Tuesday, 2 May 2017

SERIKALI YAAHIDI KUTOA AJIRA 52,000RAIS Dk. John Magufuli, ameahidi ajira 52,000, pamoja na kuboresha maslahi ya wafanyakazi, ikiwemo kuongeza mishahara na kuwapandisha madaraja wote wanaostahili kuanzia mwaka ujao wa fedha.

Pia, ameahidi kuendelea kulipa madeni ya wafanyakazi, ambayo kwa kiasi kikubwa yametokana na gharama za uhamisho huku akiagiza wafanyakazi kutokubali kuhama kituo cha kazi bila kulipwa fedha zao stahiki.

Rais Dk. Magufuli alitoa ahadi hiyo jana, katika hotuba yake ya Maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi (Mei Mosi), yaliyofanyika kitaifa kwenye Uwanja wa Chuo cha Ushirika, mkoani Kilimanjaro.

Alisema utekeleaji wa ahadi hizo hauna shaka na kusisitiza kuwa, serikali itazitekeleza.

Aidha, alitumia fursa hiyo kusisitiza kuwa, ifikapo Mei 15, mwaka huu, itakuwa kikomo cha wafanyakazi wenye vyeti vya kughushi, ambao walibainika kufuatia ukaguzi uliofanywa nchi nzima na ripoti kuwasilishwa kwake, Jumamosi iliyopita na Waziri wa Utumishi, Angela Kairuki.

Katika hotuba hiyo, Rais Magufuli aliwashukuru wafanyakazi na wananchi kwa ujumla, kwa uvumilivu wao tangu kuingia madarakani kwa serikali ya awamu ya tano, ambayo ilisitisha kwa muda ajira na ongezeko la mishahara kwa watumishi wa umma.

Alisema lengo lilikuwa ni kutatua changamoto za ajira zilizoko kwenye mashirika na taasisi za umma, ambazo kwa kiasi kikubwa zilisababisha serikali kupoteza kiasi kikubwa cha fedha kwa malipo ya watumishi hewa na wasiostahili.

Rais Magufuli alisema nia ya serikali yake kwa wananchi ni nzuri na kwamba ni muhimu wafanyakazi na wananchi wakaendelea kuielewa na kuiunga mkono ili ifikie malengo yatakayotoa maisha mazuri kwa wafanyakazi wa sekta zote.

Akizungumza kwa furaha kutokana na uwepo wa maelfu ya wakazi wa mkoa wa Kilimanjaro na mikoa ya jirani, waliojitokeza kumsikiliza, Rais Magufuli alisema anataka wafanyakazi waishi vizuri.

"Nataka wafanyakazi waishi vizuri, tuombe mtuvumilie tu, kwa sababu tuliona kabla ya kuongeza mishahara ni vema tuwaondoe wanaopata mishahara hiyo bila kustahili. Tulitaka kusafisha kwanza nyumba," alisema Rais Magufuli.

Alisema wafanyakazi ni kundi muhimu kwenye maendeleo ya taifa lolote, hivyo Tanzania kwa nafasi yake, inalithamini na kwamba, amefurahishwa na uongozi wa sasa wa TUCTA, ambao umefanyakazi kubwa kuunganisha wafanyakazi wote nchini.

"Huu uongozi wenu wa sasa ninaupongeza sana, sijui mliuchaguaje, unachapa kazi kweli kweli. Ninawaahidi sitawaangusha, ahadi yangu ya kuwaongezea mishahara, kulipa marupurupu na kupandisha madaraja nitatekeleza.

"Sina ahadi hewa mimi, mwaka huu unaoanza ni wa kushughulika na wafanyakazi hewa, kwa hiyo mwakani tukikutana tena kama hivi, naamini Inshaallah, mambo yatakuwa mazuri sana," alisisitiza Rais Magufuli.

Kuhusu madeni ya wafanyakazi, alisema tangu serikali yake ilipoingia madarakani, tayari imelipa madeni ya wafanyakazi sh. bilioni 14.23 za mishahara na sh. bilioni 42.4 zisizo za mishahara.

Alisema bado serikali ina madeni, lakini itayashughulikia na kuyalipa, huku akisisitiz kuwa, kila malipo yatafanywa baada ya kumalizika kwa uhakiki wa deni husika ili kuepuka kulipa madeni hewa.

Kuhusu suala la ajira, alisema kama ilivyo sera ya serikali ya awamu ya tano ya kukuza uchumi kupitia sekta ya viwanda, ajira nyingi zitapatikana kwa njia mbalimbali, lakini serikali nayo kwa miradi yake ya maendeleo, idadi kubwa ya Watanzania wataajiriwa kwa nyakati tofauti.

"Mbali na ajira 52,000, tunajenga reli ambapo Watanzania wengi wataajiriwa.Ni wazi bado tuna madeni, yakiwemo ya walimu, lakini hatuwezi kulipa yote kwa wakati mmoja, fedha zingine tunatekeleza miradi mbalimbali itakayotoa maelfu ya ajira kwa wananchi," alisema.

Alisisitiza kuwa lazima atatoa ajira katika mwaka ujao wa fedha kwa sababu asilimia 98, ya changamoto zilizokuwa zikiipa hasara serikali kutokana na malipo hewa kwa watumishi hewa na uwepo wa watumishi wenye vyeti vya kughushi, zimetatuliwa.

"Bado tunaendelea kuwatafuta watumishi wanaotumia ujanja kukaa kwenye nafasi walizonazo, wapo wanaojipunguzia umri kila mwaka, unaona wanazeeka, lakini hawastaafu, tutawasaka na kuwabaini," alisema Rais Magufuli.

Aidha, alisema kwa matatizo yaliyokuwepo, ambayo kila Mtanzania ni shahidi, serikali ilikuwa ikipoteza sh. bilioni 16, kila mwezi, huku kila mwaka ikipata hasara ya sh. bilioni 230.

Pia, alisema kuhusu maombi ya wafanyakazi kupitia hotuba ya Mei mosi ya Katibu Mkuu wa TUCTA, Dk. Yahaya Msigwa, kuhusu makato ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), hakuna namna nyingine zaidi ya kila mdaiwa kulipa.

Alisema bodi ya mikopo ina changamoto nyingi, ikiwemo baadhi ya wanufaika kutokulipa kwa wakati madeni yao, hivyo kuipa wakati mgumu taasisi hiyo kujiendesha, hivyo asilimia 15 iliyowekwa kisheria ni vyema ikasimamiwa.

Kuhusu ombi la kupanuliwa kwa Wizara ya Elimu, ambalo pia lilikuwemo kwenye hotuba ya Katibu Mkuu wa TUCTA, alisema suala hilo haliwezekani kwa sababu lengo la serikali yake ni kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.

Dk. Magufuli alisema serikali inaendelea kuyafanyia kazi mapendekezo ya TUCTA kuhusu kupunguza idadi ya mifuko ya hifadhi ya jamii kutoka iliyopo sasa hadi kufikia miwili, ili kuharakisha ulipaji wa mafao kwa wastaafu.

Aidha, aliagiza taasisi ambazo hazina mabaraza ya wafanyakazi, ziunde haraka kwa sababu ni maelekezo ya kisheria, ili matatizo ya wafanyakazi yajulikane na kushughulikiwa kwa utaratibu unaofahamika.

Rais Magufuli pia, alisema amepokea maombi ya wafanyakazi ya kuboreshwa kwa mfumo wa bima ya ajira, ili kusaidia wafanyakazi kulipwa mafao yao pale wanapositisha utumishi kabla ya umri wa kustaafu bila usumbufu wowote.

Katika sherehe hizo, viongozi mbalimbali wa ngazi za juu wa serikali, akiwemo Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge, Job Ndugai, Naibu wake, Dk. Tulia Ackson,
mawaziri mbalimbali na wabunge, walihudhuria na kuahidi kutekeleza yote aliyoagiza Rais Magufuli kwenye maadhimisho hayo.

Katika hatu nyingine, Emmanuel Mohammed anaripoti kuwa, vyama vya wafanyakazi vimetakiwa kujikita zaidi kwenye kuwaelimisha na kuwahimiza wafanyakazi kutambua sheria za kazi na haki zao.

Mbali na hilo, vyama hivyo vimetakiwa kuendelea na juhudi za kuingiza idadi kubwa ya wafanyakazi kwenye vyama husika kwa lengo la kutetewa maslahi yao na kutatuliwa changamoto mbalimbali.

Hayo yalisemwa jana, Dar es Saalam, katika Uwanja wa Uhuru na mbunge wa Urambo, Margareth Sitta, wakati wa sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei mosi).

Alisema ni jukumu la vyama hivyo kuhakikisha vinatatua changamoto zilizoko kwa wafanyakazi hao, ikiwemo mifumo ya mishahara duni.

“Lazima vyama hivyo vizungumzie mara kwa mara changamoto hizo kama vile makato ya kodi kubwa na unyanyasaji kwa wafanyakazi kwenye sekta binafsi,”alisema

Mbunge huyo alisema jana ilikuwa siku ya kuzungumzia masuala ya changamoto, ambazo wanazipata wafanyakazi na kuweka utamaduni wa kusemea matatizo ya wafanyakazi.

Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Kanda ya Dar es Saalam (TUCTA), George Faustine, alisema shirikisho hilo linaunga mkono hatua ya serikali kuwafukuza kazi wafanyakazi wenye vyeti feki.

Alisema suala la vyeti feki kwa wafanyakazi nchini ni janga kubwa na kwamba, sio kwa watumishi wa serikali tu, ambao wamefanya hivyo bali hata sekta binafsi.

“Haki hiyo inatokana na kwamba, mfumo uliokuwa awali wa kuajiri ni hafifu hivyo kuna haja ya kuboresha mfumo huo ili kuondoa janga hilo,”alisema.

Kaimu Mwenyekiti huyo wa kanda pia alitaja changamoto, ambazo zinawakumba wafanyakazi hao, ikiwemo kucheleweshewa fedha kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.

Alizitaja zingine kuwa ni kuwacheleweshea mishahara walimu na kutowapandisha madaraja kwa wakati, ambapo hali hiyo inachangia kupunguza morali ya utendaji kazi. 

2 comments:

 1. Ndugu Wanaotafuta Mkopo

  Wewe katika matatizo yoyote ya fedha? Je, unataka kuanza biashara yako mwenyewe? Hii kampuni ya mkopo ilianzishwa Mashirika ya haki za binadamu duniani kote kwa madhumuni ya kusaidia maskini na watu wenye matatizo ya kifedha ya maisha. Kama unataka kuomba mkopo, kupata nyuma sisi na maelezo hapa chini ya barua pepe: elenanino0007@gmail.com

  jina:
  kiasi mkopo inahitajika:
  Mkopo Muda:
  Namba ya simu ya mkononi:

  Asante na Mungu awabariki
  kujiamini
  Bi Elena

  ReplyDelete
 2. Hello.
  Mimi ni Mr Rahel binafsi wakopeshaji mkopo ambao hutoa maisha wakati nafasi ya mkopo kwa watu binafsi, makampuni ya biashara, bima, nk Je, katika shida yoyote ya kifedha au katika haja ya mkopo wa kuwekeza au unahitaji mkopo kulipa bili yako kutafuta hakuna zaidi kama sisi ni hapa kufanya matatizo yako yote ya kifedha kitu cha zamani. Sisi kutoa kila aina ya mkopo katika dhehebu lolote fedha kwa kiwango cha 2% bila fee.I upfront wanataka kutumia kati hii kubwa ya kukufahamisha kwamba tuko tayari kukusaidia kwa aina yoyote ya mkopo kutatua kwamba tatizo.Kama yako ya kifedha ndiyo basi kupata nyuma sasa kupitia barua pepe (rahelcohranloan@gmail.com) kwa maelezo zaidi, wewe ni sana makala.

  ReplyDelete