Friday, 14 October 2016

MWISENGE, SHULE YA MSINGI ALIYOSOMA MWALIMU NYERERE




SHULE ya msingi ya Mwisenge ipo nje kidogo ya mji wa Musoma. Ukitaka kufika shuleni hapo kwa kutokea mjini, unaweza kutumia usafiri wa daladala kwa kulipa sh. 300 ama bodaboda kwa bei ya sh. 1,000.

Ilianzishwa mwaka 1924. Ilijengwa na wakoloni kwa lengo la kutoa elimu kwa watoto wa machifu na watemi, ikiwa kama shule ya kati ya bweni. Ilikuwa chujio la wanafunzi kabla ya kuendelea na masomo ya juu.

Shule hii ni ya kihistoria kwani ndipo aliposoma Waziri Mkuu wa Kwanza wa Tanganyika na Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Aliingia shuleni hapo Aprili 20, 1934 hadi Oktoba Mosi, 1936. Namba yake ya kuingilia shuleni ilikuwa 308.

Mbali na Mwalimu Nyerere, viongozi wengine wa serikali waliowahi kusoma shuleni hapo ni Jaji Joseph Warioba (waziri mkuu awamu ya pili), Bhoke Munanka (waziri ofisi ya rais awamu ya kwanza), Joseph Butiku (katibu ofisi ya rais na mkuu wa mkoa wa Mara) na Deusdedit Wambura (katibu ofisi ya rais awamu ya kwanza).

Wengine ni Selemani Kitundu (mkuu wa mkoa), Osward Marwa Mang'ombe (mkuu wa mkoa), Richard Wambura (balozi), Mutaragara Chirangi (katibu wa elimu) na James Mukangara (ofisa utamaduni wa mkoa).

Baada ya Uhuru mwaka 1961, shule hii ilichukuliwa na kuendeshwa na serikali na mwaka 1979, kilianzishwa kitengo cha elimu maalumu cha walemavu wa macho na walemavu wa ngozi.

Miongoni mwa majengo yanayotumika hadi sasa shuleni hapo ni pamoja na madarasa aliyosoma Mwalimu Nyerere na bweni alilokuwa akilala. Eneo la katikati ya shule hiyo, upo mnara wa kumbukumbu ya mwalimu pamoja na mfano wa dawati alilotumia wakati akisoma.

Kwenye ofisi ya mwalimu mkuu, upo ubao mkubwa mweusi wenye orodha ya majina ya baadhi ya viongozi waliosoma shuleni hapo, namba zao za kuingilia shuleni na nyadhifa walizowahi kushika serikalini.

Mmoja wa walimu waliomfundisha Mwalimu Nyerere, shuleni hapo, James Irenge, ambaye kwa sasa ni marehemu, aliwahi kuiambia Uhuru kuwa, alikuwa mwanafunzi wake katika shule hiyo kuanzia mwaka 1934 hadi 1936. Mzee huyo, aliyefariki dunia miaka mitatu iliyopita, alikuwa miongoni mwa walimu tisa wa shule hiyo ya bweni, iliyokuwa mahsusi kwa watoto wa machifu na watemi.

“Alikuwa mwanafunzi wa ajabu sana. Alikuwa na upeo wa juu. Alisoma madarasa manne kwa miaka mitatu. Mwaka 1937, alihamia shule nyingine mkoani Tabora kuendelea na darasa la tano,”alisema mwalimu huyo wa Baba wa Taifa

“Alikuwa akipenda sana kuuliza maswali mengi yanayohitaji majibu ya kina. Alikuwa na busara na kipaji cha pekee na uwezo wa kufikiri kwa makini kabla ya kutenda tendo lolote na pia alikuwa mkweli,” aliongeza Mzee Irenge, akionyesha wazi kuwa alikuwa bado ana kumbukumbu nzuri ya Mwalimu Nyerere.

“Alikuwa kijana mwenye kusikiliza mafundisho ya darasani au kutoka kwa mtu yeyote mwenye akili. Alikuwa na akili za kuzaliwa,” alisisitiza mzee huyo, ambaye aliandika muswada unaosema ‘Maisha na Sifa za Viongozi wa Tanzania Kabla na Baada ya Uhuru’, lakini kutokana na kukosa pesa, alishindwa kuuchapisha kuwa kitabu.

Mzee Irenge alisema mwaka 1936, Mwalimu Nyerere alimuomba akamuombee kwenye kikao cha walimu wote, wamkubalie aruhusiwe kufanya mitihani ya darasa la nne ili awahi kufanya mitihani ya sekondari ya Tabora, wakamkubalia. Alisema Mwalimu Nyerere aliona kusubiri hadi amalize darasa la tatu na la nne ni kupoteza muda.

Alisema aliliona ombi hilo ni la msingi na kutokana na kipaji alichokuwa nacho, aliamini angeweza kufanikiwa. Na hivyo ndivyo ilivyokuwa.

“Niliona ombi lake lingekataliwa, ingekuwa ni kumkatisha tamaa. Kikao kilikubali na kweli alifaulu,”alisema mzee Irenge, ambaye alifariki dunia miaka mitatu iliyopita.

Kwa mujibu wa Mzee Irenge, siku Wizara ya Elimu ilipomteua Mwalimu Nyerere kwenda sekondari ya Tabora, ilikuwa shangwe kubwa kwa walimu na wanafunzi wa Mwisenge. Baadhi yao walionyesha masikitiko makubwa kwa kuondoka kwake kwa vile walimpenda na kumzoea, lakini hawakuwa na la kufanya.

Mzee Irenge alisema, binafsi alijifunza mengi kupitia kwa Mwalimu Nyerere, japokuwa alikuwa mwanafunzi wake. Aliyataja baadhi ya mambo aliyojifunza kutoka kwake kuwa ni uwezo wa kufikiria kwa makini kabla ya kutenda lolote, kusema kweli tupu bila wasiwasi wala kutishika na lolote, kujisomea na kutenda kazi kwa bidii.

Kwa mujibu wa taarifa za shule hiyo miaka mitatu iliyopita, ilikuwa na wanafunzi 1,525, kati yao hao 727 walikuwa wavulana na 798 wasichana. Wanafunzi walemavu walikuwa 50, kati ya hao wavulana 26 na wasichana 24.

Majengo yaliyopo shuleni hapo ni madarasa 20 na nyumba za walimu nane. Lakini mahitaji kamili ya nyumba za walimu ni 45 na madarasa ni 39.

Pia, kumekuwepo na mafanikio makubwa kielimu, ikiwa ni pamoja na ongezeko la wanafunzi wanaofaulu mitihani ya kwenda shule za sekondari.

Kwa mfano,mwaka 2009, jumla ya wanafunzi waliofanya mitihani walikuwa 208 na waliofaulu walikuwa 115, ikiwa ni asilimia 55 ya waliofanya mitihani wakati mwaka 2010, wanafunzi waliofanya mitihani walikuwa 175 na waliofaulu walikuwa 117, ikiwa ni asilimia 67.

Changamoto zinazoikabili shule hiyo kwa sasa ni ongezeko la walimu kwenda masomoni, vifaa vya kufundishia na kujifunzia, samani kwa wanafunzi, uandikishaji wa wanafunzi na majengo kwa ajili ya walemavu.

Changamoto zingine ni ukosefu wa vifaa vya michezo kwa walemavu na walimu wa michezo wenye taaluma hiyo, uchakavu wa nyumba za walimu, vyoo, jengo la utawala na uzio utakaoipa shule heshima na ulinzi sahihi kwa walemavu, hasa wa ngozi.

Shule hiyo ilipata mradi wa ujenzi wa bweni la walemavu mwaka 2010, uliokuwa unafadhiliwa na Shirika la Terre-Des-Hommes la Uholanzi kwa lengo la kuwasaidia walemavu. Mradi huo ulihusisha ukarabati wa mabweni mawili na ujenzi wa bweni moja lenye sehemu mbili za kulala wanafunzi, wavulana na wasichana.

Kutokana na umuhimu wa shule hiyo, serikali ilitoa sh. milioni 250 kwa ajili ya ukarabati wa madarasa chakavu, kazi ambayo bado inaendelea. Serikali iliutaka uongozi wa Manispaa ya Musoma kuhakikisha kuwa, ukarabati wa majengo utakaofanyika shuleni hapo, hauharibu mandhari na majengo ya kumbukumbu, hasa yale yaliyotumiwa na Baba wa Taifa.

No comments:

Post a Comment