Friday 14 October 2016

HOTUBA YA MWALIMU NYERERE YA KUWAAGA WATANZANIA



RAIS Julius Nyerere, amewashukuru Watanzania wote kutokana na imani na ushirikiano waliompa katika kipindi chote cha miaka 24, ambacho alikuwa Rais wa Tanganyika na hatimaye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akihutubia Taifa kwa mara ya mwisho akiwa Rais,  Novemba 4, 1985, kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam, Mwalimu alisema: "Asanteni sana Watanzania wote, mmoja mmoja, wananchi waliojiunga pamoja katika vijiji, katika vikundi vya ushirika, taasisi, mashirika yanayosaidia na wafanyakazi wote waaminifu."

"Nawashukuru kwa umoja wenu katika mapambano yote, ambayo yametukabili na bado tukaifikisha Tanzania hapa ilipo,"alisema.

Alifafanua kwamba, katika kipindi chote ambacho amekuwa akiagana na wananchi pamoja na marafiki mbalimbali wa nje, amekuwa akipata sifa nyingi, lakini sifa hizo zimetokana na mambo, ambayo Watanzania wameyafanya wao wenyewe.

Mwalimu alisema kuwa mafanikio ya kujenga Taifa la Tanzania, ambalo ni la kujivunia, hayakutokana na yeye, bali yalitokana na wananchi wenyewe, ambao walimpa imani na ushirikiano mkubwa.

"Hakuna malaika, ambaye angeweza kuijenga Tanzania peke yake, hata kama malaika huyo angekuwa anasaidiwa na kuungwa mkono na Baraza la Mawaziri, ambao wote ni malaika,"alieleza.

Aliongeza kuwa mambo mbalimbali, ambayo yamefanywa na Tanzania ni matokeo ya uamuzi wa Watanzania kutumia haki ya demokrasia kumchagua kuwa Rais pamoja na wale, ambao kwa kutimiza haki yao hiyo, walimpigia kura ya 'hapana', lakini wakaonyesha imani yao kwake baada ya matokeo ya uchaguzi kutokana na kuheshimu utaratibu wa demokrasia.

Alisisitiza: Imani kwa Rais ni fadhila muhimu kwa amani na utulivu katika nchi yeyote. Lakini siyo kila nchi inapata fadhila hiyo. Fadhila hiyo niliithibitisha zaidi wakati sehemu ya nchi yetu ilipovamiwa mkoani Kagera. Umoja wenu na vitendo vyenu katika kukabiliana na uvamizi vilinisaidia nikiwa Amiri Jeshi Mkuu."

Aliendelea kueleza kuwa, licha ya uvamizi wa Kagera, Tanzania imekumbana na matatizo mbalimbali, yakiwemo ya kuvunjika kwa Jumuia ya Afrika Mashariki, ukame na kushuka kwa bei za mazao, hasa katika kipindi cha miaka sita iliyopita, lakini Watanzania hawakufanya hamaki wala kutaka 'tuuze uhuru wetu' ili kujaribu kukabiliana na matatizo hayo.

Mwalimu alieleza kwamba Watanzania wamejenga Taifa, ambalo wengine wanalionea wivu na pia kujenga sifa ya nchi, na ni wao walijenga sifa aliyonayo.

Alisema Tanzania imekuwa ikijenga jeuri ya kizalendo na kujivunia uhuru wake kwani kwa matatizo ambayo yamekuwa yakiikabili, ingewezekana kujenga tabia ya kujikomba ili iweze kuombaomba, lakini Watanzania wamekataa tabia hiyo.

Alieleza kuwa kutokana na Tanzania kutetea haki zaidi kwa upande wa nchi zinazoendelea, wakati fulani alishukuriwa na viongozi wengi wa nchi zinazoendelea, baada ya kuzungumza kwenye Umoja wa Mataifa, masuala ambayo yalikuwa yanazigusa nchi hizo moja kwa moja.

"Hawakunishukuru kwa ajili ya ufundi wangu wa kuzungumza, walinishukuru kwa sababu nilikuwa nimesema maneno ambayo wao wasingeweza kuyasema. Sisi Tanzania tunasema ukweli na japo juhudi za nchi zinazoendelea kutaka haki zaidi hazijafanikiwa, nchi nyingi zimeanza kuelewa,"alisema.

Akizungumzia mchango wa Tanzania katika masuala yanayohusu bara la Afrika na dunia kwa jumla, Mwalimu alisema kuwa pamoja na uwezo wake mdogo, imekuwa ikipokea maelfu ya wakimbizi na kuwasaidia kujenga upya maisha na kuwasaidia wale, ambao wanapigania uhuru.

Mwalimu alisema nishani ya Nansen, ambayo alipewa kutokana na mchango wa Tanzania katika kuhudumia wakimbizi, aliipokea kwa niaba ya Watanzania.

Kuhusu ukombozi wa bara la Afrika, Mwalimu alisema wananchi ndio walioiwezesha nchi kusaidia vyama vya ukombozi nchini Msumbiji, Zimbabwe, Angola, Namibia na sehemu nyingine kutokana na michango yao ya binafsi na vikundi mbalimbali, ikiwemo damu.

"Msimamo huu unaendelea. Kuunga mkono ukombozi wa bara la Afrika ni kitendo muhimu kwa kuimarisha uhuru naa usalama wetu.

"Kwa mfano, kama tungekuwa hatukuunga  mkono ukombozi wa Msumbiji na Zimbabwe, leo hii tungekuwa tunapakana na makaburu na wangekuwa wanatushambulia. Wapigania uhuru wa Afrika wanapigania uhuru wetu. Ni wajibu wetu kuwasadia," alisisitiza.

Kuhusu mafanikio ya ndani ya nchi, Mwalimu alisema kwamba maadui wa ndani na nje wangeweza kutumia mathalani vikundi vya makabila, dini au misingi ya rangi kuwavuruga Watanzania, lakini wananchi waliyakaa mambo hayo.

Alifafanua kuwa tofauti za dini zingeweza kuwa hatari zaidi, hasa kwa kuwa wakati wa kupata uhuru, kulikuwa na karibu idadi sawa ya wakristo na waislamu, huku wakristo wakiwa na nafasi zaidi za elimu, lakini waislamu hawakukubali kugawanywa na serikali ilichukua hatua za kurekebisha mfumo wa elimu uliokuwepo wakati wa ukoloni.

Aliwachekesha wananchi na viongozi aliposema kuwa hivi sasa siyo rahisi kuwatambua wakristo na waislamu kwa majina kwa sababu wapo wakristo wenye majina ya kiislamu na waislamu wenye majina ya kikristo.

Mwalimu pia aliwashukuru viongozi mbalimbali, ambao walimsaidia kuongoza serikali na hata mahali pengine kubeba lawama kutokana na kutekeleza maamuzi yake au kutokana na makosa yake mwenyewe.

Aliwashukuru wananchi kwa kumchagua Ndugu Ali Hassan Mwinyi kuwa Rais wa Pili wa Jamhuri ya Muungano na akawataka kumsaidia kwa kuongeza juhudi ili kulikwamua Taifa kwenye hali ngumu ya kiuchumi.

Alieleza kuwa yeye anaona fahari kubwa kuitumikia Tanzania chini ya uongozi wa Rais mpya.

Mapema Mwalimu, ambaye alikabidhiwa zawadi mbalimbali na wawakilishi wa mikoa yote nchini, vikiwemo vifaa vya kilimo, chakula, mifugo na magari, alisema baadhi ya zawadi itabidi ziuzwe na fedha zake kuwekwa kwenye akaunti maalumu, ambapo nyingine zitakuwa katika sehemu maalumu ya kumbukumbu atakayojengewa na serikali huko Butiama na nyingine atazitumia pamoja na Mama Maria.

Aliwashukuru wananchi kwa zawadi hizo na kueleza kuwa hiyo ni ishara kwamba, wasingependa Rais wao wa kwanza aishi katika dhiki. Hata hivyo, alisema anaamini pia Watanzania wasingependa Rais wao awe tajiri ghafla.

No comments:

Post a Comment