Thursday, 21 September 2017

MAJALIWA: FEDHA TULIZOOKOA ZINATUMIKA KULETA MAENDELEO




SERIKALI imesema fedha zilizokuwa zikichotwa na mafisadi na wala rushwa, zimeanza kutumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo maji.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alipozungumza na wananchi wa Wilaya ya Longido, wakati wa uwekaji jiwe la msingi katika mradi wa maji wilayani humo, ambao thamani yake ni sh. bilioni 16.
Majaliwa alisema, serikali baada ya kusimamia vita dhidi ya wala rushwa na mafisadi, kutokana ubadhilifu waliokuwa wakiufanya kwa kuweka fedha za wizi kibindoni, sasa wanazipeleka kwa wananchi ili ziweze kutekeleza miradi.
“Mafisadi wameleta athari kubwa, wala rushwa wameleta athari, fedha ambazo zingetakiwa kwenda kwa wananchi kuhudumia miradi, ikiwemo afya, maji, elimu, kilimo, uvuvi na ujenzi wa barabara zilikuwa zikichukuliwa na mafisadi,”alisema.
“Baada ya vita hii, ambayo Rais Dk. John Magufuli ameiongoza, sisi tunapambana. Naamini na ninyi wana Longido mko pamoja na rais katika hili, twende tupigane tumalizie miradi ya maji na mingine,” alisema.
Waziri Mkuu alisema wameanza kuwapelekea fedha na kwamba, katika mradi uliozinduliwa, tayari sh. bilioni nne, zimeshatolewa ili ukamilike kwa wakati.
Alisema katika mradi huo, waliwatafuta makandarasi wanne, ambao wamepangiwa kazi za kufanya kulingana na mkataba walioingia na serikali, hivyi ana imani utakamilika kwa wakati.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, makandarasi hao waliwachuja, waliwatathmini na kuwaangalia uwezo wa na kujihakikishia kwamba, wanaweza kufanya kazi hiyo.
“Leo wana Longido tunazungumza ili kuwathibitisha mradi umeanza kujengwa, leo naweka jiwe la msingi, kazi inaendelea kwa kasi kubwa ya kukamilisha mradi huu, ambao rais atakuja kuuzindua,”alisema.
Majaliwa alisema, awali walitanguliza sh. bilioni 2.4, kwa ajili ya kutekeleza miradi kwenye vijiji na halmashauri zimefanya kazi nzuri katika miradi tisa.
Waziri Mkuu alisema serikali ya Rais Dk. Magufuli, inatekeleza miradi ya maji kwa wananchi ili wasipate shida ya kutafuta maji umbali mrefu.
Alisema mkakati wa kupeleka maji katika kampeni iliyoanzishwa na Rais Dk. Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwa, imeongeza fedha ya bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji.
“Mheshimiwa Rais katika vita tunayopigana hii, angalau fedha sasa zipo na tunaanza kuzipeleka kwenye halmashauri ili tupeleke maji, nia ni kumwezesha Mtanzania kupata maji kwa umbali usiozidi mita 400.
“Hata kama hatufiki mita 400, basi asiende umbali mrefu sana ili wapate maji kwa karibu. Kila kijiji angalau tuwe na kisima, kazi hiyo tunaendelea nayo na wana Longido muwe na imani na serikali yenu ili kuhakikisaha maji yanapatikana kwenye maeneo yenu,”alisema.
Majaliwa alisema anafahamu Longido ina wafugaji asilimia 75, ambao ni wahitaji wakubwa wa maji kwa ajili ya kunyweshea mifugo yao.
Pia, Majaliwa alisema wameongeza mabakuli ya kunyweshea mifugo ili ng'ombe waweze kupata maji, hivyo wataendelea kufanya kila linalowezekana katika hilo, kwani watapata maji kwa asilimia 100 na kila mwananchi atavuta na kupeleka kwake.
Alisema wameleta watendaji katika wilaya hiyo, ambao wanafanyakazi kwa kuongeza mtandao wa maji, hivyo serikali inaangalia uwezekano wa kuongeza wahandisi wa maji ili waweze kufanyakazi vizuri.
Majaliwa alimwagiza Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge, aendelee kutafuta vyanzo vingine vya maji na wapeleke wataalamu katika wilaya hiyo ili waendelee kufuatilia vyanzo vingine.
Waziri Mkuu alisema wakipata vyanzo vingine, itakuwa rahisi kusambaza maji na kwamba, operesheni ya kutafuta vyanzo hivyo itakapoanza, watahamia Loliondo kwani nako kuna shida kubwa ya maji.
“Kwa hiyo wataalamu wako walete Longido, lakini wapeleke na Loliondo, kutafuta vyanzo vya maji kwenye maeneo ya makazi ya watu, badala ya kutafuta maji tuwapelekee kwenye vijiji vyao, katika kipindi kifupi mtavipata na tutatafuta fedha,”alisema. 
VIWANDA
Majaliwa alisema kukiwepo maji ya kutosha katika wilaya hiyo, viwanda vingi vitajengwa.
Aliwataka wana Longido watumie fursa hiyo kwa kuanzisha viwanda pamoja na wawekezaji wengine kutokana na maji mengi yatakayopatikana.
Pia, aliwataka watumie bidhaa za ndani ili waweze kuteta tija kutokana na azimio la serikali la Tanzania ya Viwanda na wawekezaji waje wawekeze kwa wingi.
UMEME
Waziri Mkuu alisema, mkakati wa Rais Magufuli ni kuhakikisha kila Mtanzania ifikapo 2020, anakuwa na umeme na zimetengwa sh. trilioni moja kwa ajili ya vijiji vyote kuwekwa nishati hiyo.
Alisema Rais Magufuli alielekeza kwamba, kuna mambo wanatakiwa kuyaacha, ikiwemo kuwatoza wananchi sh. 380,000, kwa ajili ya kuwekewa umeme, ambapo kwa sasa itakuwa sh. 27,000.
Pia, alielekeza hakuna kujaza fomu kwa sh. 6,000, hivyo zitakuwa zinatolewa bure kwa kila Mtanzania.
Majaliwa alisema katika wilaya hiyo, vijiji vyote vitawekwa umeme na tayari walishatangaza zabuni na wameshapatikana na wameanza kazi ya kusambaza umeme.
Kwa upande wake, Waziri Lwenge aliwataka wana Longido kutunza vyanzo vya maji, ikiwemo miti na kuvuna maji ya mvua.
Alisema wilaya hiyo itapata maji kwa asilimia 100 na wameweka miundombinu mizuri kwa ajili ya mifugo na kwamba, mradi huo unatarajiwa kukamilika Julai, mwakani.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, alisema wilaya hiyo asilimia 95 ya wakazi wake ni wafugaji, ambao wanategemea maji kwa kiasi kikubwa.

No comments:

Post a Comment