Thursday 21 September 2017

MGODI WAFUNGWA, MMILIKI ATIMUA MBIO




SERIKALI imefunga mgodi wa uchimbani mchanga wa Kolagwa, ulioko mkoani Pwani, ambao unamilikiwa na mwekazaji Christopher Lema.
Hatua hiyo, ilifikiwa baada ya kubainika kuwepo athari za mazingira katika eneo hilo.
Sababu nyingine iliyotajwa ni uchimbaji wa mgodi huo kutofuata utaratibu na kuwepo kwa ubadhilifu, hivyo kutakiwa uchunguzi wa kina kufanyika katika kipindi cha wiki mbili.
Akizungumza wakati wa ufungaji wa mgodi huo, uliopo wilayani Mkuranga mkoa wa Pwani, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Luhaga Mpina aliwahakikishia wananchi kwamba, serikali haiwezi kuvumilia ukiukwaji wa sheria unaofanywa na mwekezaji huyo.
Alisema kuwa utaratibu wa utoaji kibali cha uchimbaji wa mchanga katika mgodi huo  kutoka taasisi za madini, haukufuata utaratibu.
"Huu ni uchimbaji holela, zipo taasisi za serikali zimehusika kukiuka utaratibu wa sheria, hivyo uzalishaji usitishwe kuanzia sasa na wataalamu wa sekta ya madini, halmashauri na Mamlaka ya Usimamizi wa Hifadhi na Mazingira (NEMC), wafanye uchunguzi wa kina kwa wiki mbili," aliagiza Mpina.
Alisema hatua ya kupuuzwa kwa malalamiko ya wananchi wa eneo hilo kwa muda mrefu ni utendaji mbovu, kwa sababu kanuni za mazingira zinaeleza wazi masharti ya uwekezaji wa migodi ya mchanga kuwa mita  200 ya makazi ya wananchi.
Alisema ni vyema kila mwekezaji kufuatilia kwa kina na kutimiza masharti ya sheria ya uhifadhi wa mazingira.
Naibu waziri huyo pia alielekeza jopo hilo la wataalamu, iwapo watabaini ukiukwaji wa sheria,  wamtoze faini kubwa mwekezaji huyo na kumpa masharti ya kurejesha mazingira hayo katika hali ya kawaida na kulipa fidia kwa wananchi.
Alisema kwamba ameshangazwa na mwekezaji huyo kutojitokeza eneo la tukio.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkuranga Dk. Seveline Malika alisema, mgogoro  kati ya mwekezaji na wananchi hao ni wa muda mrefu na umekuwa na changamoto zaidi katika kuutatua kwa kuwa busara zinahitaji.
"Ni vyema busara zitumike ili kuchukua hatua kwa kuwa ipo  wazi, mwekezaji huyu anakiuka sheria na kunyanyasa wananchi, lakini inashangaza anapozuiwa ghafla, kunakuwapo na mazingira ya kuhakikisha anaendelea na uzalishaji," alisema.
Diwani wa Kata  ya Tengelea, Kijiji cha Kolagwa, Shabani Manda, alisema utekelezaji wa kuzingatia sheria katika mgodi huo umekuwa na mashaka kwa kuwa baraza la madiwani linapoamua kusitisha shughuli za mgodi, halmashauri wanaziruhusu.
Alisema ni vyema sheria za mazingira kuangaliwa kwa kina kwa kuwa uchimbaji huo umevuka masharti ya mkataba na sasa analazimisha shule iliyopo pembezoni  kuhama ili kupisha uchimbaji.
"Mwekezaji aliuziwa eneo na mwananchi mmoja, lenye ekari moja, sasa imefikia anachimba zaidi ya ekari saba na kufikia maeneo ya huduma za kijamii, ikiwemo shule, visima vya maji barabara na kuharibu makazi ya watu," alisema.
Nao wananchi wa kijiji hicho, akiwemo Athuman Tungi, alisema wanafunzi wa eneo hilo wapo hatarini, hivyo wanaiomba serikali kuingilia kati kwa kuwa mwekezaji huyo amekuta makazi ya wananchi.

No comments:

Post a Comment