Friday, 13 October 2017

WANAJESHI WAWILI WA JWTZ WAUAWA DRC


ASKARI wawili wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wameuawa baada ya kushambuliwa na waasi, wakiwa katika ulinzi wa amani Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

Taarifa ya JWTZ iliyolewa kwa vyombo vya habari jana, ilisema Koplo Maselino Paschal Fabusi na Praiveti Venance Moses Chimboni, walifariki dunia baada ya kupigwa risasi na kikundi cha waasi, Oktoba 9, mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, tukio hilo lilitokea umbali wa kilomita 24, Mashariki mwa mji wa Beni.

"Majeshi yetu yamefanikiwa kuwarudisha nyuma waasi hao na kudhibiti eneo hilo,"ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

JWTZ ilisema kutokana na shambulizi hilo, Umoja wa Mataifa (UN), umeunda Bodi ya Uchunguzi kuchunguza tukio hilo.

Ilisema maofisa na askari wa JWTZ, wanaendelea kutekeleza majukumu yao katika operesheni hiyo.

"Umoja wa Mataifa unaandaa utaratibu wa kuleta miili ya marehemu nchini. Mtajulishwa utaratibu wa mapokezi, kuaga miili ya marehemu hao na mazishi,"ilisema.

No comments:

Post a Comment