Wednesday, 30 March 2016

ORODHA YA WATUMISHI HEWA YATUA SERIKALINI

SERIKALI imesema imeshapokea ripoti kutoka kwa wakuu wa mikoa yote 26 ya Tanzania Bara, kuhusu kuondolewa kwenye malipo watumishi hewa.

Waziri  wa TAMISEMI, George Simbachawene, alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, kuwasilishwa kwa ripoti hizo ni utekelezaji wa agizo lililotolewa na Rais Dk. John Magufuli, kutaka watumishi hewa waondolewe kwenye mishahara ya wafanyakazi wa serikali.

Simbachawene alisema jana ilikuwa siku ya mwisho ya utekelezaji wa agizo hilo na kwamba, wakuu wote wa mikoa wamelitekeleza kama ilivyoagizwa.

“Taarifa za watumishi hewa tayari zimewasilishwa kwa maandishi Ofisi ya Rais-TAMISEMI kuanzia mwishoni mwa wiki.

“Kwa sasa taarifa hizo zinafanyiwa kazi na zitakapokuwa tayari kwa matumizi ya umma, zitatolewa kwa vyombo vya habari kwa lengo la kuufahamisha umma,”alisema.

Waziri huyo wa TAMISEMI alisema kwa sasa taarifa hizo zinakusanywa kwa pamoja ili kupata idadi kamili.

Wakati huo huo, mkoa wa Kilimanjaro umebaini kuwepo na watumishi hewa 111, ambao wanalipwa mishahara, akiwemo mtumishi aliyeko gerezani na wengine waliofariki.

Hali hiyo imeisababishia serikali kupata hasara ya sh. milioni 281.5, kutokana na kulipa mishahara hewa, ambapo idadi kubwa ni waalimu.

Mkuu wa Mkoa huo, Saidi Sadiki, alitoa taarifa hiyo Dar es Salaam, jana, kufuatia agizo la Rais Dk. John Magufuli, la kuhakiki watumishi hewa, ambao wamekuwa wakilipwa mishahara.

Alisema mkoa huo una watumishi 21,134 na wakati wanapita kuhakiki, walioukutwa katika vituo vya kazi ni 19,516, waliopo masomoni 1,056, na waliohama lakini bado wapo kwenye orodha ya mishahara ni 247.

Sadiki alisema watumishi sita walifariki, mmoja anatumikia kifungo na wengine waliokutwa watoro ni 79, waliostaafu 25, waliohama bila kuwepo kwenye ordha ya mishahara ni 25, waliopewa likizo na ruhusa ni 137, wagonjwa 30, waliosimamishwa kazi tisa.

Alisema uchunguzi walioufanya umebaini kuwa ofisi ya mkuu wa mkoa haina mtumishi hewa, lakini Halimashauri ya Wilaya ya Rombo inao watumishi hewa 11, ambao wametia hasara ya sh. milioni 61.5 na Manispaa ya Moshi wapo 18 waliotia hasara sh. milioni33,4.

Halmashauri ya Wilaya ya Moshi inao watumishi hewa 15, walioitia hasara serikali sh. milioni 46.3, Halmashauri ya Wilaya Hai inao watumishi hewa 31 na kusababisha hasara ya sh. milioni 88.7.

Nyingine  ni Hamashauri ya Same yenye watumishi hewa tisa, walioitia serikali hasara ya sh. milioni 43.1 na Halmashauri ya Mwanga yenye watumishi hewa 26, huku ikiwa imetia hasara sh. milioni 119.1

Sadiki alisema kwa sasa mkoa huo hauna tena watumishi hewa baada ya kufanyika kwa uhakiki huo na kuonya kuwa, atakayefanya kosa hilo atachukuliwa hatua kali za kisheria na kinidhamu.

Alisema watatumia vyombo vya usalama, ikiwemo Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na wakaguzi wa hesabu za serikali ili kuhakikisha kila aliyehusika anachukiliwa hatua na kwamba fedha za serikali zinarudishwa.

Katika hatua nyingine, jumla ya watumishi  84, wa idara mbalimbali za serikali kuu na halmashauri zilizoko mkoani Tanga, wamebainika kuwa ni hewa kufuatia  uchunguzi ulioendeshwa kutokana na agizo la Rais John Magufuli.

Hayo  yamebainishwa  na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela, ambaye amesema serikali mkoani hapa inao jumla ya wafanyakazi 24,716, waliopo katika utumishi kwenye idara za serikali kuu na halmashauri,  lakini baada ya kufanyika uchunguzi wiki iliyopita, 84 walibainika kuwa hewa.

Shigela alisema wilaya inayoongoza kwa kuwa na watumishi hewa ni Lushoto, yenye watumishi 46, ikifuatiwa na Muheza (11), Mkinga (7), Tanga Jiji (7), Pangani (5), Bumbuli (5), Korogwe Vijijini (2) na Kilindi (1).

“Kama nilivyoagiza mara baada ya kukabidhiwa ofisi,nilitoa wiki moja niwe nimeletewa orodha ya wafanyakazi hewa na leo (jana) imebainika kuwa 84  ni wafanyakazi hewa, lakini idadi kamili ya watumishi wa serikali mkoani hapa ni 24,716,” alisema Shigela.

Mkuu huyo wa mkoa alisema katika orodha hiyo, wapo watumishi hewa waliokuwa wakilipwa mishahara kila mwezi, licha ya kwamba walishastaafu muda mrefu na wengine walishafariki huku baadhi yao wakiwa wameachishwa kazi kwa makosa mbalimbali.


1 comment:

  1. Je, na wale walioko masomoni bila ya ruhusa nao pia ni hewa? pia, je, watakaporudi watapokelewa kama watumishi wa wilaya hiyo au mpaka waombe tena kazi upya?

    ReplyDelete