGEUZI NDANI YA CHAMA SASA

Muda mfupi baada ya kutoa hotuba yake ya kuadhimisha miaka 34 ya kuzaliwa kwa CCM; Mwenyekiti wa  CCM Taifa, aliteua kikosi kazi cha watu wanaoifahamu  CCM vizuri  na kuwatuma wafanye utafiti wa kina na kutoa ushauri wa  mambo (factors), ambayo yanakiweka Chama chetu katika hali ngumu hivi sasa; ili mageuzi yanayokusudiwa yaweze kujielekeza moja kwa moja katika mambo hayo.

Ufuatao ni muhtasari wa mambo yaliyojitokeza katika uchambuzi wao:-

UWANDA WA KIMATAIFA
Kupambana na changamoto zinazosababishwa na kuwapo kwa ukoloni mamboleo.
Utafiti umebaini kwamba changamoto  zilizopo ziko katika uwanda wa kimataifa, wa kitaifa na wa  ya Chama chetu. Mageuzi yanayohitajika ni yale yatakayokiwezesha Chama chetu kukabiliana na changamoto hizo na kukidhi matarajio ya wanachama na wananchi kwa jumla ya hivi sasa na ya miaka mingi ijayo.

Changamoto za ukoloni  mamboleo
Utafiti uliofanywa unaainisha kwamba tangu Chama chetu kilipozaliwa miaka 34, iliyopita, mazingira ya kimataifa yamebadilika sana.  Kiuchumi, mfumo wa soko huria na ubepari wa kiliberali umeshika kasi sana duniani na kupewa jina la utandawazi.

Mabadiliko hayo yamesimikwa na teknologia mpya ya habari na mawasiliano; inayohusisha kompyuta, interneti, simu za mkononi na mawasiliano ya anga (telecommunications). 

Watafiti wanasema kuwa 'Ubepari wa habari unatajirisha na kufukarisha. Ndiyo maana, pamoja na juhudi kubwa za Chama chetu na serikali yake, pamoja na wananchi wenyewe, bado hali ya uchumi kwa wananchi walio wengi ni duni. Chama chetu lazima kilione hili na kulifanyia kazi'

Katika nyanja za siasa, njia zinazotumiwa na mfumo wa ukoloni mamboleo ni pamoja na kufadhili mamluki katika jamii kupitia vyama vya siasa vya upinzani, asasi zisizo za kiserikali, vyombo vya habari, wasomi na matabaka tegemezi; ili kuvitia kashikashi vyama tawala na serikali zake, kwa lengo la kuvitoa madarakani vyama vyenye historia ndefu iliyotukuka ya mapambano dhidi ya ukoloni na ukoloni mamboleo.  Kwa mfano:

•Upo mwelekeo wenye nguvu kubwa unaoshinikiza kwamba, ukomavu wa demokrasia unafikiwa pale tu yanapofanyika mabadiliko ya kukiondoa chama tawala madarakani  (regime change) . Aidha, vyama vya ukombozi kama CCM, vinaonekena kuwa vikwazo kwa ukomavu wa demokrasia.

L Limezuka wimbi duniani la kuziangusha serikali zilizokaa madarakani kwa muda mrefu.

•Midia za kijamii (social media) kama vile simu za mikononi, blogu, twitter na U-tubes,  ni vyombo vyenye nguvu kubwa katika kuhamasisha watu. Ongezeko la wasomi kutokana na kupanuliwa kwa elimu ya sekondari na vyuo vya elimu ya juu, kumeongeza idadi kubwa ya watu, hasa vijana, wanaoingia katika mtandao wa teknologia ya mawasiliano na kupashana habari.  Mfano hai ni “Jamii Forums”,  ulioundwa na vijana wa CHADEMA, ambao wanafanyakazi hatarishi kwa Chama chetu na serikali yake kwa kutoa taarifa nyingi za upotoshaji, ambazo zinasomwa na watu wengi sana duniani.

Kwa hiyo lazima CCM ifanye mageuzi yatakayokiwezesha Chama chetu kutumia fursa hii ya ‘midia jamii’  kwa manufaa ya Chama chetu, hususan, mageuzi yatakayotujengea uwezo wa kujikinga dhidi ya mashambulizi kama hayo ya Jamii Forums; kwa kuwa na
watu wenye elimu na uwezo wa kutumia teknolojia hiyo.

UWANDA WA KITAIFA

Mfumo wa rika za watu  (demographic structure)

•Taifa letu limebadilika sana katika kipindi hiki, siyo tu kwamba, idadi ya watu imeongezeka sana na kufikia zaidi ya milioni arobaini, lakini pia katika ongezeko hilo, karibu theluthi mbili ni vijana wenye umri wa miaka  thelathini na tano hadi arobaini. Asilimia arobaini ni vijana wa umri kati ya miaka kumi na tano mpaka arobaini.  Wengi wao hawana ajira za kuaminika.

Hali ngumu ya maisha ya watu.
•Kutokana na mabadiliko makubwa ya kiuchumi duniani, watu wengi hivi sasa wana maisha magumu, hali ambayo inasababishwa na mfumuko wa bei.

•Kuhusu wafanyakazi, hasa wa kipato cha chini, ongezeko la kipato haliendani na kupungua kwa ukali wa maisha.  Kwa upande wa wakulima wetu,  hata kama mazao yao yanaongezeka, lakini kipato chao kutokana na mazao hayo  hakiongezeki kwa uwiano sawia.

Matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2010.

Utafiti umebaini kwamba, matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2010, yamekuwa kama ‘mlio wa jogoo wa asubuhi’,  unaoarifu kwamba kumekucha.  Matokeo hayo yameonesha kupungua kwa idadi ya viti vya majimbo ya ubunge na uwakilishi, pamoja na viti vya madiwani wa kata / wadi kwa Chama chetu.

Aidha, kura walizopata wagombea wetu wa urais zilipungua kutoka asilimia 80.2 ya mwaka 2005, hadi kufikia asilimia 61.2, mwaka 2010.  Vilevile, jumla ya kura walizopata wabunge wetu pia zilipungua na kuathiri mgawo wetu wa viti maalumu CCM, ambapo ilipata jumla ya viti 187 (78%) na upinzani katika ujumla wao walipata viti 52 (22%); ikilinganishwa na viti 26 (11%) walivyopata mwaka 2005.

Ili kusitisha au kubadilisha mwelekeo huu wa kushuka kwa kura za CCM, hatuna budi kufanya mageuzi ya dhati ndani ya CCM.

Kupanuka kwa  wigo na ushiriki wa makundi mbalimbali ya jamii

Utafiti umebaini kwamba, katika miaka ya karibuni, wigo wa siasa na ushiriki wa makundi mbalimbali ya jamii umepanuka na kuingiza makundi mapya yenye ushawishi wa kipekee, ambayo ni Asasi za Kiraia, Asasi zisizo za Kiserikali; Jumuia za Kidini; Vyombo vya Habari; na wasanii. 

Ikumbukwe kwamba, zamani Chama kilikuwa na jumuia zake kubwa zilizowakilisha wakulima na wafanyakazi. Jumuia ya WASHIRIKA kwa upande wa wakulima; na JUWATA kwa upande wa wafanyakazi. Kwa sababu Chama chetu kilijulikana kuwa ni Chama cha wakulima na wafanyakazi. Kwa upande wa wanafunzi, kulikuwa na MUWATA,  lakini hivi sasa Chama chetu hakiko karibu na makundi mengi ya jamii yaliyopo sasa.

Chama hakina budi kubuni mikakati ya kuwa karibu na makundi haya, ambayo hivi sasa yako nje ya jumuia zile tatu zinazoongozwa na Chama.

Suala la Udini.

Utafiti umebaini kwamba, suala  la udini ambalo ni hatari sana kwa uhai wa Chama chetu na umoja wa Taifa letu, lilijitokeza kwa nguvu wakati wa uchaguzi uliopita. Lakni ni viongozi wachache sana walioweza kujitokeza kulikemea suala hili hatarishi.

Hatuwezi kushinda vita dhidi ya udini na ukabila, endapo tutawaachia viongozi wachache tu kuyakemea maovu hayo.

Hivyo lazima tufanye mageuzi, ambayo yatawajibisha viongozi wa ngazi zote kukemea mambo yote yale ambayo Chama chetu kinayapiga vita, kutokana na kuwa hatarishi kwa amani na umoja wa Taifa letu.

Suala la rushwa

Utafiti umebaini kwamba, suala la rushwa limekwisha kuwa ni mzigo mkubwa sana kwa Chama chetu. Pamoja na juhudi kubwa, ambazo serikali ya CCM imezifanya katika kupambana na rushwa nchini, ikiwa ni pamoja na kutunga sheria mpya dhidi ya rushwa;  kuunda upya Tasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa; na kutunga sheria ya kudhibiti matumizi ya fedha katika uchaguzi; bado wananchi wengi wanainyooshea vidole CCM kwa kuishutumu kwamba inakumbatia wala rushwa.

Tunataka kufanya mageuzi yatakayotuondoa katika muonekano huo, ili tuonekane kuwa ni Chama kinachopambana na rushwa kwa vitendo

Wimbi la chuki dhidi ya CCM.

•Limezuka wimbi la chuki dhidi ya CCM, linalosababishwa na kelele nyingi za ufisadi, unaohusishwa na baadhi ya viongozi wa CCM; rushwa katika uchaguzi, hususan wakati wa kura za maoni ndani ya Chama;  chuki dhidi ya baadhi ya  viongozi watendaji wa CCM, ambao waliwadhulumu  baadhi ya wagombea ubunge na udiwani kwa kuchakachua matokeo au kubadilisha orodha za ushindi zilizopelekwa kwenye Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

UWANDA WA NDANI YA CHAMA CHETU.

Muundo na mfumo wa Chama

Tatizo ambalo utafiti uliliona katika muundo wa Chama chetu, ni umbali uliopo baina ya viongozi na wanachama wetu. Yaani viongozi wetu wako mbali na wanachama wa kawaida.  Viongozi wengi wa ngazi za juu huishia kukutana na viongozi wenzao tu wa ngazi za chini yake. Viongozi wa wilaya wanaishia kuekekeza viongozi wa kata; viongozi wa kata wanaishia kutoa maelekezo kwa viongozi wa matawi; na viongozi wa matawi wanaishia kutoa maelekezo kwa viongozi wa mashina. Hali hii inawafanya viongozi wa kila ngazi kuwa ni mangimeza.

Kuna haja ya kufanya mageuzi yatakayowajibisha viongozi wa CCM kuwa karibu na wanachama wetu. Aidha, kuna haja ya kufanya mageuzi katika mfumo wa utendaji kazi ndani ya Chama.
Utafiti umebaini kuwa vikao vingi vya Kikatiba havifanyiki kama inavyotakiwa. Mageuzi yanahitajika, yatakayoondoa upungufu huu ndani ya Chama chetu.

Uwingi wa shughuli za uchaguzi

Utafiti umebaini kuwa katika kila kipindi cha uongozi cha miaka mitano, CCM hutumia miaka minne kwa shughuli za uchaguzi tu, na kila uchaguzi una majeruhi wake. Kwa mfano, katika kipindi cha uongozi kilichoishia 2015;  CCM ilikuwa na uchaguzi mkuu wa Chama mwaka 2012; mwaka 2013 ulifanyika uchaguzi wa Jumuia za Chama; mwaka 2014 uchaguzi wa serikali za vijiji; mwaka 2015 uchaguzi mkuu wa serikali kuu.

Iko haja ya kuangalia uwezekano wa kufanya uchaguzi wa Chama na Jumuia zake katika mwaka mmoja, ili kupata nafasi na muda wa kutosha kufanya kazi za Chama ndani ya Chama na ndani ya umma; na kufanya maandalizi kwa ajili ya uchaguzi wa kuingia katika vyombo vya dola, ili kukiwezesha Chama kupata ushindi mnono kutokana na maandalizi makini.

Utaratibu wa utoaji kadi za uanachama wakati wa kura za maoni.

Utafiti umebaini kuwa utaratibu wa utoaji kadi za uanachama, unahitaji kufanyiwa mabadiliko. Ingefaa kuwe na siku ya mwisho wa utoaji kadi kwa wanachama kabla ya siku ya upigaji kura za maoni.

Katika uchaguzi wa mwaka 2010, muda huo wa mwisho kwanza uliwekwa kuwa Juni 30, 2010, halafu ukaongezwa hadi tarehe  Julai 15, 2010.  Uzoefu wa matatizo yaliyojitokeza katika uchaguzi huo unatosha kutuwezesha kufanya mabadiliko ya kuweka muda mrefu zaidi. Wapo wanaoshauri kwamba muda wa mwisho wa utoaji kadi za wanachama kwa ajili ya upigaji kura za maoni uwe Desemba 31 ya mwaka unaotangulia ule wa mwaka wa uchaguzi mkuu.

Taswira ya Chama chetu.

Utafiti umebaini kuwa taswira ya Chama chetu mbele ya umma imeathiriwa sana na migogoro ya viongozi na makundi yanayozozana ndani ya Chama; tuhuma za ufisadi; na udhaifu wa vikao vya Chama vya maamuzi; kujipenyeza kwa kasi kwa wafanyabiashara wasio waaminifu na adilifu katika vikao vya Chama;  na baadhi ya viongozi kujilimbikizia vyeo; kufifia kwa utamaduni wa kuwajibishana ndani ya Chama

Kufifia kwa utamaduni wa kuwajibishana ndani ya Chama pia umechangia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa imani ya wananchi kwa Chama cha Mapinduzi. CCM imebebeshwa mzigo wa kuwa ni  Chama kinachokumbatia mafisadi. Aidha, kwamba Chama kimeshindwa kuisimamia serikali yake hadi serikali ikaingia katika mikataba mibovu isiyokuwa na maslahi kwa Taifa.

Aidha, CCM imepoteza sifa yake ya awali ya kuwa ni Chama kinachojali maslahi ya wanyonge. Sasa kinabebeshwa mzigo wa kuwa ni  ‘Chama cha matajiri’.

Kwa hivyo, tunawajibika kufanya mageuzi, ambayo yataonesha kuwa CCM bado ni Chama kinachojali maslahi ya wanyonge; kwamba CCM siyo Chama kinachokumbatia mafisadi na wala rushwa.

Mageuzi ya ndani ya Chama chetu lazima yalenge katika kuondoa matatizo hayo, ili kukiongezea Chama chetu mvuto kwa wananchi.
Lengo la kukiongezea Chama chetu mvuto kwa wananchi.

2.1 Matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2010 ni kilio cha jogoo wa asubuhi.

Ili tuweze kufikia lengo hilo, mkakati wa mageuzi ndani ya Chama  hauna budi ujielekeze katika kuondoa sababu za kuwapo kwa chuki hiyo dhidi ya CCM.

Utafiti umeonesha kwamba, sababu kubwa ya kushuka kwa idadi ya watu waliokwenda kupigakura katika uchaguzi mkuu wa 2010 hadi kufikia asilimia 42% tu ya wapigakura wote waliokuwa wamejiandikisha, ilikuwa ni kwamba, wengi wa wale ambao hawakujitokeza wameichukia CCM, pengine kwa sababu zinazotofautiana, lakini zaidi kutokana na kuwapo kwa shutuma nyingi za ufisadi ndani ya CCM, pamoja na madai ya kuwalinda mafisadi hao wanaotuhumiwa.  Kwa hiyo, kuliko kwenda kuvipigia kura vyama vya upinzani na kuvipatia ushindi, wakaona njia nzuri ni kutokwenda kupigakura kabisa.

Lazima mageuzi ndani ya Chama yalenge kukiwezesha Chama kuwa na mvuto kwa wananchi ili wapende kukipigia kura.

Hilo la kwanza. Pili, ni kwamba kutokana na sura ilivyo ya Taifa letu, inayoonesha kwamba, asilimia kubwa zaidi ya wananchi wote ni vijana,  mageuzi ndani ya Chama hayana budi kujielekeza katika kuwavuta vijana waweze kukipenda zaidi Chama chetu.

Tatu, mageuzi ndani ya Chama  hayana budi yalenge katika kuvunja nguvu za  wale wanaokichukia Chama chetu kwa sababu tu ya kuwa kimekaa madarakani kwa muda mrefu, kwa hiyo wanataka mabadiliko.

Mwisho, ili utekelezaji wa mageuzi hayo ya ndani ya Chama uweze kupata ufanisi mzuri, mageuzi hayo hayana budi yawe ya aina inayokubalika na kuungwa mkono na wanachama wetu walio wengi. Ni vizuri kusisitiza maneno ‘wanachama wetu walio wengi zaidi’, kwa sababu ni dhahiri kabisa kwamba, hakuna mageuzi yatakayomridhisha kila mwanachama. Lazima wapo watakaonuna kutokana na kuathiriwa binafsi na mageuzi hayo.

3. Mageuzi hayo yajielekeze kwenye muundo wa Chama, kuona kama unakidhi haja.

Muundo wa Chama chetu umeainishwa katika Katiba ya Chama, na umekuwa ukihuishwa mara kwa mara ili uweze kwenda na wakati.
Lakini maneno ‘muundo wa Chama’ yana maana mbili. Kwanza, ni maana ya mtandao wake (network). Mtandao wake ndio umeainishwa katika Katiba ya Chama; kwamba kuna ngazi mbalimbali za Shina; Tawi; Kata / Wadi; Jimbo (kwa upande wa Zanzibar tu); Wilaya; Mkoa; na Taifa; na Jumuia zinazoongozwa na Chama. Katiba pia inaainisha vikao vilivyopo katika kila ngazi, pamoja na kazi ya kila kikao kinachohusika.

Maana ya pili ya muundo wa Chama, ni aina (composition) ya wajumbe wanaoingia katika vikao vya kila ngazi.  Uchambuzi wetu utajielekeza kwenye maana zote mbili.

Muundo wa Chama kwa maana ya mtandao wake.

Kuna mawazo au maoni ya aina mbili kuhusu muundo wa Chama kwa maana ya mtandao wake.  Aina ya kwanza ni ya wale wanaofikiri kwamba, kutokana na wingi wa ngazi zake, ambao unaweka umbali mkubwa  kutoka kwa wanachama hadi ngazi ya Taifa, unahitaji kufanyiwa mabadiliko ya kuondoa baadhi ya ngazi hizo, ili kuharakisha maamuzi kuwafikia wanachama kwa ajili ya utekelezaji;  na  kupunguza gharama za uendeshaji.  Ngazi zinazofikiriwa kuondolewa ni ngazi ya kata/wadi; na ngazi ya mkoa.

Hoja za upande wenye mawazo hayo ni hizi zifuatazo:
(a) Kwa kuwa CCM ni Chama Tawala, muundo wake una sura ya utawala zaidi kuliko sura ya uhamasishaji wa wananchi kwa lengo la kushinda uchaguzi, ambalo ndilo lengo la kwanza kabisa katika orodha ya malengo na madhumini ya Chama cha Mapinduzi, kama yalivyoorodheshwa katika Ibara ya 5 ya Katiba ya CCM.

(b) Muundo huu wa utawala umeendelea kushikiliwa na Chama bila kujali ukweli kwamba, mfumo wa utawala wa kiserikali ulifanyiwa marekebisho makubwa mwaka 1999, ambayo yaliacha mkoa ukiwa na majukumu ya ushauri tu.

(c) Chama kinafuata ngazi za utawala wa serikali hata katika maeneo ambayo hayana vyombo vya serikali vya uwakilishi na maamuzi.

(d) Hali hii imesababisha Chama kuwa na ngazi sita za maamuzi, na vikao vingi sana. Wingi wa ngazi hizi husababisha maamuzi ya Chama kuchelewa kuwafikia wanachama, hata kama vikao vya ngazi zote hizi vitakaa kwa wakati. Lakini kikao katika ngazi moja kisipokaa kwa wakati, basi kuna hatari ya maamuzi hayo kutowafikia wanachama.

(e) Wingi wa ngazi hizi maana yake ni gharama kubwa za uendeshaji

(f) Uzoefu uliopo unaonesha kwamba, muundo uliopo hautumiki ipasavyo, kwani vikao havifanyiki kwa mujibu wa Katiba ya Chama. Kutokufanyika kwa vikao kunakinzana na dhana sahihi ya Chama kwamba “Chama ni Vikao”


Aina ya pili ya mawazo ni ya wale wanaoona kuwa kuwapo na kuonekana dhahiri kuwapo kwa Chama katika ngazi zote hizo, kunaimarisha  uhai wa Chama.

Kwani  wahenga walisema, ‘asiyekuwapo na lake halipo’. Kwa hiyo ni vizuri kwa Chama kuendelea kuwapo katika maeneo yote hayo.

Muundo wa Chama kwa maana ya aina (composition) ya wajumbe wa vikao vyake.
Utafiti umeonesha kwamba, wapo wanachama wengi wenye mawazo kuwa  aina ya wajumbe wanaoingia katika Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa, inahitaji kufanyiwa mabadiliko.  Hususan, kwamba yanahitajika mabadiliko ya  ‘kutenganisha kofia’ ili wale viongozi wenye nyadhifa za kiserikali, kama mawaziri,  wazuiwe kwa mujibu wa kanuni kugombea nafasi  za ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, wala ujumbe wa Kamati Kuu, ili kuweka wazi ile dhana ya Chama kusimamia serikali yake.

Hoja ni hiyo hiyo pia kwa ngazi za chini yake, kwamba viongozi wa Chama wazuiwe kugombea nafasi katika vyombo vya dola vya ngazi inayohusika, yaani katika serikali za vijiji na katika serikali za mitaa zinazohusika.

Pamoja na hilo, pia zipo sauti nyingi miongoni mwa wanachama wa CCM, zinazosisitiza kuzingatiwa kwa ukamilifu ile kanuni inayomtaka mtu awe amekuwa mwanachama wa CCM kwa miaka isiyopungua mitano mfululizo, ndipo apate sifa ya kugombea uongozi  ama wa ndani ya Chama chetu, au wa kuiingia katika vyombo vya dola kwa tiketi ya Chama chetu.

4.  Mageuzi hayo yajielekeze kwa viongozi watendaji, kuona kama wanakidhi haja

Chama cha Mapinduzi kinao viongozi watendaji katika ngazi zote, kuanzia shina hadi Taifa. Wengi  zaidi miongoni mwao, hususan katika ngazi za shina hadi kata, siyo waajiriwa wanaolipwa mshahara kila mwezi, bali  ni viongozi wa kuchaguliwa ambao wanatekeleza majukumu yao kwa kujitolea tu.

Huu ni utekelezaji wa kifungu cha Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya uchaguzi wa mwaka 1995, kinachosema hivi:

“Kufanya kazi za Chama kwa kujitolea ndiyo mila inayoendana na mifumo ya vyama vingi duniani kote . CCM itahakikisha msimamo huu wa kujitolea unaimarika, kukubalika na kuenezwa ndani ya Chama.”

Baadhi ya wanachama wana maoni kwamba  viongozi watendaji,  ambao ni waajiriwa wangebaki  katika ngazi ya makao makuu tu; kwa maana ya kwamba wale makatibu wa CCM wa mikoa na wilaya, ukiondoa wahasibu ambao wanapaswa kuwa ni wataalamu waliosomea kazi hiyo,  wangechaguliwa na Halmashauri Kuu za CCM za ngazi hizo kama ilivyo kwa makatibu wa kata na matawi, ili kuondoa gharama kubwa  za uhamisho wa mara kwa mara wa watendaji hao.

Maoni mengine ni kwamba watendaji wa Chama wasiruhusiwe na kanuni kugombea nafasi za uongozi, ambazo wao pia huhusika katika vikao vya maamuzi  kuhusu uteuzi wa wagombea wa nafasi hizo. Kama ni suala la kutowanyima haki yao ya kikatiba ya kugombea, basi walazimike kujiuzulu nyadhifa zao wakati wanapoamua kugombea.

Utafiti uliofanywa katika eneo hili, umeonesha kwamba pamoja na kazi nzuri, ambayo imekuwa ikifanywa na  viongozi watendaji wa Chama chetu, bado kuna baadhi ya watendaji, ambao wamekuwa mzigo kwa Chama kutokana na kwamba, hawakidhi mahitaji ya Chama kwa hivi sasa, hususan kwa kutokuwa na uwezo wa kutekeleza majukumu yanayopaswa kutekelezwa.

Aidha, umeonesha kwamba, kulundikana kwa watumishi katika Makao Makuu ya Chama, ambao weledi na ufanisi wao katika utekelezaji wa shughuli walizopangiwa ni wa mashaka. Kwa hiyo imeshauriwa kwamba:

“Ili kuondokana na mzigo huu, Chama hakina budi kutathmini uwezo, maadili, na msimamo (commitment) wa watendaji wake wote na kutumia matokeo ya tathmini hiyo kuchukua hatua zifaazo.” 

Kuimarisha Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa.

Tafiti zilizofanywa zimetoa maoni kwamba, kuwapo kwa sekretarieti ni muhimu, na muundo wake unakidhi haja. Lakini  sekretariet hiyo iimarishwe katika maeneo yafuatayo:-

• Sekretarieti iwe ndogo yenye uwezo na inayofanyakazi muda wote.

•Makatibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, ambao wanasimamia idara, wawe wanafanya kazi muda wote (full time).

Mengineyo katika lengo la kukifanya Chama chetu kiwe na
Mvuto kwa wananchi

Mageuzi ndani ya Chama kwa lengo la kukifanya kirejeshe mvuto wake kwa ananchi, yanahitaji kujielekeza vilevile kwenye mambo mengine,  ambayo nayo yamesababisha kuwapo kwa hali ya  kudhoofisha  mvuto huo. Mambo hayo ni pamoja na haya yafuatayo:

SUALA LA UCHAGUZI

(A) Kuchoshwa  na mfululizo wa shughuli  za uchaguzi

Katika kila kipindi cha miaka mitano ya uongozi,  ni mwaka mmoja tu ambao hauna shughuli za uchaguzi zinazokihusu Chama cha Mapinduzi.  Kwa mfano, mwaka 2010, ulikuwa na shughuli za uchaguzi mkuu kitaifa; mwaka 2012 ulikuwa na shughuli za uchaguzi mkuu wa ndani ya Chama;  mwaka 2013, ulikuwa na shughuli za uchaguzi wa Jumuia za Chama;  mwaka 2014, ulikuwa na shughuli za uchaguzi wa serikali za mitaa ngazi ya vitongoji na vijiji;  na mwaka 2015, ulikuwa na shughui za uchaguzi mkuu kitaifa.

Yapo maoni yanayoshauri kwamba, ni vizuri mpangilio huu uhuishwe, kwa mfano, kwa kuunganisha uchaguzi wa Chama na ule wa Jumuia zake ufanyike katika mwaka ule ule mmoja.

(B)  Chama kujiwekea muda mfupi mno wa kushughulikia malalamiko ya uchaguzi.

Malalamiko mengi  yaliyopokelewa makao makuu baada ya kura za maoni katika uchaguzi wa 2010, hayakuweza kushughulikiwa wakati huo kwa sababu ya kutaka kuwahi ratiba ya Tume ya Uchaguzi ya uteuzi wa wagombea ubunge na udiwani.

Ili kuondoa tatizo hilo, kuna mawazo kwamba zoezi la kupiga kura za maoni lingefanyika mapema zaidi katika mwaka husika wa uchaguzi, ili kutoa nafasi  ya kutosha kuweza kushughulikia malalamiko yanayowasilishwa makao makuu, ambayo baadhi yake  yanathitihsha kuwa mlalamikaji huyo kweli hakutendewa haki. Lakini hapakuwa na muda wa kutosha kushughulikia malalamiko hayo ili muhusika aweze kupewa haki yake  aliyodhulumiwa.

SUALA LA KUDHIBITI  WANAOKIUKA MAADILI.

Kifungu cha 159 cha Mwongozo wa Chama wa mwaka 1981, kinasema hivi:

“Imani ya kiongozi inaambukiza na kuimarisha imani ya wale anaowaongoza. Kiongozi anayegundulika kuwa ni mnafiki kwa  vitendo vyake, ni adui mkubwa kwa Chama kwani anawavunja moyo wanachama, anawavuruga wananchi na kuunda hali itakayowafanya wananchi wasiwe na imani na Chama kizima.”

Maoni yanayosikika yakitolewa na wengi katika eneo  hili, ni kwamba Chama hakina budi kuwachukulia hatua viongozi wake, ambao wanatuhumiwa kwa tuhuma, ambazo zina athari za kisiasa kwa Chama chetu, kwa maana ya kukipotezea Chama chetu imani ya wanachama na wananchi wengine, kama vile tuhuma za ufisadi. 

Ni kweli kwamba  kisheria na kikatiba,  mtuhumiwa yeyote hana hatia mpaka tuhuma hizo zitakapothibitishwa kuwa ni za kweli na chombo cha utoaji haki, yaani Mahakama.  Lakini kisiasa, tuhuma zina athari kubwa. Kwa kuzingatia hilo, kiongozi anayetuhumiwa anapaswa kujiuzulu wadhifa wake kwa maslahi ya Chama. Lakini anaposhindwa kufanya hivyo, Chama kinawajibika kumuondoa katika wadhifa alio nao, kwa maslahi hayo hayo ya Chama.

SUALA LA KUIMARISHA CHAMA KIFEDHA NA KIUTENDAJI
Ni dhahiri kabisa kwamba, Chama chetu kukiimarika kifedha na kiutendaji, matokeo yake yatakuwa ni kufanya kazi nzuri  ndani ya Chama; nje ya Chama na ndani ya Jamii;  kazi  nzuri ambayo inakijengea Chama heshima machoni mwa jamii. Uimarishaji wa Chama katika maeneo hayo  umekwisha kujadiliwa katika vikao vilivyopita, kilichobaki ni utekelezaji tu.

USHAURI NA MAPENDEKEZO.

Katika hotuba yake iliyonuliwa mwanzoni mwa waraka huu, Mwenyekiti wa CCM Taifa alisema yafuatayo:
“Nitapenda tuelewane juu ya namna tutakavyotekeleza agenda hii muhimu kwa uhai wa Chama chetu”.

Kutokana na uchambuzi uliofanywa katika vifungu vilivyotangulia vya waraka huu, tunatoa mapendekezo  ya namna tutakavyotekeleza agenda hii, kama ifuatavyo:

1. Kuhusu mundo wa Chama

Inapendekezwa kwamba muundo wa Chama kwa maana ya mtandao wake, ubaki kama ulivyo katika ngazi zake zote. Tumezingatia maoni yaliyotolewa na wale wanaofikiria kupunguza mtandao huu kwa kuondoa ngazi  za kata/wadi; na pia kuondoa ngazi ya mkoa katika mtandao huu.

Lakini tunaona kuwa kufanya hivyo hakutaleta mvuto zaidi kwa Chama chetu, ambalo ndilo lengo kuu la zoezi hili. Kuwapo na kuonekana kuwapo kwa Chama katika ngazi zote zilizopo sasa kunakipatia Chama chetu nguvu kubwa katika ushindani wake na vyama vingine ambavyo havina mtandao mkubwa kama huu wa CCM. Hiyo ndiyo sababu muhimu ya kupendekeza kwamba mtandao wa CCM ubaki kama ulivyo sasa.

Kuhusu muundo wa Chama kwa maana ya aina ya wajumbe wanaoingia katika vikao vyake, tunakubaliana na maoni ya wale wanaoshauri mabadiliko yafanyike katika ujumbe wa vikao vya ngazi ya Taifa, yaani Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa, kwa kutenganisha kofia za uongozi wa kiserikali, na zile za uongozi wa Chama katika vikao hivyo, kwa sababu ile iliyoelezwa katika sehemu ya uchambuzi,  ya kuweka wazi ile dhana ya Chama kusimamia  utendaji wa serikali yake, kwa kutenganisha wale wenye jukumu la kusimamia na wale ambao utekelezaji wao unasimamiwa.
Utaratibu huo utumike pia kwa viongozi wa ngazi za vitongoji, vijiji, na katika Halmashauri za Serikali za Mitaa zinazohusika.

Lakini tunashauri kwamba, kutenganisha huko kusihusishe nafasi ya Mwenyekiti wa Chama, ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Uongozi katika nafasi hiyo unapaswa kubaki kwa mtu mmoja, kwa sababu kuzitenganisha kunaweza kuleta mgogoro wa ‘nani zaidi’ baina ya viongozi hao wawili.  Hali itakuwa shwari kama wanaelewana. Lakini pale ambapo  kutakuwa na malumbano baina yao, Chama na serikali yake vyote vitaathirika.

Vilevile, yapo maoni yaliyotolewa kwamba  viongozi wastaafu wanakuwa wajumbe wa vikao vya kitaifa kutokana na wadhifa huo wa wastaafu,  wasamehewe jukumu hilo la kuwa wajumbe wa vikao hivyo. Badala yake, kwa kuwa ushauri na busara zao zinahitajika sana katika michakato ya kufanya maamuzi ndani ya Chama, uwekwe utaratibu wa kuwaalika pale tu ushauri wao unapohitajika, hususan katika masuala magumu na yeti; kuliko kuwatwisha mzigo wa kuwa ni  wajumbe wa kila kikao cha vikao hivyo.

Hatuoni mantiki ya maoni hayo na tunasita kukubali yaingizwe katika zoezi hili la ‘Chama kujivua gamba’. Kwani wapo wabaya wetu watakaotoa kejeli na matusi kwamba, wastaafu hao ndio walikuwa ‘gamba’  ambalo sasa CCM imelivua!

Mageuzi kujielekeza kwa watendaji wa Chama.

Muundo wa utendaji katika Chama ulibuniwa wakati wa Chama kimoja cha siasa, wakati ilipoamuliwa ‘kutenganisha kofia’ za uongozi katika Chama na uongozi katika serikali.  Katika ngazi za mikoa na wilaya, ambapo  walianza kuteuliwa makatibu wa mikoa tofauti na wakuu wa mikoa; na makatibu wa wilaya tofauti na wakuu wa wilaya. Lengo likiwa ni kuimarisha utendaji  katika Chama, kwa kuweka makatibu wa mikoa na wilaya, ambao walikuwa na kazi moja tu ya  shughuli za Chama muda wote.

Wakati huo suala la gharama za uendeshaji wa muundo huo halikuwapo, kwani gharama zote za mishahara na za uendeshaji zilikuwa zinalipwa na serikali, kupitia kwa Katibu Mkuu wa Chama.  Ndiyo sababu Chama kilikuwa kinalipa watendaji wake katika ngazi zote hadi ngazi ya  wenyeviti na makatibu wa matawi.

Baada ya kuingia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa, haikuwezekana tena kutumia fedha za serikali kulipia gharama za watendaji wa Chama Tawala peke yake.

Kwa hiyo malipo kwa watendaji wa ngazi za chini yakasimamishwa kutokana na ukosefu wa fedha za kuwalipa. Ndipo ukabuniwa utaratibu wa kuachana na kuajiri watendaji katika ngazi za kata na matawi; badala yake vyeo vya utendaji katika ngazi hiyo vikabadilishwa kuwa ni vyeo vya kuchaguliwa na Halmashauri Kuu za ngazi husika. Makatibu wa kuajiriwa wakabaki katika ngazi za mikoa na wilaya tu; pamoja na makao makuu.

Kwa maneno mengine, uamuzi huo ulitokana na sababu moja tu ya ukosefu wa fedha za kuwalipa. Hoja iliyotumika ya kuendelea kuwa na makatibu waajiriwa katika ngazi hizo za mikoa na wilaya nayo ilikuwa ni moja tu, ya kuhifadhi sura ya ‘utaifa’ wa Chama chetu.

Ilifikiriwa wakati huo kwamba, tukiacha watendaji wote wa Chama wakachaguliwa katika maeneo yao, Chama chetu kitakuwa “local’ sana na kitapoteza sifa hiyo muhimu cha kuwa ni cha kitaifa.

Maoni yaliyotolewa katika sehemu ya uchambuzi, kwamba utaratibu wa kuwabadilisha makatibu wa CCM wa mikoa na wilaya wawe pia ni viongozi wa kuchaguliwa, katika maeneo yao, pia yamejikita kwenye hoja hiyo hiyo hiyo ya gharama za kuwalipa. Lakini kwa upande mwingine, kuna usemi usemao kwamba, “all politics are local”.

Kwa hiyo pengine kuna faida ya kuwa na watendaji ambao ni ‘local’, kwani watakuwa wanazielewa ‘ocal politics’  vizuri zaidi,  kuweza kuwasaidia katika harakati za ushindani na vyama vingine katika uchaguzi. Tunashauri wazo hilo likubaliwe na lifanyiwe kazi.

Kuna suala lilngine linalowahusu watendaji wa Chama chetu, ambalo pia limejitokeza kuhusu mapungufu yaliyoonekana katika uendeshaji wa mchakato wa uchaguzi.

Malalamiko mengi yamewasilishwa makao makuu kuhusu watendaji, ambao walifanya upendeleo wa wazi wazi kwa baadhi ya wagombea katika zoezi la kura za maoni; na wengine ambao walibadilisha matokeo hayo baada ya kupitishwa na vikao husika, n.k.

Kwa kuwa malalamiko hayo yametaja majina ya wahusika pamoja na madhambi waliyoyafanya katika  mchakato huo, tunapendekeza kwamba wahusika wote waliodhulumu haki za wanachama wetu waondolewe kazini, ili kurejesha imani ya wale waliodhulumiwa, watakapoona kuwa wabaya wao wamechukuliwa hatua stahiki.

Lakini pia, kama ilivyoelezwa katika sehemu ya uchambuzi, wapo baadhi ya watendaji wa Chama chetu ambao “weledi na ufanisi wao katika utekelezaji wa shughuli walizopangiwa ni wa mashaka”,  kwa hiyo wanakuwa ni mzigo tu kwa Chama.

Tunakubaliana na maoni kwamba, ili kuondokana na mzigo huo, Chama kifanye  tathmini ya uwezo na maadili ya kila mmoja wa watendaji waliopo ili kutambua wale ambao uwezo wao wa kutekeleza majukumu yanayopaswa kutekelezwa una mashaka na kuwachukulia hatua zifaazo.  Kuhusu namna ya kutekeleza jambo hili, tunashauri zichukuliwe hatua mbili zifuatazo:

(i) Mwenyekiti wa Chama ateue kamati ndogo ya watu wenye ujuzi na uzoefu katika masuala ya utumishi wa umma, na akabidhi kwake kazi hiyo ya kutathmini watendaji wote waliopo kwa lengo la kubaini wale ambao ni mzigo kwa Chama.

(ii) Kanuni za Chama zifanyiwe marekebisho yatakayowezesha kuwapo kwa Kamati ya Ajira ya Chama, badala ya kazi hiyo kufanywa na Kamati Kuu au Halmashauri Kuu ya Taifa, kama ilivyo sasa. Hii ni kwa sababu vikao hivyo vikubwa havina nafasi ya kuwapima vizuri watu wanaoingia katika utumishi wa Chama, na kuwafanyia tathmini kila mwaka kama inavyotakiwa na kanuni za utumishi wa umma.

Kuimarisha  Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa.

Tunakubaliana moja kwa moja na maoni yaliyotolewa katika sehemu ya uchambuzi kuhusu eneo hili la muundo wa Chama, kwa maana ya watu wanaoingia katika chombo hicho muhimu; kwamba wawe ni watu ambao wanafanya kazi muda wote, bila kuwa na majukumu mengine ya kiserkali wala ya ki-bunge. Tunapendekeza hilo likubaliwe na kufanyiwa kazi ipasavyo.

Kuhusu ukubwa wa sekretarieti, tunaona kwamba ukubwa wake kama ulivyo sasa unakidhi mahitaji, kwani ni ndogo na udogo wake huo unaiwezesha kufanya kazi kwa ufanisi bila matatizo

Kudhibiti viongozi wanaokiuka maadili

Kama ilivyoelezwa katika sehemu ya uchambuzi,  maoni ya wengi ndani na nje ya Chama ni kwamba, suala la kutowachukulia hatua viongozi ambao wanatuhumiwa kwa ufisadi ndilo ambalo limekiumiza Chama chetu zaidi katika uchaguzi uliopita.

Tunakubaliana na hoja kwamba, kiongozi anayetuhumiwa kwa kosa ambalo kisiasa linavuruga imani ya wananchi kwa Chama chetu, anapaswa kujiuzulu wadhifa wake kwa maslahi ya Chama, na kama atashindwa kufanya hivyo, anakuwa ni mzigo kwa Chama. Kwa hiyo Chama kinawajibika kumwachisha uongozi alio nao. Tunashauri kwamba huo ndio uwe msimamo wa Chama chetu, na hatua zichukuliwe za kutekeleza msimamo huu.

Mengineyo kuhusu mfululizo wa chaguzi katika kipindi cha uongozi.

Maoni yaliyotolewa ni kwamba tufikirie kufanya uchaguzi wa CCM na uchaguzi wa Jumuia zake katika mwaka mmoja, badala ya kufanyika katika miaka miwili tofauti.

Hatuoni kwamba utaratibu uliopo unatupunguzia mvuto kwa wananchi, kwa sababu hatujasikia utaratibu huo ukilalamikiwa.

Tunaona kwamba, hakuna mantiki yoyote ya kufanya mabadiliko hayo, kwani hayatatuelekeza kwenye lengo lililokusudiwa la kujivua gamba.

No comments:

Post a Comment