Saturday 17 June 2017

MREMA: RAIS MAGUFULI AWEKA HISTORIA MAPAMBANO YA UCHUMI



Na Mwandishi Wetu

Mwanasiasa mkongwe nchini Augustine Lyatonga Mrema amesema Rais John Pombe Magufuli ameweka historia ya mapambano ya uchumi nchini kutokana na namna ambavyo analishughulikia suala la madini.

Bwana Mrema amesema kuwa kitendo cha Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Cooperation Profesa John Thornton kusafiri usiku kucha kuja kuonana na Rais Magufuli na kukubali kuilipa Tanzania fedha zote ilizokoseshwa na Kampuni Acacia ni kielelezo kuwa sio tu kuwa ujumbe wake umefika lakini zaidi inadhihirisha kuwa madai yake dhidi ya kampuni hiyo ya uchimbaji madini ni ya msingi.

“Ni kiongozi gani barani Afrika aliyethubutu kuishutumu kampuni ya nje kama alivyofanya Rais Magufuli halafu viongozi wake wakasafiri kuonana na kiongozi huyo kutaka suluhu kama alivyofanya Mwenyekiti huyo wa Barrick kwa Tanzania?”alihoji Bwana Mrema.

Mwanasiasa huyo aliungana na wito wa Rais Magufuli wa kuwataka baadhi ya watu wanaowahusisha viongozi wastaafu na taarifa za Tume za Rais za kuchunguza Makinikia.

“Si vizuri na kwamba si sheria kwa mtu yeyote kuwatukana au kuwashambulia marais wastaafu kama ilivyo kwa Rais aliye maradakani na sheria inatoa dhabu kali kwa wanaofanya hivyo” alieleza bwana Mrema.

Alibainisha kuwa kuwahusisha na taarifa hizo wakati hazijawataja kunaweza kusababisha kuigawa nchi na kuhatarisha mshikamano wa Taifa katika kipindi hiki ambacho watanzania wanapaswa kuwa kitu kimoja kumuunga mkono Rais wao na Serikali kwa hatua mbalimbali anazozichukua kuimarish uchumi.

“Tumekubali kikatiba Marais wetu waliopo madarakani na wastaafu walindwe kwa kuwa ndio ni msingi wa utulivu, amani na mshikamano wetu hivyo hatuna budi kuwaheshimu kwa kutekeleza hilo tulilokubaliana” alieleza Mrema.

Mwansiasa huyo alieleza kushangazwa kwake na baadhi ya watu wakiwemo baadhi ya wabunge kumdhihaki Rais na kutozipa uzito jitihada zake za kutetea maslahi ya nchi na kuhoji mbona wananchi wa nchi nyingine kama Uingereza na Japan hawawabezi watawala wao akimaanisha Malkia na Mfalme.

“Baadhi ya wabunge wanaacha ajenda ya msingi ya kupambana na unyonyaji unaofanywa na makapuni ya madini badala yake wanaanzisha kampeni dhidi ya Rais”alieleza Bwana Mrema na kusema kuwa vitendo hivyo ni vya kichochezi, usaliti na ni vya kizandiki kwa Taifa.

Bwana Mrema alifafanua kuwa kitendo cha baadhi ya wabunge kusema eti “Rais kama angekuwa makini” asingechukua hatua alizochukua za kuzuia mchanga na kuunda Tume ni kitendo cha kumdhallisha Rais ambaye alichaguliwa baada ya kuwashinda wagombea wengine alioshindana nao katika mbio za uchaguzi wa nafasi hiyo.

“Huyo Rais ‘makini’ ni yupi zaidi ya yule aliyewashinda wengine wote. Rais amekuja na mpango anautekeleza, tumuunge mkono…sisi ndio tuliomchagua” Alisisitiza bwana Mrema

Anabainisha kuwa haiwezekani mtu mkubwa na mashuhuri kama Profesa John Thornton atoke Canada kuja kuonana na Rais wetu tena akiwa na Balozi wa nchi yake iwe ni jambo la kupuuzwa.

Bwana Mrema alisema wako waliotaka Rais ataifishe mali za makampuni zinazotuhutumiwa kuiibia Tanzania lakini Rais Magufuli ametambua kuwa huu si wakati tena wa kutaifisha mali bali ni wa kutumia sheria zilizopo kupata haki na ndivyo anachofanya.

Mrema ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha TLP alilikumbusha Jeshi la Polisi wajibu wake wa kumlinda Rais dhidi ya kejeli za baadhi ya watu wakiwemo wabunge na kulitaka jeshi hilo kutofanya ajizi kuwakamata watu wanaofanya vitendo hivyo dhidi ya Rais na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

“Sheria ziko wazi kuhusu jambo hilo. Hata mimi mwenyewe niliwahi kushitakiwa mahakamani kwa kesi kama hiyo lakini nikashinda kwa kuwa waendesha mashitaka walishindwa kuthibitisha pasipo shaka kuwa nilifanya kosa hilo” alifafanua Mrema na kujinasibu kuwa akiwa mtu safi aliyelelewa vyema na Taifa lake kamwe hathubutu kumtusi au kumdhihaki kiongozi wa nchi yake.

Tangu Rais Magufuli aunde Tume za Kuchukunguza Mchanga wa madini kumwekuwepo na baadhi ya watu wanaopinga hatua hiyo kwa madai kuwa inaweza kuitia Tanzania katika mgogoro wa kisheria na kampuni ya Acacia.

Hata hivyo, baada ya ripoti ya Kamati ya Pili ya Uchunguzi kuwasilisha taarifa yake kwa Rais Magufuli hivi karibuni ambayo ilizidi kuonesha namna Kampuni hiyo ilivyoikosesha Serikali trilioni za shilingi, Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Cooperation Profesa John Thornton alikuja nchini kwa mashauriano na Rais.

Katika mazungumzo hayo muafaka ulifikiwa kuwa iundwe Tume ya mashauriano kati ya kampuni hiyo na Serikali huku kiongozi huyo wa Barrick akiahidi kurejeha fedha zote ambazo itabainika kuwa kampuni ya Acacia ilipaswa kuilipa Tanzania.

No comments:

Post a Comment