Thursday 21 September 2017

KIAMA ZAIDI VYETI FEKI, WAHUSIKA SASA KURUDISHA MISHAHARA




WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki, amesema mtumishi atakayebainika kutumia cheti cha kughushi, atalazimika kurejesha mishahara yote aliyochukua.
Amewataka watumishi wa umma wanaoendelea kutumia vyeti vya kughushi, wajiondoe wenyewe kazini.
Kairuki aliyasema hayo mjini Kibaha, jana, kwenye mkutano na watumishi wa Halmashauri za Kibaha Mjini, Vijijini na watumishi wa mkoa wa Pwani, baada ya kazi ya kuhakiki vyeti iliyofanywa mkoani Pwani.
Martha Nzungu, ambaye alikuwa Katibu Tawala Msaidizi Kibaha, Waziri Kairuki aliagiza mshahara wake uondolewe baada ya cheti chake cha kidato cha nne, kubainika kuwa na kasoro ya majina.
Waziri Kairuki alisema, kuna sababu za kufanya uchunguzi wa suala lake la kutumia majina tofauti ya kwenye malipo ya mshahara na jina lake lililopo katika cheti cha kidato cha nne.
Alisema kwamba, cheti chake hicho kipelekwe Baraza la Mitihani (NECTA) kwa ajili ya kuhakikiwa.
Alipongeza hatua ya Martha kusimamishwa kazi kutokana na kushindwa kuwasilisha vyeti vya taaluma tangu Julai, mwaka huu, alipotakiwa kufanya hivyo.
 "Jitihada zinazoendelea za uhakiki wa watumishi wa umma, bado kazi hiyo imekuwa na dosari, kuna watumishi wanaoendelea kutumia vyeti visivyo vyao.
"Makatibu Tawala wa Mikoa wanapaswa kuangalia na kujiridhisha na majina ya watumishi kwenye orodha ya malipo ya mishahara ya watumishi wa umma na kwenye kazi ya uhakiki kama yanafanana.
“Majina yalioonekana kwenye zoezi la uhakiki, yanapaswa kuonekana kwenye orodha ya malipo ya mishahara na kama kuna mtumishi hajahakikiwa, anatakiwa aondolewe kwenye malipo ya mshahara,” aliongeza Kairuki.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo, alisema kazi hiyo ilifanywa mkoani hapo, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la serikali kuu kwa lengo la kubaki na watumishi wenye sifa.
Ndikilo alisema kwamba, watumishi waliopewa dhamana ya kusimamia mfumo huo wa kuhakiki watumishi, wasifanye kazi hiyo kwa kulindana ili kuepuka kuendelea kuwa na watumishi wasio na sifa.
Hivi karibuni, Martha Nzungu, ambaye ni mke wa Katibu Tawala (RAS) mstaafu wa Mkoa wa Pwani, Bernard Nzungu, alitakiwa kuwasilisha vyeti vya taaluma.
Hiyo ilitokana na kubainika jina analotambulika ni tofauti na lile la kwenye malipo.
Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Magufuli, moja kati ya vipaumbele vyake ni kuwaondoa watumishi wenye vyeti feki katika utumishi wa umma.
Tangu serikali ilipoanza kuwaondoa watumishi hewa, zaidi ya wafanyakazi 19,000, walibainika kuwa na vyeti feki.
Kuondolewa kwao kumesaidia kuokoa fedha iliyokuwa ikitumika kuwalipa mishahara, ambayo sasa zimeelekezwa katika mahitaji mengine kama elimu, maji na umeme.

No comments:

Post a Comment